Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:- Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni cha muda mrefu na pia kimetumika kuandaa viongozi wa nchi yetu na nchi jirani:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hicho kuwa Chuo Kikuu? (b) Je, kwa nini Serikali haipeleki fedha za maendelo katika Chuo hicho kama zilivyopangwa?

Supplementary Question 1

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Chuo hiki cha Mwalimu Nyerere kilijengwa na Wazalendo wa nchi hii, tena kabla ya Uhuru na Mwalimu Nyerere alikipa jina ya Kivukoni lenye maana ya eneo lililopo Chuo kilipo. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hiki kuwa Chuo Kikuu, ili tumuenzi Baba wa Taifa, ukizingatia kwamba Barani Afrika kuna nchi nyingi ambazo wamezipa majina ya Waasisi kama Mandela South Africa, Kenyata Kenya lakini Nkurumah Ghana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Chuo hiki, Mheshimiwa Waziri kuna bweni ambalo limejengwa toka mwaka 2013 kwa ajili ya wanafunzi hawa wa Shahada ya Uzamivu, lakini mpaka sasa halijakamilika. Je, ni kwa nini halijakamilika na ni lini litakamilika na nini kauli ya Serikali katika kukamilisha bweni hilo. Ahsante.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza linaenda kwenye majibu ya swali langu la msingi, tumesema mpango wa Serikali kwa sasa si kupandisha hadhi Vyuo. Vilevile tukubaliane kwamba ili kupandisha Chuo kuwa na level ya Chuo Kikuu, kuna vitu vingi inabidi kuzingatia, kwanza inabidi uunde Kikosi kazi cha Wataalam waende wapitie Mitaala, aina ya Walimu kama wanatosha, eneo lenyewe Hatimiliki ya eneo lao. Kwa hiyo kuna vitu vingi vya kuangalia, lakini kwa sababu tunazungumza kuna vitu vingi vya kufanya, tumesema tuboreshe hivi vilivyopo, itakapofika wakati, Serikali ikaona haja ya kufanya hivyo, tutafanya hivyo kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi ambazo zimewekwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anasema kuna bweni ambalo halijakamilika, naomba hili tulichukue tulifanyie kazi, lakini kwa kweli kama kuna bweni lipo pale na kuna upungufu wa mabweni, tutafanyia kazi ili liweze kukamilika.

Name

Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:- Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni cha muda mrefu na pia kimetumika kuandaa viongozi wa nchi yetu na nchi jirani:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hicho kuwa Chuo Kikuu? (b) Je, kwa nini Serikali haipeleki fedha za maendelo katika Chuo hicho kama zilivyopangwa?

Supplementary Question 2

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, wote tunatambua jambo kubwa linalotuweka Watanzania pamoja ni kutokuwa na ubaguzi, lakini mikopo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu imekuwa ikitolewa kwa ubaguzi. Mfano, mimi nimepata division one nasoma Feza, mwenzangu kapata division one anasoma Msalato, atakayepewa mkopo ni yule anayetoka Msalato kwa maana ya kwamba wa Feza ni wa kishua, wa Msalato ni maskini, huu ni ubaguzi wa hali juu, tunajua hustles zinazotumiwa na wazazi kuwapeleka watoto wao shule nzuri tu na si kwamba wana pesa nyingi sana. Je, Wizara itakubaliana na mimi umefika wakati sasa wa kubadilisha kigezo cha kupata mikopo na kigezo kikuu kiwe ni ufaulu wa mwanafunzi badala ya kwamba huyu ana mahitaji zaidi ya mwenzie? Nashukuru.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Halima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vigezo vilivyowekwa ni hasa vinazingatia hali halisi ya uhitaji wa mwanafunzi kwamba mwanafunzi mwingine hana uwezo. Kwa hiyo kama hana uwezo ndiyo atakayesaidiwa kwanza.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:- Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni cha muda mrefu na pia kimetumika kuandaa viongozi wa nchi yetu na nchi jirani:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hicho kuwa Chuo Kikuu? (b) Je, kwa nini Serikali haipeleki fedha za maendelo katika Chuo hicho kama zilivyopangwa?

Supplementary Question 3

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya msingi, kwenye swali la Kivukoni, mimi ni moja ya product ya Kivukoni. Kwa kuwa historia ya Chuo hiki kilikuwa ni Chuo cha ku-train Viongozi na kutokana na changamoto tunazoziona katika utekelezaji wa majukumu yao hasa Viongozi kwenye Local Government, wilayani, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa.

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kukirudishia chuo hiki kazi yake ya msingi ya kufundisha viongozi skills za namna ya kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao na nakubaliana na uamuzi wa Serikali wa kutokukipandisha hadhi badala yake tukibadilishie sasa majukumu kitoke kwenye ku-train social sciences kiende
kwenye ku-train viongozi wetu kwa sababu kwa kweli changamoto ya utekelezaji wa majukumu yao kwenye maeneo yao imekuwa ni kubwa sana?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NASERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba nimjibu Mheshimiwa Nape Nnauye swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba Chuo hiki kimeanzishwa kwa majukumu aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge na yataendelea kufanyika hivyo, sasa kama kuna upungufu umeonekana, hilo ni jambo la kulichukua na kwenda kulifanyia kazi, lakini tunaamini kwamba kazi ya msingi iliyoanzishwa kwayo inaendelea kufanyika. Ahsante.