Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Wachimbaji wadogo wadogo wa madini nchini wamekuwa wakipoteza maisha mara kwa mara kwenye mgodi:- Je, ni lini Serikali itawapatia zana za kisasa pamoja na elimu ya kutosha wachimbaji hao?

Supplementary Question 1

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wachimbaji wadogo wadogo wanachangia sana pato la Taifa kwa kulipa kodi na Wizara ya Madini kwa kuongeza kukusanya maduhuli. Je, Serikali ina mikakati gani kurudisha maduhuli haya katika Wizara ya Madini ili kutatua changamoto hasa hizi za wachimbaji wadogo wadogo kupata zana za kisasa za uchimbaji ili waweze kuliingizia tena Serikali pato la Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wale ambao walikopeshwa ruzuku kwenye sekta ya madini kama mikopo na wakaitumia sivyo. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha wale waliochukua mikopo ile wanachukuliwa hatua na mikopo ile kurudishwa tena kwa wachimbaji wale wadogo wadogo ili waweze kuendeleza sekta hizo za madini za wachimbaji wadogo wadogo?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wachimbaji wadogo tunawategemea sana katika kukusanya maduhuli. Wachimbaji wakubwa walikuwa wanachangia zaidi ya asilimia 95 za michango yote ambayo ilikuwa inakwenda Serikalini na wachimbaji wadogo walikuwa wanachangia asilimia 4 mpaka 5. Sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa wachimbaji wadogo, tukiwawezesha tutapata maduhuli mengi ya kutosha. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tulikuta katika Wizara ya Madini walikuwa tayari wachimbaji wadogo wanapewa ruzuku kutoka Serikalini. Ruzuku ile walipewa wanaostahili na wasiostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara ya Madini tumewafuatilia wale maafisa wote waliokuwa wanawawezesha wachimbaji wadogo wasiostahili kupata ruzuku zile. Tumeshawafuatilia na wengine tumeshawaondoa katika nafasi zao za kazi. Vilevile kwa wale wachimbaji wa madini waliopewa fedha kinyume na taratibu na hawana sifa ya kupewa fedha hizo tumewafikisha katika vyombo vya sheria na sasa hivi kuna kesi zinaendelea ziko chini ya PCCB na zingine zimepelekwa Mahakamani. Tunachotaka ni kwamba warudishe fedha hizo na tuangalie namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Nia yetu kama Serikali tunataka wachimbaji wadogo tuwawezeshe, wawe wengi kwa sababu tunatambua kabisa kwamba tukiwawezesha tutaweza kupata kipato kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tarehe 22 alikaa na wachimbaji wadogo na walizungumza changamoto zao. Changamoto nyingine ilikuwa ni za kodi ambazo tunawatoza katika uchimbaji huo. Kwa hiyo, hatua tunachukua kuangalia namna ya kuwasaidia wachimbaji hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili ni kwamba changamoto za wachimbaji zipo na sisi kama Serikali tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wachimbaji hao wadogo wanapata elimu ya kutosha katika uchimbaji huo na wanatunza kumbukumbu ili wawe na sifa za kupata mikopo katika benki na vyombo mbalimbali ambavyo vinakopesha (financial institutions) na sisi kama Serikali tutashawishi vyombo hivyo kuwakopesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.