Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Akina mama na vijana wa Jimbo la Buhigwe wanajituma sana katika kilimo na uwekezaji. (a) Je, ni lini Serikali itawasaidia kimtaji ili waweze kujikomboa? (b) Je, ni kiasi gani kimetolewa kuwawezesha akina mama na vijana katika miaka ya 2010 hadi 2017?

Supplementary Question 1

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa vikundi vingi vimehamasika na wengi wanahitaji mkopo na uwezo wa Halmashauri yetu siyo mkubwa kiasi hicho na katika Wizara mbalimbali tunazo fedha kwa ajili ya maendeleo ya vijana katika mifuko mbalimbali.
Ni lini TAMISEMI itaunganisha nguvu na Wizara nyingine ili sasa na sisi kule fedha hizo ziweze kuwafikia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kila siku tunasikia kwenye vitabu vya CAG na Wabunge wakilalamika kwamba hizi fedha haziendi kwa wananchi kutoka kwenye halmashauri. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba sheria hii ya asilimia kumi kwenda kwa akina mama, vijana na walemavu itatekelezwa kiufasaha?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza juu ya uwezo mdogo wa Halmashauri na kuitaka Serikali kuunganisha nguvu kupitia fursa tofauti tofauti, naomba nimhakikishie kama ambavyo amesema yeye mwenyewe kuna fursa kwa mikopo kwa vijana kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu ambayo iko chini ya Mheshimiwa Mhagama ni fursa ambayo ni vizuri wananchi wa Buhigwe wakaitumia katika kuweza ku-access mikopo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili juu ya halmashauri kusuasua katika kutenga asilimia 10, anataka kauli ya Serikali. Kama ambavyo nimekuwa nikisema na leo narudia hata kama ingepatikana shilingi moja kinachotakiwa ni asilimia kumi ya shilingi moja hiyo itengwe. Kama ambavyo nilishawahi kujibu hapa katika moja ya maswali wakati tunaenda kukamilisha Finance Bill kuna kipengele ambacho kitampa Waziri mwenye dhamana ili iwe ni takwa la kisheria na kama kuna Mkurugenzi yeyote atashindwa kutenga fungu hilo hatua ziweze kuchukuliwa.

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Akina mama na vijana wa Jimbo la Buhigwe wanajituma sana katika kilimo na uwekezaji. (a) Je, ni lini Serikali itawasaidia kimtaji ili waweze kujikomboa? (b) Je, ni kiasi gani kimetolewa kuwawezesha akina mama na vijana katika miaka ya 2010 hadi 2017?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Lengo la kutenga pesa hii lilikuwa ni kuwainua vijana na wanawake jambo ambalo limekuwa ni kinyume na lengo ambalo lilikusudiwa hasa pale zinapotolewa kipindi cha Mwenge. Serikali haioni kuna umuhimu wa kupeleka pesa hizi kulingana na mahitaji hasa kwa wale ambao wanajishughulisha na kilimo ikatolewa kipindi cha msimu wa kilimo? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana kwa maswali yale ya awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Aida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tumetoa maelekezo maalum kwa fedha hizi na niwasihi Waheshimiwa Wabunge, siku zote tunasema kwamba fedha hizi zinaishia katika halmashauri hata kule Hazina hazifiki. Ni jukumu la Kamati ya Fedha kila mwezi wanapofanya collection wahakikishe kama wamepata shilingi milioni 100, asilimia kumi ya shilingi milioni 100 maana yake ni shilingi milioni kumi zitolewe kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Kamati za Fedha zote, dada yangu Mheshimiwa Aida nimepata concern yako, zihakikishe wanatenga fedha hizi. Ndiyo maana katika Finance Bill ya sasa hivi tunafanya mabadiliko ya sheria katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290 ili kuhakikisha kwamba Waziri mwenye dhamana anasimamia vizuri eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wazi kwamba mtu yeyote atakaye-temper na fedha hizi ambapo kwa mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 61, kwa kweli hatutakuwa na ajizi ya aina yoyote. Hata hivyo, niwasihi Wabunge tunapokaa katika Kamati ya Fedha tuweze kuzisimamia vizuri fedha hizi kwa sababu ni jukumu letu wananchi wetu hasa vijana na akina mama waweze kupata mikopo hii.