Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Ugonjwa wa Mguu Kifundo unatibika katika Hospitali ya Rufaa Kitete – Mkoani Tabora ambapo hupokea zaidi ya Watoto 40 wenye tatizo hilo kila mwezi:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa vya kutosha kama vile POP, bandeji, pamba, kiatu na gongo-pinde ili kusaidia watoto hao? (b) Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo kwa watoto Mkoani Tabora na familia nyingi hazina uwezo wa kufika Hospitali kupata huduma; je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ili watoto wengi zaidi waweze kupata huduma hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Waziri amesema kwamba ugonjwa huu ni tatizo kubwa nchini lakini katika Mkoa wa Tabora hasa Wilaya za Sikonge, Kaliua pamoja na Uyui umekuwa ni mkubwa zaidi hadi kusababisha kila siku watoto 40 kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete. Watoto hawa ni wengi sana na ndiyo hawa ambao wamejitokeza kuja hospitalini, hatujui hawa ambao hawajaja hospitalini. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wazazi kuhusu ugonjwa huu wa mguu kifundo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Daktari aliyepo katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete yupo tayari kufanya kliniki kwenye Wilaya hizi ili angalau kuwafuata wazazi ambao hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao Kitete?

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti kidogo ili Daktari huyu aweze kufika kwenye Wilaya hizi na kuweza kutibu watoto wetu? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge kutoka Mkoa wa Tabora, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba mguu kifundo kwa lugha ya kitaalam tunaita Talipes ni ugonjwa ambao hutokea kwa baadhi ya watoto; mmoja kati ya watoto 1,000. Niseme tu kwamba mtoto akibainika mapema anaweza akapata matibabu na zaidi ya asilimia 80 ya hawa watoto miguu hurejea kuwa katika hali ya kawaida. Nitumie fursa hii kuongea na jamii ya Watanzania kusema kwamba wazazi wote ambao wana watoto ambao wana tatizo hili la mguu kifundo wawafikishe katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya ili waweze kupata huduma za utengamao. Kama nilivyosema hapo awali, ugonjwa huu unaweza ukatibika kwa kutumia utaratibu wa hizi huduma za utengamao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, sisi kama Wizara hatuna shida kama tuna mtaalam pale katika hospitali yetu ya Kitete kumpa usaidizi ili kuweza kufanya kliniki katika Wilaya zote. Hili Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukakaa tukaangalia utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba hii huduma inaweza ikapatikana katika Wilaya nyingine ambapo si rahisi kufika katika hospitali yetu ya Kitete pale Tabora.