Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:- Katika Jimbo la Mpwapwa Vijiji vya Mkanana, Nalamilo, Kiboriani, Igoji Kaskazini, Mbori, Tambi, Nana, Majani (Mwenzele), Mafuto, Kiegea, Kazania, Chimaligo, Mbugani, Chilembe, Mazaza, Mwanjili, (Makutupora) na Chibwegele havina huduma ya umeme:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia huduma ya umeme vijiji hivyo?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa line inayopeleka umeme Wilaya ya Mpwapwa inahudumia pia Wilaya za Chamwino, Kongwa, Gairo na Mpwapwa yenyewe na hivi karibuni line hiyo imeongezwa Tarafa ya Mwitikila, Mpwayungu na Nagulo. Kwa hiyo, line hii imekuwa overloaded na kusababisha kukatikakatika kwa umeme katika Mji wa Mpwapwa. Je, mko tayari kujenga line mpya ya umeme kuanzia Zuzu Main Station itakayopita Kikombo Station, Kiegea mpaka Mbande ambako mtajenga substation na pale ijengwe line moja kwa moja kuelekea Mpwapwa itakayojulikana kama Mpwapwa fider?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Mima, Sazima, Igoji Mbili, Isalaza, Chamanda na Iwondo tayari vinapata huduma ya umeme lakini mkandarasi aliruka Kijiji cha Igoji Moja na tatizo la sasa ni transfoma. Je, uko tayari kupeleka transfoma katika Kijiji cha Igoji Moja ili wananchi wa pale waweze kupata huduma ya umeme?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwa kufuatilia masuala ya nishati kwa wananchi wa Mpwapwa, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje la kwanza, ni kweli umeme unaokwenda Mpwapwa unatoka Zuzu ambapo ni umbali wa kilomita 120 ni mbali sana. Mpango uliopo ni kwamba sasa hivi Serikali kupitia TANESCO tumeanza utekelezaji wa kujenga line mpya ya kutoka Zuzu kupita Kikombo ambapo ni kilomita takribani 42 na kutoka Kikomo mpaka Msalato kilomita 45 lakini kwenda Mpwapwa tutatoa sasa Kikombo kupita Kiegea kutoka Kiegea tunajenga substation Mbande na pale Mbande kwenda mpaka Mpwapwa itakuwa takribani kilomita 70. Kwa hiyo, wananchi wa Mpwapwa sasa wataanza kupata umeme kutoka Mbande ambao utakuwa ni mkubwa kuweza kuwahudumia wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili, ni kweli tumepeleka umeme kwenye vijiji takribani 32 Mpwapwa lakini viko vijiji vya Mkanana, Mbande pamoja na maeneo aliyoyataja kama Igoji Moja au Igoji Kaskazini, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge Igoji Kaskazini au Igoji Moja wakandarasi wameanza kazi tangu juzi na kufikia Jumapili ijayo watawasha umeme na watafunga transfoma nne za kilovoti 50 na kilomita zingine mbili wataweka na kufunga transfoma mbili za kilovoti 120 na wataunganisha wateja wa awali 78 wa phase one na wateja 9 wa phase three. Kwa hiyo, Igoji itakwenda kuwashwa umeme Jumapili ijayo. Nashukuru sana.