Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Serikali kupitia Kanuni mbalimbali za Utumishi inatambua mtumishi wa mke au mume na watoto au wategemezi wanne. Hata hivyo, utumishi wa umma hautambui baba wala mama hasa linapotokea tatizo la msiba, mara zote huduma ya misiba ya wazazi imekuwa ni jukumu la mtumishi mwenyewe:- Je, ni lini Serikali itawajumuisha wazazi wa mtumishi kama wanufaika wa huduma mbalimbali anazopata mtumishi wa umma?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kabla ya maswali yangu niseme jambo moja, kwanza siyo dhambi huyo mzazi kuwa na watoto zaidi ya mmoja ambao baadaye atapata hii huduma kwa sababu naye katika kuwasomesha ili watumikie Taifa hili bila shaka ametoka jasho. Kwa hiyo, kwenye jibu hilo nimeona ni jibu jepesi kwa Serikali. Sasa naenda kwenye maswali yangu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, sasa hivi tunaenda kwenye E-government hata malipo mbalimbali kiserikali tunafanya kwa njia ya mitandao, teknolojia ya mawasiliano imeendelea kukua kwa kasi. Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kufanya walau huo utambuzi ili kuwezesha watumishi ambao wanakutana na matatizo kama haya kupata huduma hiyo? Fikiria mtu amefiwa na mzazi Tunduru ampeleke Karagwe na huyu ndiyo mzaa chema mwenyewe!
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hiyo nia njema ya Serikali kuruhusu watumishi waweze kuchangiana wakipata matatizo kama hayo ni jambo jema lakini wakati mwingine, mimi nilikuwa mtumishi wa umma mifuko hiyo ina-burst, je, Serikali iko tayari japo kutenga ruzuku ndogo kuisaidia hiyo mifuko ili watumishi wakipata matatizo kama hayo waweze kupata hiyo huduma kwa wepesi zaidi? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cosato Chumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwenye swali lake la kwanza na yeye namuingiza katika Ibara ya 63(2) na (3) ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Bunge linaweza likaishauri Serikali. Kwa hiyo, kulingana na maendeleo ya TEKNOHAMA na E- government kama unavyosema upo uwezekano mkubwa sana hapo baadaye tukawa na mfumo madhubuti wenye utambuzi kwamba Bwana Joseph Kakunda ana watoto saba wameajiriwa katika sehemu mbalimbali za Serikali, amefariki Joseph Kakunda basi pengine mtoto wake wa kwanza ndiyo atabeba hilo jukumu la kupewa hayo mafao ya mazishi. Kwa hiyo, inawezekana huko baadaye hili likafanyika, tunachukua mchango wake kama maoni kwa mujibu wa Ibara hiyo ya Katiba.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuweka ruzuku kwenye mfuko. Kwanza, napenda nitoe wito kwamba ni vizuri sana kila mahali pa kazi pakawa na mahusiano mazuri, watumishi wenyewe wakawa na mahusiano mazuri wao kwa wao kwanza, kwa sababu katika baadhi ya maeneo ya kazi Mifuko hii ya Rambirambi iko vizuri sana. Hata hapa Bungeni uko Mfuko wa Faraja lakini si Wabunge wote ni wananchama. Kwa hiyo, mimi natoa wito tuanze sisi kwanza kuonesha mfano Bungeni humu Wabunge wote wawe wanachama wa Mfuko wa Faraja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile mahali pote pa kazi watumishi wajiunge katika Mifuko ya Faraja hii ya Kufa na Kuzikana ambayo ni muhimu sana. Tunauchukua ushauri tena ushauri wake kwamba baadaye tutafikiria kuweka kifungu kidogo kwa ajili ya kuunga mkono uchangishanaji ambao unafanywa na watumishi. Ahsante.

Name

Saed Ahmed Kubenea

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ubungo

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Serikali kupitia Kanuni mbalimbali za Utumishi inatambua mtumishi wa mke au mume na watoto au wategemezi wanne. Hata hivyo, utumishi wa umma hautambui baba wala mama hasa linapotokea tatizo la msiba, mara zote huduma ya misiba ya wazazi imekuwa ni jukumu la mtumishi mwenyewe:- Je, ni lini Serikali itawajumuisha wazazi wa mtumishi kama wanufaika wa huduma mbalimbali anazopata mtumishi wa umma?

Supplementary Question 2

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hoja ya msingi ni wazazi pia kuna suala la wake. Baadhi ya madhehebu ya kidini na makabila yanakuwa na mke zaidi ya mmoja. Kwa kuwa Mfuko wa Bima ya Taifa unatambua mke mmoja, je, Serikali iko tayari kuruhusu watu ambao wana wake zaidi ya mmoja waweze kuingizwa katika Mfuko wa Bima ya Taifa? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KAKUNDA):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saed Kubenea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nadhani katika nchi hii kwa sababu Serikali inatambua kwamba wananchi wake wana dini na baadhi ya dini na mila zinaruhusu mke zaidi ya mmoja, hili amelileta kama mchango wa Mbunge na ushauri kwa Serikali, wacha tulichukue kwa ajili ya kulifanyia kazi zaidi. (Makofi)

Name

Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Serikali kupitia Kanuni mbalimbali za Utumishi inatambua mtumishi wa mke au mume na watoto au wategemezi wanne. Hata hivyo, utumishi wa umma hautambui baba wala mama hasa linapotokea tatizo la msiba, mara zote huduma ya misiba ya wazazi imekuwa ni jukumu la mtumishi mwenyewe:- Je, ni lini Serikali itawajumuisha wazazi wa mtumishi kama wanufaika wa huduma mbalimbali anazopata mtumishi wa umma?

Supplementary Question 3

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa na changamoto ya wazazi wanaopata watoto ambao ni pre-mature babies, hawa watoto njiti, kupata leave inayofanana na wazazi waliojifungua kawaida. Serikali haioni kuna haja sasa akina mama watumishi wanaojifungua watoto ambao hawajatimiza muda wao wakaongezewa ile leave ili waweze kuwalea vizuri wakiwa bado ni wadogo? (Makofi)

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kusimamia haki na maslahi ya wafanyakazi kwenye maeneo tofauti ikiwemo eneo hili la afya pamoja na hili la afya ya uzazi tumekuwa na sheria mbalimbali zinazotuongoza. Sheria hizo zimekuwa zikifanyiwa mabadiliko kwa kuzingatia hali halisi ya namna nzuri ya kuweza kuwahudumia wafanyakazi. Tumeshapokea maombi ya kuangalia ni namna gani wafanyakazi wanaokumbana na hasa wanawake wanaopata matatizo ya namna moja ama nyingine kwenye kujifungua wasaidiwe.
Mheshimiwa Spika, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu pamoja na Mheshimiwa Mbunge hayo ni mambo ambayo yanaendelea kujadiliwa na kufanyiwa kazi ili kuweza kuwasaidia wanawake. Hii pia ni hata kwa wanaume ambao wake zao wamejifungua watoto ambao wamezaliwa kabla ya umri wao ili waweze kupewa haki na kusaidia malezi ya watoto na malezi ya familia kwa ujumla. (Makofi)