Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Serikali imekuwa ikitangaza kukua kwa hali ya uchumi wa nchi yetu kila mwaka:- Je, ni vigezo gani sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu?

Supplementary Question 1

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwa makini swali langu likukune mithili ya nazi na unipe jibu mfano wa tui. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nakubaliana na maelezo uliyoyatoa juu ya uanishaji wa kukua kwa uchumi wa nchi. Mheshimiwa Waziri lakini katika kipindi hiki ambacho tunashuhudia pato la Taifa likiwa limesimama la dola 976 mpaka mwaka 2016, tunashuhudia upungufu wa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, tunashuhudia bei za huduma zikitetereka mfano majengo ambapo sasa hivi yanakosa wapangaji, tunashuhudia fedha yetu ikiendelea kushuka… (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kuna uhusiano gani wowote ambao unaonesha kweli hali ya uchumi inakua wakati hali ya wananchi kukosa pesa inazidi kuongezeka miongoni mwetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nchi za kiafrika zimeingia katika mtego au mahusiano na China inayosababisha wote kukimbilia kukopa China. Jambo hili linasababisha wanaposhindwa kurejesha mikopo kukamatiwa mali zao na tayari baadhi ya nchi jirani zimeanza kukamatiwa mali zao na kudhibitiwa na China. Je, mnachukua tahadhari gani kwa nchi yetu kuja kutumbukia katika mfumo huo wa kuja kukamatiwa nchi yetu na ikawa koloni la China? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khatib Said Haji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimwambie pato la Taifa halijasimama wala halijashuka. Tumeendelea kuleta taarifa sahihi ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu ukuaji wa uchumi wa Taifa letu, tumeonyesha jinsi gani unakua na nimeonyesha vigezo hivi na kitakwimu Mheshimiwa Khatib tuwasiliane ili nikupatie takwimu ujue taifa letu linakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza amezungumzia wananchi kukosa pesa, naomba nimwambie Mheshimiwa Khatib na Bunge lako Tukufu kwamba money supply kwenye uchumi siyo kigezo cha kukua kwa uchumi wa Taifa. Money supply kwenye uchumi inaonesha kwamba Taifa hilo limeshindwa ku-control ukuaji wa uchumi wake. In short run inaweza ukajidanganya ukuaji wa uchumi upo lakini in long run matatizo na madhara yake ni makubwa sana. Nimpongeze sana Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na wataalam wake wanafanya kazi kubwa kuhakikisha hakuna pesa za ziada kwenye uchumi wetu ili tusiingie kwenye matatizo makubwa ya kiuchumi, hilo ni jibu la kwanza kwa swali la Mheshimiwa Khatib. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la pili, hizi ni speculative ambazo zipo kwenye vyombo vya habari. Napenda kumwambia kwamba kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tupo makini sana wapi tunakwenda kukopa, kwa riba ya kiasi gani na kwa nini tunakwenda kukopa. Ndiyo maana sasa hivi Bunge lako Tukufu linajadili Muswada wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma, ni umakini ule ule wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano kuhakikisha Taifa letu linakwenda kuwa salama. (Makofi)

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Serikali imekuwa ikitangaza kukua kwa hali ya uchumi wa nchi yetu kila mwaka:- Je, ni vigezo gani sahihi vinavyoainisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu?

Supplementary Question 2

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri bado anaona kwamba uchumi unakua wakati masoko ya wananchi ya mazao yao hayapo, hakuna annual increment kwa wafanyakazi, hakuna mazingira mazuri ya wafanyabiashara wetu kufanya biashara jambo ambalo limesababisha stress kwa wananchi na tumeshuhudia matukio ya watoto kuchomwa moto kwa upotevu wa Sh.2,000 na mwanafunzi kuuawa kwa sababu ya Sh.75,000…
Kwa nini bado anaona uchumi unakua wakati stress hizi zimesababisha matukio makubwa katika Taifa letu? (Makofi)

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naamini uchumi wa Taifa unakua ni kwa sababu ya takwimu na hali halisi ya uchumi wetu ulivyo.
Napenda kuliambia Bunge lako tukufu na uniruhusu nisome kipengele hiki kwenye mkutano uliokwisha mwezi uliopita wa Wakuu wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) yalisemwa haya yafuatayo kuhusu uchumi wa Taifa letu, naomba kusoma, mkutano uliombwa ku-note that the majority of member states underperformed in achieving the agreed microeconomic indicators only three member states of SADC have attained that and all these three countries is Botswana, Lesotho and Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Taifa letu unakua, watu wa nje wanaona kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania wanayaona na tupo imara tutaendelea kusimamia uchumi wa Taifa letu. (Makofi)