Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya Simu katika Kata za Yayeda, Ampa Arr, Tumati, Gidilim Gorati, Endaagichan na Haydere katika Jimbo la Mbulu Vijijini ili wananchi waweze kuwasiliana?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mkataba ukisainiwa utachukua miezi sita mpaka mnara ujengwe. Nina minara mitatu ambayo kimsingi imejengwa miaka miwili mpaka sasa haijamalizika, kwa mfano; mnara wa Airtel ambao uko Maga, mnara wa Halotel ambao upo Gidilim na mnara wa Halotel mwingine ambao upo Tumati haujakamilika. Je, Mheshimiwa Waziri atasaidiaje minara hii ikamilike kwa sababu Serikali imeweka fedha nyingi ili wananchi wa Mbulu vijijini wapate mawasiliano?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji ni vingi ambavyo havina mawasiliano, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja kuonja taste ya kukaa nje ya mawasiliano? Kwa mfano; Getereri, Mewadan, Migo, Harbaghe, Endadug, Eshkesh, Endamasaak, Gorad na Endamilai, yuko tayari sasa kuja ili uone hali ya mawasiliano ilivyo vibaya Mbulu Vijijini ili akatupangia vijiji hivi kupata minara?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna minara mitatu ambayo imefungwa muda mrefu na mpaka sasa haifanyi kazi ipasavyo. Kuna mnara wa Maga ambao ulijengwa na Airtel, kuna matatizo yaliyotokea kati ya wakandarasi na jamii inayozunguka eneo hilo iliyosababisha mpaka sasa hivi mgogoro ambao unaendelea kutatuliwa kwa ngazi ya kata.
Mheshimiwa Spika, nahakikisha kwamba naendelea kuwafuatilia hawa watu wa Airtel kwa sababu wao waliingia mkataba na UCSAF kwa ajili ya kupeleka mawasiliano. Masuala ya mgogoro kati ya Airtel na Kata yanatakiwa yatatuliwe miongoni mwao lakini mawasiliano ya wananchi wa maeneo ya Maga yapatikane.
Mheshimiwa Spika, vilevile eneo la Gidilim ambako Halotel wamejenga mnara kuna kama miaka miwili haujaanza kufanya kazi kutoka na Mkandarasi kutopata vifaa vya kutosha kupeleka maeneo hayo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafuatilia yote hayo pamoja na Yaeda, Ampa ambako Halotel vile vile wamefunga ili kuhakikisha kwamba hiyo minara inaanza kufanyakazi kwa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu kuambatana na yeye kuona maeneo hayo aliyoyataja. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Massay, kwa kweli anafanya kazi kwa bidii sana. Muda mwingi sana huwa tunawasiliana kuhusu masuala ya mawasiliano; na mimi kama mwenye dhamana ya mawasiliano namhakikishia kwamba Serikali tunajua umuhimu wa kuwa na mawasiliano kwa wote kwa sababu mpaka sasa hivi tuna asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana. Hatutaki wabaki hata kidogo inapofika mwisho wa mwaka huu, tunataka Watanzania wote wawe wanawasiliana. Ahsante sana.