Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wananchi wa Wilaya ya Lushoto wamejitahidi kujenga maboma mengi ya maabara lakini mpaka sasa Serikali haijawaunga mkono:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kumalizia maboma haya?

Supplementary Question 1

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Hata hivyo, kabla ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wa Wilaya ya Lushoto kwa mvua zinazoendelea kunyesha takriban sasa ni miezi minne bila kujua zitaisha lini. Niwatoe hofu kwamba taarifa za mvua zimefika sehemu husika, ni imani yangu kubwa sasa kwamba baada ya mvua kupungua miundombinu ile itarejeshwa na wananchi watapata huduma kama ilivyokuwa awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mwili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze kwa majibu mazuri Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kusema kuwa ametupatia fedha za maabara, ni kweli. Hata hivyo, kuna shule nyingi sana katika Wilaya ya Lushoto zaidi ya 50 lakini zenye maabara hazifiki sita. Kwa nini sasa Serikali isitumie mfumo kama ule wa mwaka jana wa kutoa fedha za kukarabati maboma ya madarasa ili kukarabati maabara kuepusha usumbufu kwa wanafunzi wetu hasa wasichana ambapo tutaepusha mimba za utotoni?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Jimbo la Lushoto lina sekondari nyingi sana zaidi ya 28 lakini zenye hosteli naamini hata tatu hazifiki. Je, kwa nini sasa Serikali isitupe hata fedha kwa mwaka huu ili kukarabati maboma ya hosteli ambayo yameshajengwa kwa nguvu za wananchi mfano Mlongwema…

SPIKA: Mheshimiwa Shekilindi nafikiri umeeleweka, majibu ya maswali hayo Mheshimiwa Naibu Waziri.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza umeona Mheshimiwa Mbunge amehemewa, mimi nimeenda Lushoto pamoja na kwa Mheshimiwa Shangazi ni kweli wana shule nyingi na wanajenga kwa nguvu za wananchi. Nawapongeza sana Mheshimiwa Shekilindi na Mheshimiwa Shangazi kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika kupeleka elimu katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimetembelea baadhi ya maboma ya maabara ambayo kwa kweli hayajakamilika. Maombi ya Mheshimiwa Mbunge tumeyapokea, Serikali ina mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapata maabara katika kila shule ya sekondari kwa sababu ni lazima tuwe na masomo ya sayansi ambayo yanafundishwa kwa vitendo na siyo nadharia.

Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ya mwaka huu na bajeti ambayo tunaendelea nayo, nimhakikishie kwamba katika maombi ambayo ameshayaleta pale ofisini tutayafanyia kazi, hawezi kukosa baadhi ya maabara ambazo zitakamilika. Hatujengi maabara tu, tunajenga maabara lakini pia kupeleka vifaa ili wanafunzi waweze kufanya mazoezi kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote mwaka huu ambao tunaendelea nao tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara na majengo mbalimbali lakini na mwaka huu ambao tunaanza mchakato wa bajeti tutatenga fedha. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge Halmashauri huko wanaendelea kutengeneza bajeti ni muhimu kwenye bajeti hii ambayo tunaenda nayo 2020/2021 tutenge fedha kuanzia vyanzo vya Halmashauri na sisi Serikali Kuu tutatafuta fedha tuwekeze pale ili tuweze kuboresha maabara, majengo ya hosteli, kumbi za mikutano na nyumba za walimu. Ahsante sana.