Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:- Mradi wa Kilimo wa RUBADA - Rufiji, umekuwa mradi wa kitapeli ambao watu wachache wanajinufaisha na rasilimali za Rufiji bila ya Wana-Rufiji kupata maendeleo yoyote. Je, ni lini Serikali itafikiria kuleta mradi wa kilimo katika Bonde la Mto Rufiji ambalo kwa miaka mingi liko tupu bila shughuli yoyote ya kilimo hasa ikizingatiwa kuwa bonde hilo lina kila kitu?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza majibu mazuri ya dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, mchapa kazi na ninaona kabisa anakwenda kuchukua Jimbo la mtu huko Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza kabisa Rufiji tunatambua jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais za ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge kama ambavyo amelisema Mheshimiwa Naibu Waziri na kwamba tunatambua Serikali inapelekea zaidi ya shilingi trilioni mbili kwenye mradi huu na kuifanya Rufiji kuwa moto moto kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa Stiegler’s Gorge una zaidi ya ekari 150,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kilimo. Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo: Je, Serikali inawaandaaje Warufiji sasa ili kuweza kupokea fursa hizi za eneo hili la kilimo zaidi ya ekari 150,000 katika kuweka miradi mbalimbali ikiwemo na ule mradi wa kiwanda kikubwa cha sukari kule Rufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Watanzania wa Rufiji kwa asilimia 90 wanategemea kilimo na RUBADA ilikuwa katika Kata ya Mkongo pale Rufiji; na hii ndiyo kata iliyoathirika sana kwa wafugaji kuingiza mifugo yao eneo la wakulima; je, Serikali inajipangaje kuwasaidia wakulima hususan katika vijiji vya Mbunju, Ruwe pamoja na Mkongo Kusini ambao wameathirika sana kwa mazao yao kuliwa na wafugaji? (Makofi)

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza kipekee kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kwa dhati kabisa kwa maana yeye alikuwa ni sehemu mojawapo ya watu ambao walishatueleza na wakatuambia kabisa kwamba mradi huu wa RUBADA ni non-starter na yeye alikuwa ni sehemu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, kuleta na kupendekeza kwamba mradi huu wa RUBADA haufanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba naiende moja kwa moja kumjibu maswali yake madogo sana ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba sisi kama Serikali katika Bonde hili la Rufiji ni hekta 1,350 kwa ajili ya mradi wa Stiegler’s Gorge. Naomba niseme kwamba eneo la hekta 300,000 limetengwa kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizo hekta 300,000 zilizotengwa kwa ajili ya kilimo, ni kwa ajili ya irrigation scheme. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wananchi wa Rufiji na maeneo mengine yote watanufaika kwenye kilimo kupitia mradi huu ambao unaitwa irrigation scheme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lile la (b) ni kuhusu suala zima la migogoro aliyoizungumzia kuhusu ardhi. Ni kwamba Serikali tumejipanga na mpaka sasa hivi sheria inaandaliwa; tunaangalia suala zima la migogoro hii ya ardhi na maandalizi tayari yameshafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, Serikali inaandaa suala zima la ardhi kwa sababu tumegundua kwamba kuna migogoro mingi sana kati ya wakulima na wafugaji. Nakushukuru. (Makofi)