Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Mabweni katika shule za sekondari zilizoanzishwa Kitarafa ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu iliyo bora Mkoani Shinyanga?

Supplementary Question 1

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali ya nyongeza. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaifanya katika kuhakikisha inaboresha miundombinu katika shule zetu. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha inajenga mabweni katika shule zetu zilizoanzishwa kimkakati zaidi katika shule ya sekondari Samuye, Kizumbi, Isagenhe na Ukenyenge zilizopo katika Mkoa wa Shinyanga kwa sababu Wanafunzi wamekuwa wakitembea umbali mrefu na hivyo kukumbana na vishawishi vingi barabarani na kupelekea kupanga mitaani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Je, Serikali hamuoni sasa ni wakati muafaka wa kuweza kufikiria kutokuwapangia shule zilizoko mbali wanafunzi hawa kwa kuwa kila Kata sasa hivi ina shule?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikiri, Mheshimiwa Azza takribani wiki mbili au tatu zilizopita alikuwa akinijulisha suala zima la changamoto ya miundombinu ya elimu katika Mkoa ule wa Shinyanga na nilimuhakikishia kwamba Serikali tutafanya kila liwezekanalo, lile linalowezekana tutaenda kulifanyia kazi alichanganye pamoja na ajenda hiyo ya elimu pamoja na ajenda ya afya.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo naomba niseme kwamba Serikali tutaangalia kila kinachowezekana katika maeneo uliyoyaainisha lile litakalowezekana kwa sasa tutaweza kulifanya. Lakini ni azma ya Serikali kuhakikisha tunapambana miundombinu inaimarika kama tulivyofanya pale sekondari ya Tinde ambapo Mbunge tumeenda wote pamoja pale kwa ajili ya kuona eneo gani lazima tufanye hilo.

Mheshimiwa Spika, suala la kutowapangia mbali kwa vile kila Kata sasa ina shule, jambo hili ndiyo kielelezo chetu ni kwamba kama katika Kata hasa zile zetu ambapo kama kuna vijana wamefaulu katika eneo lile ni vyema sasa watoto wakapangiwa kwa karibu zaidi kuepusha usumbufu huo mabao Mheshimiwa Mbunge ulizungumza. Kwa hiyo, tumelichukua Serikali na tutalitolea maelekezo katika maeneo mbalimbali.

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Mabweni katika shule za sekondari zilizoanzishwa Kitarafa ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu iliyo bora Mkoani Shinyanga?

Supplementary Question 2

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba wanajenga mabweni, utakubaliana nami kwamba baadhi ya mabweni hayo yamekuwa yakiungua mara kwa mara na hivi karibuni shule ya Ashira mabweni yake mawili ya wasichana yameungua.

Je, Serikali mna utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na ulinzi katika shule hizo ili hii rasilimali kubwa ambayo imeshatumika ya fedha kujenga mabweni hayo iweze kulindwa?

Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Dada yangu Susan.

Mheshimiwa Spika, ni kweli na niwape pole Wananchi wote wa Tanzania kwa sababu watoto wale, juzi nilikuwepo Ashira ile shule wkeli imeungua lakini ukija kuangalia taarifa ya awali inaonyesha kwamba ni hujuma tu kwa sababu yale mabweni mawili hayaungani na siyo kwamba kulikuwa na short ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli inawezekana maeneo mengine kuna hujuma na nawaomba niwaeleze Serikali juzi nilisha-deploy timu yangu ya Mainjinia iko pale tokea jana inafanyakazi na leo hii haraka iwezekanavyo ndani ya wiki mbili, tatu tuanze ukarabati wa yale majengo kwa sababu siyo muda mrefu vijana wa form five wengine tutawaingiza katika maeneo yale. Kwa hiyo, tutafanya ukarabati wa shule ile yote kwa ujumla wake kuhakikisha inarudi Ashira katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo ni maelekezo yetu sasa kipaumbele suala zima la walinzi na hasa kuangalia usalama wa shule zetu nini kifanyike kwa sababu tunatumia fedha nyingi sana, haiwezekani watu wenye nia mbaya wakahujumu juhudi hii kubwa ya Serikali na Wananchi wake kwa ujumla.