Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Primary Question

MHE. JULIUS K. LAIZER aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA kama ilivyoahidi katika vijiji vya Munjere, Baraka, Mbaasha, Lepurko, Mti Mmoja, Arkatan, Arkaria, Mfereji, Ndonyonaado, Mswakini, Naitolia, Emurua, Lashaine, Orkenswa, Engaaroji, Oldonyolengai na Naalarami? (b) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Shule ya Sekondari Oldonyolengai ambayo laini imefika tangu mwaka 2015 lakini mpaka sasa umeme haujawaka?

Supplementary Question 1

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na kwa kweli nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri kwa sababu katika Wilaya ya Monduli vijiji vilivyokuwa vimepatiwa umeme peke yake vilikuwa 16 na sasa karibu vijiji vyote 64 vitaingizwa kwenye awamu ya tatu. Lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo kubwa la REA katika maeneo mengi ni kwamba umeme unafika kwenye kijiji lakini vitongoji na maeneo mengi ya wananchi umeme ule haufiki.

Je, nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo umeme haujafikia japo inaonekana kijiji kimefikiwa umeme unaweza kupelekwa kwa wananchi kuliko kuwa na umeme ambao umefika kijijini lakini wananchi hawajapata umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili katika Kata ya Engaruka katika Shule ya Oldonyolengai tayari laini kubwa imefika ni kazi ya kuunganisha tu katika shule ya msingi Engaruka Juu na katika zahanati ya Oldonyolengai. Je, nini kauli ya Serikali kwa mkandarasi aliyoko site ili aweze kuunganisha umeme katika maeneo hayo?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Julius na kwa niaba yake napokea pongezi zake kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Mkoa wa Arusha na maeneo mbalimbali na pia nimpongeze Mheshimiwa Julius kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika jimbo lake la Monduli.

Mheshimiwa Spika, kama alivyouliza na nakiri ndani ya Bunge lako kweli miradi hii ya umeme inayoendelea REA awamu ya tatu au na REA awamu mbalimbali kazi yake ya msingi ya kwanza ni kufikisha miundombinu ya umeme mkubwa katika baadhi ya maeneo kwenye vijiji.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo na ndio maana Serikali yetu ya Awamu ya Tano imebuni mradi wa ujazilizi awamu ya kwanza ambao ulifanyika katika mikoa 8 na tumepata mafanikio makubwa wateja takribani 30 wamepatiwa umeme katika vijiji 305. Mpango unaoendelea sasa hivi ni Ujazilizi Awamu ya Pili A kwenye mikoa tisa ikiwemo Mkoa wa Arusha pia Mkoa wa Mwanza, manispaa za Ilemela na Nyamagana na maeneo mbalimbali. Sambamba na hilo katika mradi huu wa REA wa Ujazilizi Awamu ya Pili takribani Bunge lako tukufu limetupitishia pesa shilingi bilioni 169 ambayo inaenda kuwezesha wateja wa awali 60,000 kuunganishiwa umeme.

Kwa hiyo, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa bajeti imeshapita tunawaahidi kwamba tutaendelea kuisimamia ili vitongoji vyote viendelee kuunganishwa lakini kwa kweli kazi kubwa kwanza ni kufikisha umeme katika maeneo ya makao makuu ya vijiji kasha usambazaji ni jambo endelevu. Pia naomba niseme taarifa ya ziada tumeielekeza TANESCO wamebaini maeneo 754 ambayo yamepitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa na pale kazi kubwa itakuwa ni kuweka transfoma na kushusha huo umeme na kwa kuwa tumeamua TANESCO, REA yote ishambulie na ndio maana Serikali imefanya maamuzi ya makusudi ya kisera kufanya kwamba bei ya kuunganishia umeme 27,000.

Mheshimiwa Spika, naomba nikutaarifu na Bunge lako juzi tulikuwa na mkutano mkubwa na tutaanza kuzindua wateja wanaounganishwa kwa bei shilingi 27,000 na tunaanza Wilaya ya Kondoa wameshaunganishwa wananchi 500 baada ya uamuzi wa Serikali. Kwa hiyo, niwatoe hofu wananchi wote na vitongoji ambavyo hawajaguswa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ameelezea masuala ya kwa kuwa laini kubwa imefika katika Kata ya Engaruka, ameuliza; Serikali inatoa maelekezo gani kwa mkandarasi ambaye ni NIPO Group aliyeko katika Mkoa wa Arusha. Juzi mkutano wetu baina ya REA na TANESCO tumeendelea kutoa msisitizo umuhimu wa kuunganisha taasisi za umma katika miradi inayoendelea.

Kwa kuwa TANESCO tumeipa mamlaka sasa na wao kuendelea kusambaza umeme vijijini kwa bei ya shilingi 27,000 na kwa kuwa imetenga shilingi bilioni 40 na Bunge mmeidhinisha ni wazi maeneo haya ya taasisi za umma yatafikiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, REA na TANESCO wataendelea kushambulia maeneo mbalimbali ili kukamilisha na watanzania wapate fursa ya kutumia umeme kwa bei nafuu ikiwa ni azma ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Ahsante sana.