Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:- Serikali iliahidi kutaifisha mashamba makubwa ya uwekezaji yasiyoendelezwa:- Je, mpaka sasa mashamba mangapi yametaifishwa?

Supplementary Question 1

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilitegemea Waziri angeniambia kwa sababu kutaifisha ni suala lingine na kuendeleza ni suala jingine, kwamba hizi ekari zaidi ya elfu 67 ambazo zimetaifishwa Serikali hii imeziendeleza vipi? Sasa maswali yangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kumekuwa na matumizi mabaya ya hii sheria ya kutaifisha mashamba. Wapo watu ambao walikuwa wakimiliki mashamba kihalali na wana hati, lakini wamenyang’anywa mashamba hayo. Wapo watu ambao walishinda hata kesi Mahakamani, lakini mashamba yao wamenyang’anywa. Ni lini Serikali hii itaacha uonevu kwa wananchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Kata ya Tungi, eneo la Kiyegeya katika Manispaa ya Morogoro tangu mwaka 1984 walikuwa wakimiliki mashamba ya Tungi Estate, lakini mwaka 2014 wananchi wamenyang’anywa mashamba yale kwa maana ya kuachia ujenzi wa Star City.
Kwa kuwa, Serikali mpaka sasa haina lengo la kuanzisha mji ule wa Star City, lakini vilevile mpaka sasa Serikali haijalipa fidia. Naomba kufahamu ni kwa nini Serikali isiwaache wananchi hawa wakaendelea na shughuli zao za kilimo?

Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko na tumekuwa tukifuatilia hata kwenye vyombo vya habari. Baadhi ya mashamba ambayo yanafutwa na wamiliki ambao wamekuwa wakilalamikia kwamba, walikuwa na mashamba hayo kwa muda mrefu, lakini wamenyang’anywa. Kwa hivyo, naomba Waziri anayafahamu vizuri, yakiwemo ya Mvomero, yakiwemo ya Hananasifu…

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali hatujataifisha mashamba. Nilimsahihisha kidogo kwenye swali lake nikasema, yaani kwa Kingereza ni revocation, revocation siyo kutaifisha. Rais anaweza akayachukua mashamba kwa manufaa ya umma, lakini hajafanya hivyo. Haya mashamba yote tuliyochukua niliyoyataja ni yale mashamba ambayo waendelezaji wamekiuka sheria.
Mheshimiwa Spika, kila mwananchi anapopewa shamba au kiwanja lazima azingatie sheria na masharti aliyopewa kwenye hati yake yameandikwa. Kama amepewa shamba kwa ajili ya mifugo, lazima alitumie kwa mifugo na alipe kodi stahili na aliendeleze. Kamishna ana uwezo wa kulipima uendelezaji wake kila mwaka ameendeleza kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, nataka kukuhakikishia mashamba haya niliyoyataja hayakutaifishwa kama anavyosema Mheshimiwa Devotha, isipokuwa wenye mashamba haya na wana hati. Ukisikia Mheshimiwa Devotha shamba limefutwa maana yake lina hati, kumbe afutiwe nani?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hawa watu wenye hati wamefutiwa kwa sababu, wamekiuka masharti ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 99, Sura 113, wakiwemo hao unaowasema, mimi siwajui, lakini hao ambao anafikiri tumewaonea, hakuna hata mwananchi mmoja ameonewa katika utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Spika, nataka kuwahimiza wamiliki wote wa mashamba nchini, mtu yeyote ambaye ana shamba amepewa, lazima afuate masharti. Kama haliendelezi, kama halipi kodi stahili, shambapori, sheria itafuata mkondo wake. Sheria inaanzia kwenye Halmashauri husika, Afisa Ardhi husika anatoa notice kwa mhusika ya siku 90 ajieleze kwa nini hatua zisichukuliwe. Wengine hawa wote hawajibu hata notice, baada ya hapo Halmashauri inapandisha zoezi hilo mpaka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na mimi nampelekea Mheshimiwa Rais anatimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Devotha Minja jambo hili wakikusikia wenye Halmashauri zao watakushangaa kweli kwa sababu wao ndiyo wamefanya, Halmashauri hizi ndiyo zimeleta maombi ya kufuta mashambapori. Nasi tutaendelea kutekeleza hili jambo na ninawahimiza Waheshimiwa Wabunge mahali popote mtakapokuta mashamba yasiyoendelezwa, bila kujali ya nani, bila kujali siasa, bila kujali mashamba haya alikuwa anamiliki mkubwa gani au mtu gani, yaleteni kwa mujibu wa sheria na sisi tutachukua hatua.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Shamba la Tungi. Shamba hili la Tungi ni la watu, linamilikiwa kwa mujibu wa sheria, lina mmiliki halali. Nataka nimwombe tu kwa sababu, maelezo haya ni mengi, nimwombe Mheshimiwa Devotha Minja aende pale kwa Mkuu wa Mkoa atampa maelezo mengi kwa sababu, mimi mwenyewe nimeshakaa na timu ya Mkoa, hawa wananchi walipelekwa tu pale kulima wakati wa siasa ya Kilimo cha Kufa na Kupona, lakini walikuwa wanalima kwenye shamba lisilo lao.
Mheshimiwa Spika, pale pana hati ya mtu na Mkuu wa Mkoa amefanya jitihada sana, Mheshimiwa Dkt. Kebwe ya kuwatetea wale wananchi na wenye shamba wamewapa ardhi wale wananchi wa pale ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa hiyo, jambo hili Serikali imeshalishughulikia.
Mheshimiwa Spika, lile la mwisho ulilotaka kuuliza ushahidi la Mvomero, anajua Mvomero kuna shamba limefutwa na naamini bado limefutwa na Mheshimiwa Rais ametimiza wajibu wake. Mashamba yote yaliyofutwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya tunawaomba watupe mapendekezo namna bora ya kuyatumia katika Wilaya zao.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuamrishi tunataka mashamba yaliyofutwa wayapange viongozi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ili wananchi wale ambao wameyachungulia kwa muda mrefu na hawana nyenzo za mashamba ya kulima waweze kugawiwa yale mashamba. Kwa hiyo, kama kuna shamba Mvomero limefutwa, namwomba Mheshimiwa Murad na Viongozi wote wa Mvomero wapange utaratibu wa kutumia lile Shamba la Mvomero lililofutwa.

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:- Serikali iliahidi kutaifisha mashamba makubwa ya uwekezaji yasiyoendelezwa:- Je, mpaka sasa mashamba mangapi yametaifishwa?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pia niruhusu nimshukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilimpelekea shida ya mpaka wa Kenya na Tanzania kule Tarakea, alikwenda kule amesaidia sana kuleta utulivu kule mpakani. Mheshimiwa Waziri namshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa sana eneo la Holili, viwanja vimegawanywa hovyohovyo, vimechukuliwa kiholela kabisa na ni tatizo la miaka zaidi ya 10. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, akipata tena nafasi, kama timu yako inaweza kwenda pale kuangalia uhalali wa namna ambavyo vile viwanja vimegawanywa kwa sababu, ni tatizo ambalo limeshindikana, Wakuu wote wa Mikoa wamejaribu wameshindwa. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Name

William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Answer

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikwenda Rombo, lakini tulikuwa na zoezi la kuangalia mpaka. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua kuweka mpaka wenye alama zinazoonekana kwa wananchi kati ya nchi ya Tanzania na Kenya, Wilaya ya Rombo ni Wilaya ya mpakani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli nilikwenda huko na nimekwenda mpaka Mkoa wa Mara na zoezi hili litazinduliwa na viongozi wa nchi hizi mbili hivi karibuni. Tumeweka mipaka ya alama mia mia, ili wananchi waweze kuona alama zile waweze kujua nchi yao ya Tanzania inaishia wapi. Kama tunavyojua kwamba, alama hizi zilikuwa zimewekwa kwa umbali wa kilometa elfu moja, mpaka elfu mbili, nyingine mpaka kilometa mia mbili mpaka mia tatu. Kwa hiyo, zilikuwa hazionekani na watu walikuwa wanaingiliana, wananchi wa upande mmoja walikuwa wanaingia upande mwingine bila kujua na wananchi wa upande mwingine walikuwa wanaingia.
Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa pongezi zake na tutaangalia hayo maeneo mengine, sina taarifa kamili hizo alizoniambia nitafurahi zaidi kama Mheshimiwa Selasini akiniandikia vizuri ili nipate message vizuri. Amezungumza kwa haraka sana lakini kwa kadri tutakavyolielewa,
tutalishughulikia. (Makofi)