Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Primary Question

MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK aliuliza:- Tanzania ina jumla ya Majiji sita likiwemo Jiji la Tanga; katika Majiji hayo kuna maeneo ambayo yako nje ya Jiji ambayo ni Mitaa, Vitongoji na Vijiji (Perry Urban); Kitengo cha Perry Urban kimekabidhiwa jukumu la kusambaza umeme wa REA III katika Majiji:- Je, ni lini Perry Urban itaanza kusambaza umeme katika Jiji la Tanga?

Supplementary Question 1

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini pamekuwa na malalamiko katika yale maeneo ambayo yameshapelekewa transfoma za Kilovolt 50. Je, tatizo hili kwa nini linajirudia tena? Kuna baadhi ya maeneo yametajwa kwamba katika transifoma 35, transifoma saba za KV 50 halafu kuna transifoma nyingine nne. Kwa nini tusipeleke zile ambazo ni za kuanzia KV 100?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili katika taarifa hii haikuainisha baadhi ya maeneo ambayo ndiyo hasa yaliyokusudiwa. Kwa mfano, kwenye Kata ya Kirare kina maeneo ya Mapojoni, Mtambuuni, Msakangoto, Kirombere lakini kwenye Kata ya Mzizima kuna maeneo ya Kihongwe, Rubawa, Mleni, kwenye kata ya Kiomoni kuna maeneo ya Pande Muheza, Pande Masaini, Pande Mpirani, Kata ya Marungu kuna Mkembe, Geza Ndani na Geza Barabarani; Pongwe kuna maeneo ya Pikinangwe; na Kata ya Maweni kuna Machembe, Mtakuja na Mwisho wa Shamba: Je, maeneo haya sasa hususan noyo yamo katika huu mradi na lini hasa yataanza kufanyiwa huu uwekezaji wa REA III? (Makofi)

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli yako maeneo ambayo tulikuwa tukipeleka transfoma za KV 50 na nyingine 100 na 200 na kuendelea, lakini maeneo tunayopeleka KV 50 inategemea pia na uwekezaji na aina ya wateja. Ziko faida nyingi sana za kupeleka transfoma ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo na hasa katika kukabiliana na uharibifu wa mitambo inapotokea dharura. Kunapokuwa na transfoma za 50 nyingi, kwa hiyo, kunapokuwa na dharura ya kuharibika transifoma moja, wateja wengine wanaendelea kupata umeme bila matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hasara za kuwa na transifoma moja kubwa, ni kwamba ikishaharibika wateja wengi wanakosa umeme, lakini tumelichukua ombi la Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kusambaza transifoma za kila aina kukabiliana na hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili katika Jiji la Tanga tunayo maeneo 12 yatakayopelekewa umeme wa Perry Urban ikiwemo kama alivyotaja maeneo yake, lakini yako maeneo ya Chongoleani, Mabwakweni, Majani Mapana na maeneo mengine mpaka 12 na utekelezaji unaanza Julai mwakani na kukamilika mwezi Desemba, 2021. (Makofi)