Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Serikali imekuwa ikiwapandisha madaraja walimu lakini haitoi malipo stahiki kwa madaraja hayo mapya kwa kipindi kirefu tangu walipopandishwa madaraja yao:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao mara wanapopandishwa madaraja?

Supplementary Question 1

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri lakini naomba kuuliza maswali mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, wapo walimu ambao mpaka wanastaafu walikuwa wako katika daraja jipya lakini mlipokuja ku-calculate mafao yao mka- calculate kwa kikokotoo cha mshahara wa zamani. Je, ni lini sasa Serikali mtaona umuhimu wa kuwalipa wastaafu hawa mapunjo yao ya mafao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pesa ya likizo na matibabu kwa walimu hawa ni takwa la kisheria kwa mujibu wa sheria za kazi lakini walimu hawa wamekuwa wakienda likizo au kwenye matibabu pasipo kupewa pesa zao kwa wakati. Je, ni lini sasa Serikali mtaona umuhimu wa kuwalipa walimu hawa pesa kwa wakati mara wanapokwenda likizo au kutibiwa? Ahsante.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Kiza maswali yake ya nyongeza mawili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua wale waliolipwa mafao yao kwa kikokotoo cha zamani, naomba nitoe maelekezo kwa waajiri wao na Maafisa Utumishi kwenye Halmashauri zetu, twende case by case walifanyie kazi halafu sisi tutashauriana namna bora ya kulishughulikia ili kuondoa changamoto na malalamiko kwa watumishi hawa.

Swali la pili, ni nia ya Serikali kuendelea kulipa watumishi wake na kuwapandisha madaraja kwa wakati. Sasa hivi tumeshafanya calculation na tumejiridhisha kwamba tuna walimu zaidi 86,000 ambao wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 43, tuna walimu wa sekondari zaidi ya 18,000 ambao wanadai karibu zaidi ya shilingi bilioni 18. Jumla ya madai ya walimu wote ya madaraja, likizo na malimbikizo mbalimbali kwa maana ya areas zao ni jumla ya zaidi ya shilingi bilioni moja. Kwa hiyo, Serikali imefanya utafiti na uhakiki sasa tunafanya mchakato wa kutafuta fedha ili walimu wetu waweze kulipwa madai yao na kupunguza malalamiko ambayo kwa kweli ni mengi sana. Ahsante.