Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:- Wafanyakazi wa Kiwanda cha MUTEX ambacho kilifungwa tangu mwaka 1984, wamekuja kulipwa stahiki zao Disemba, 2018 na badala ya kulipwa shilingi 400,000/= kwa gharama ya kila mwezi wakalipwa shilingi 100,000 tu:- Je, Serikali haioni kuwa inawakandamiza wastaafu hao?

Supplementary Question 1

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante, niseme tu, sawa majibu ni marefu lakini hayajaniridhisha. Kwa mujibu wa sheria Mfilisi anapofilisi kiwanda au anaponunua kiwanda ni lazima kuwalipa wafanyakazi wote malimbikizo ya madai yao yote. Je, ni sahihi madeni ya msingi ya wale wananchi yapotee bure?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; hivi Serikali ilichukua hatua gani ili kwa aliyenunua kile kiwanda kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wale stahili zao zote toka shilingi 400,000, hatimaye wakawalipa laki moja, zile laki tatu zitalipwa lini? Ahsante.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba Serikali haiko tayari kuona Mtanzania yeyote wa aina yeyote akipoteza stahiki zake mahali popote ndiyo maana kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwa urefu jitihada zote ambazo Serikali imechukua kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za ufilisi. Kwa hiyo, hakuna Mtanzania yeyote au mtumishi yeyote wa kiwanda hiki ambaye stahiki zake zitapotea.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza wazi; watumishi 512 walilipwa tangu mwaka 1994 kulingana na sheria, kanuni na taratibu zinavyoelekeza, hawa waliokataa wamekwenda mahakamani zaidi ya mara mbili na wote mahakamani walikokwenda malalamiko yao yametupiliwa mbali, wameelekezwa kurudi kwa mfilisi. Ni mfilisi ndio anayetoa fedha hizi za kulipa baada ya kuwa ameshalipa madeni mbalimbali ambayo kiwanda hiki kilikuwa kinadaiwa, kinachobaki ndicho wanacholipwa watumishi hawa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza aliyenunua kiwanda hiki anatakiwa kulipa. Kulinaganga na sheria na kanuni na taratibu za ufilisi anayetakiwa kulipa siyo aliyenunua kiwanda, aliyetakiwa kulipa ni Serikali kwa sababu Serikali ndiyo iliyokuwa inamiliki kiwanda hiki na ndiyo maana mpaka leo Ofisi ya Msajili wa Hazina inashughulikia watumishi 312 waliobaki ili wakiwa tayari waweze kulipwa shilingi milioni 20 kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi. Kwa hiyo aliyenunua kiwanda hiki hana liability yoyote ya kuwalipa watumishi hawa na Serikali tuko tayari kuwalipa kwa wakati wowote.