Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:- Bandari katika mwambao wa Ziwa Nyasa kutoka moja kwenda nyingine zipo kwa umbali mrefu sana hususan upande wa Wilaya ya Ludewa; hii imekuwa ni kero kubwa kwa sababu hakuna miundombinu ya barabara ambayo ingerahisisha huduma ya usafiri:- (a) Je, ni lini Serikali itatupatia bandari katika Vijiji vya Nkanda, Nsele, Kyaghomi, Makonde na Yigha? (b) Je, ni lini huduma za usafiri wa meli zitaanza tena ili kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi waishio kandokando ya Ziwa Nyasa?

Supplementary Question 1

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kutokana na usanifu ambao unafanyika sasa na timu ya wataalam wa bandari ili eneo hili liweze kupatiwa vituo vya kushusha na kupakia abiria, je, timu hii ni lini itamaliza kazi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tayari kuna tengo la mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kujenga gati katika Bandari za Lupingu na Manda. Je, wananchi hawa ambao walipisha maeneo haya watalipwa lini fidia yao ili waendelee na shughuli nyingine? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA - NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana huduma ya usafiri wa majini lakini huduma ya usafiri wa nchi kavu. Niseme tu kwamba zoezi hili litakamilika kwa muda mfupi kwa sababu hivi ninavyozungumza wataalam wanaelekea maeneo haya na najua adha wanayoipata wananchi kule ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, litakapokuwa limekamilika, siyo lazima vijiji vyote alivyovitaja tuweze kuweka vituo vya kushusha na kupakia lakini wataweza kutambua maeneo gani ambayo yatawafanya wananchi hawa wasisafiri sehemu ndefu sana kwa ajili ya kupata huduma. Kwa hiyo, avute subira na sisi tutampa mrejesho. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo haya watoe ushirikiano ili tupate information za kutosha tuweze kukamilisha zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wale wananchi ambao wanapisha maeneo yao kwa ajili ya maendeleo na sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba fedha zikipatikana tunawalipa mara moja. Kwa sababu tunajua kwamba fidia kama itachelewa kulipwa pia huduma itachelewa kwenda kwa wananchi hawa.