Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACKLINE K. ANDREA Aliuliza:- Je, Serikali imeweka mpango gani wa elimu ya sheria ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda ili waendeshe kwa kutii sheria na kuepusha ajali?

Supplementary Question 1

MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba tunajua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inajitahidi kupunguza ajali za bodaboda, tukiangalia kwa mwaka 2019 tulikuwa na ajali 567 lakini mwaka 2020 tuna 240. Je, Jeshi la Polisi lina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizi zinapungua zaidi? Tukiangalia wahanga wakubwa ni vijana na wanawake ndiyo wanaopata shida ya kupoteza vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; utafiti unaonyesha askari wastaafu wanachelewa kupata mafao yao, je, Wizara husika ina mpango gani wa kuhakikisha askari hawa baada ya kustaafu wanapatiwa mafao yao kwa haraka ili kuepusha wanapokuwa kazini kuchukua rushwa ili kujilimbikizia akiba?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi inaonekana Mheshimiwa tumempa sababu moja au njia moja ambayo tunaweza tukaitumia katika kuepuka hizi ajali. Zipo njia ambazo tumeshazichukua kama Serikali na nyingine tuko mbioni kuzichukua kwa kushirikiana na Wizara nyingine au kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba hizi ajali za barabarani zinapungua. Cha kwanza tumefikiria kuendelea kuwafundisha zaidi hasa vijana wa bodaboda namna ya kutumia alama za barabarani ambazo zina uwezo mzuri wa kuwaeleza kwamba wanakoelekea wanaweza wakapata ajali.

Mheshimiwa Spika, lingine tuna mpango sasa wa kutengeneza mfumo wa kufunga au ku-control ajali kwa kutumia vidhibiti mwendo, ambapo tunahisi hivi vinaweza kupunguza ajali. Pia tuna mpango wa kufanya marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda moja kwa moja kwenye masuala ya faini na adhabu katika mambo haya ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie pia kuwaelimisha vijana kwa sababu naamini katika mkoa wake vijana wa bodaboda wapo, basi azidi kuwaelimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu mafao ya Askari. Kwa kweli Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunawalipa wastaafu posho zao mara tu baada ya wao kustaafu. Katika kipindi cha 2018/2019 tumejitahidi kati ya wastaafu 591; jumla ya wastaafu 479 tayari tulishawapatia mafao yao na sasa hivi wengi wanaishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kinachokuwa kinatukabili kama sehemu ya changamoto, inafika wakati inakuwa OC nazo na bajeti nayo inakuwa mtihani, kwa hiyo, ndiyo maana kuna wakati wanachelewa kidogo kulipwa. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama itakuwa kuna mtu ambaye hajapata mafao yake na amestaafu, basi tukitoka hapa tuonane, tuone tunamsaidia vipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACKLINE K. ANDREA Aliuliza:- Je, Serikali imeweka mpango gani wa elimu ya sheria ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda ili waendeshe kwa kutii sheria na kuepusha ajali?

Supplementary Question 2

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la msingi la ajali za barabarani kwa bodaboda na vyombo vingine vya usafiri. Tatizo hili ni Kitengo cha Usalama Barabarani kugeuza kitengo hiki kama chanzo cha mapato. Watu wanakwepa matrafiki, wanakimbia kwa sababu ukikamatwa hakuna onyo, ni faini. Bodaboda siku hizi wanakamatwa kwa kukimbizana na trafiki. Nadhani hii inasababishwa na uzee wa sheria hii ni ya mwaka 1973. Ni lini Serikali italeta mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ili tufungue mjadala wa namna gani tutaiboresha ili kupunguza ajali za barabarani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDAIN YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Salome, Muswada huu uko njiani, muda wowote tutauleta tuje tuujadili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya mabadiliko ya baadhi ya sheria hizi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, tuko mbioni kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.