Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:- Wapo wahitimu wengi sana kutoka Vyuo mbalimbali vya Ufundi nchini ambapo hadi sasa hawajapata ajira wala hawajaweza kujiajiri, ikiwa pia tuko kwenye wakati wa kuanzisha uchumi wa viwanda ambapo taaluma za wahitimu hao zinahitajika sana:- Je, ni lini Serikali itafanya juhudi za dhati za kushughulikia suala hili kwa lengo la kuongeza tija?

Supplementary Question 1

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kupata majibu hayo ya kina ambayo yameelezea vizuri sana juu ya miradi muhimu kama hiyo REA, Standard Gauge na bomba la mafuta lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni kwa nini Serikali isije na utaratibu wa kuwachukua vijana hawa moja kwa moja kutoka kwenye vyuo ili kuwapunguzia mihangaiko ya kuzunguka na barua za maombi na kushinda mitandaoni kama ilivyokuwa kwenye sekta nyingine, mfano, afya na elimu ambapo watu hupata ajira kwa wepesi zaidi kutokana na taaluma zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Wizara hii na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ina mikakati gani kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo Incubation Centres za uhakika za kutosha, mitaji, vitendea kazi kwa wahitimu hawa ili waweze kupata wepesi wa kujiajiri na vilevile kwenda na Sera yetu ya Tanzania ya Viwanda, Inawezekana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza la kuwachukua vijana hawa wahitimu wa vyuo vya ufundi moja kwa moja, tunachokifanya kama Serikali kwanza kabisa kwa kushirikiana na sekta binafsi ambazo pindi nafasi zinapopatikana huwa tunawaunganisha moja kwa moja na vyuo vyetu vya ufundi ili vijana hawa waweze kupata nafasi za ajira za moja kwa moja. Pia baadhi ya vyuo, kwa mfano, Chuo cha Don Bosco kimekuwa kina utaratibu wa kila mwaka kuandaa Kongamano la Waajiri ambapo wamekuwa wakiunganisha wahitimu hawa moja kwa moja na waajiri na vijana wengi wameajiriwa kwa kupitia mfumo huo. Kwa hiyo, naamini kabisa wazo la Mheshimiwa Mbunge ni jema, nasi kama Serikali tutaona namna ya kuweza kuviunganisha vyuo vyetu vya ufundi pamoja na waajiri ili vijana hawa wapate nafasi za ajira za moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, suala la incubation kwa ajili ya kuwandaa vijana hawa, kuwalea na kuwapatia mitaji, sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tunavyo Vituo vya Vijana. Kipo Kituo cha Vijana Sasanda-Mbozi, Ilonga pale Kilosa na Kilimanjaro. Vituo hivi viko kwa ajili ya kuwalea vijana na kuwandaa kuwa na sifa za kuajiriwa. Pia vijana hawa wanawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana ambao umekuwa ukitoa mikopo kwa vikundi vya vijana lakini vilevile na asilimia 5 za mapato ya ndani ya Halmashauri yamekuwa yakisaidia katika kuwakomboa vijana kwa kuwapatia mitaji.

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:- Wapo wahitimu wengi sana kutoka Vyuo mbalimbali vya Ufundi nchini ambapo hadi sasa hawajapata ajira wala hawajaweza kujiajiri, ikiwa pia tuko kwenye wakati wa kuanzisha uchumi wa viwanda ambapo taaluma za wahitimu hao zinahitajika sana:- Je, ni lini Serikali itafanya juhudi za dhati za kushughulikia suala hili kwa lengo la kuongeza tija?

Supplementary Question 2

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tatizo hili la ajira halipo tu kwa wahitimu wa vyuo vya ufundi, lipo pia kwa wahitimu wengine wa vyuo vikuu hapa nchini. Kwa kuwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu tayari ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, kwa maana hiyo ni watu ambao wanaaminika. Kwa nini Ofisi ya Waziri Mkuu isishirikiane na Wizara ya Elimu kuandaa mikopo ya wahitimu ya kuanzia maisha pale ambapo wanamaliza masomo yao ili waweze kujitengenezea fedha ambazo zitasaidia kuendesha maisha yao lakini kurejesha mikopo waliyokopa wakiwa vyuoni. (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuendelea kuwakusanya vijana wahitimu wa vyuo vikuu katika makundi tofauti tofauti na mmoja mmoja ambao wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi na lengo letu ni kuweza kusaidia kufikia malengo yao. Chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunalo Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ambapo ndani ya Baraza lile tuna mifuko zaidi ya 19 inayotoa mikopo na grants. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa vijana wote nchi nzima hasa wahitimu wa vyuo vikuu wenye mawazo mbalimbali ya kibiashara, watumie fursa ya uwepo wa Mfuko wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na mifuko mingine ili waweze kujikwamua kiuchumi. Naamini kabisa kwa kutumia Baraza hili itasaidia sana wao kuweza kupata sifa ya kupata ajira lakini vilevile na kutengeneza kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili huwa napenda kutoa mfano na naomba nirudie mfano wangu, tunao vijana waliomaliza Chuo Kikuu cha Sokoine pale Morogoro ambao walipohitimu walijiunga pamoja, wakaunda kampuni, sisi kama Serikali tukawapa dhamana ya mkopo na hivi leo wanafanya kazi kubwa sana katika kilimo cha mboga mboga hapa nchini na wameanza kuwaajiri mpaka vijana wenzao. Kwa hiyo, natoa rai kwa vijana wengine wote kufuata mfano huo na inawezekana kabisa kutimiza malengo yao.