Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE.SHALLY J. RAYMOND (K.n.y. ANNE K. MALECELA) aliuliza: Tarafa ya Ndungu iliyoko Wilaya ya Same imesheheni uchumi mkubwa sana wa mazao ya chakula na biashara, Serikali ya Awamu ya Nne ya Chama cha Mapinduzi ililiona hilo na ikakubali kujenga barabara ya lami kutoka Mkomazi kupita Ndungu, Kisiwani hadi Same; barabara hiyo iliwekwa lami vipara vipara kwa kilomita tatu Kihurio, tano Kisiwani, tano Ndungu na tano Maore. Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kuunganisha vipande hivi ili kukamilisha barabara hii ya Mkomazi, Kisiwani hadi Same kwa kiwango cha Lami?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena. Nianze kwa kumshukuru sana Naibu Waziri aliyepata muda wa kuitembelea barabara hiyo na Mheshimiwa Anne Kilango mnamo tarehe 8 Agosti. Mheshimiwa Anne Kilango anatuma salamu na anasema ahsante sana na nadhani aliiona kazi kubwa hiyo. Pamoja na shukurani hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ni adui mkubwa sana wa barabara ya lami na baada ya mvua kila wakati vile vipande vya lami vilivyojengwa katika eneo husika zikiwemo zile kilomita tatu Kihurio, kilomita tano kisiwani, kilomita tano Ndungu zinaendelea kumomonyoka kila wakati. Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kufanya haraka kuunganisha vipande hivyo ili lami ile iliyowahi isifagiliwe kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wote wa Kilimanjaro ilionekana wazi kwamba katika vikao vya RCC Same iko nyuma sana kwenye miundombinu ya barabara na barabara iliyotajwa hapa ni barabara muhimu ambayo pia ina Mbuga za Wanyama. Je, ni lini sasa, baada ya upembuzi yakinifu Serikali iko tayari kupeleka hela hiyo mapema ili zoezi hili lifanyike kwa sababu hii ni ahadi ya Waheshimiwa wagombea Marais toka Awamu ya Nne na Awamu ya Tano? Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo anafanya kazi zake kutetea Mkoa wa Kilimanjaro na wananchi wake kwa ujumla. Swali lake la kwanza ni kweli kwamba mvua au maji ni adui mkubwa sana wa barabara zetu na hasa zile za lami na hata zile ambazo si za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la awali, kwamba baada ya usanifu wa kina kukamilika na kujua gharama tutatangaza tena tutampata mkandarasi, tukishampata mkandarasi hatua za haraka za kutafuta pesa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, sisi tunasubiri taarifa za kitaalam, zitakapokuwa tayari na kujua gharama hatutachukua muda mrefu kama Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na tutaendelea kuilinda hiyo barabara kwa pesa tulioitenga kwenye bajeti ya mwaka huu. Ahsante.