Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. MARTHA M. MLATA – (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuwatengea eneo la kuchimba madini katika Mgodi wa Shanta ulioko Mang’onyi (Singida), wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida wanaotegemea kupata kipato kwa shughuli hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali jambo hili Mheshimiwa Tundu Lisu Mbunge wa Singida Mashariki amekuwa akilifuatia kwa muda mrefu sana, Serikali imeeleza kwamba leseni ya Shanta ni ya toka mwaka 2004...
lakini mpaka mwaka 2012 miaka nane Shanta walikuwa hawajajenga mgodi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ubaguzi nilishakuandikia muda kwamba nauliza hili swali kwa niaba…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali; la kwanza toka 2004 mpaka sasa kampuni ya Shanta haijajenga mgodi wala haijaanza kuchimba. Ni kwa nini leseni yote wasinyang’anywe wakapewa wachimbaji wadogo wakaenda kuchimba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia Mheshimiwa Rais…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Kishoa nina haki ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, naomba niendelee…
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya makinikia mwaka jana 2017 ilielezwa kwamba kampuni ya Acacia haipo kisheria…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza ni kwa nini Serikali ilipofuta leseni siku chache zilipopita haikuifutia leseni kampuni ya Acacia, kampuni ya Pangea, kampuni ya Barrick na kampuni ya Bulyanhulu kwa sababu zinadaiwa mabilioni hazijalipa na zinavunja sheria na pesa hatujapewa toka, Serikali itoe ripoti ya makinikia?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Shanta umepewa leseni siku za nyuma toka mwaka 2002 walipewa leseni ambayo ni prospect license yaani leseni ya utafiti. Baada ya pale miaka minne iyopita kampuni ya Shata ilipewa leseni ya uchimbaji yaani mining license. Walipewa mining license namba 455, 456 na 457. Leseni hizo wamepewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na leseni hizo zinadumu kwa muda wa miaka kumi; mwekezaji anatakiwa ndani ya miaka kumi aweze kujenga mgodi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi Shanta walikuwa wamekwama kutokana na kwamba kuna baadhi ya wamiliki wa ardhi yaani wenye surface areas walikuwa wamegoma kutoka, mmojawapo alikuwa ni Diwani Emili wa eneo lile. Hata hivyo, mpaka sasa hivi diwani yule na bwana mwingine ambaye alikuwa lile eneo wamekwishakubali kupewa fidia na sasa wako tayari kuondoka na wengine wako tayari kuachiwa maeneo kwa ajili ya kuwajengea wale wakazi wa maeneo yale kuwajengea nyumba za kudumu, kwa maana ya kuwaondoa lile eneo la uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwezi Novemba Shanta wataanza kujenga processing plant na vilevile wataanza kujenga TSF na vilevile wataanza kufungua lile eneo la kufanyia uchimbaji wa mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu Acacia na makinikia na kuhusu kutoa zile leseni au leseni zilizofutwa. Leseni za juzi zimefutwa na Tume ya Madini na leseni zilizofutwa siyo mining license wala siyo leseni za utafiti, zilifutwa leseni ambazo ni za kusubiria land detention license, mwekezaji anaweza akaomba leseni ya kusubiri uzalishaji kwa muda fulani. Sasa Serikali imegundua kwamba kuna watu wengine wanakaa muda mrefu na zile leseni bila kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake mwaka 2017 zile sheria baada ya kufanya marekebisho leseni za retention license zimeamua kuondolewa na zinarudishwa Serikalini na Serikali itaangalia namna bora ya kuwapa tena wawekezaji wengine ambao wako serious ili waweze kuwekeza na waweze kuzalisha ili Serikali ipate kipato na wananchi waweze kupata ajira na faida zingine Serikali, nashukuru sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nipende tu kuongezea maana yake kumekuwa na mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na wengine wanaofuatilia, wafuatilie kifungu cha (16) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake mwaka 2017 na wasome pia na kanuni ya 21(1) na (2) ya kanuni zetu za madini ya mwaka 2018 kuhusiana na mineral rights ataweza kuona ndiyo maana detention license zile 11 zimeweza kufutwa kutokana na sababu hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA M. MLATA – (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuwatengea eneo la kuchimba madini katika Mgodi wa Shanta ulioko Mang’onyi (Singida), wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida wanaotegemea kupata kipato kwa shughuli hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba hili swali la wananchi niseme ifuatavyo wa Singida. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja Itigi kufungua barabara ya Chaya-Tabora, aliwahaidi wachimbaji wote wadogo atamsimamia Shanta aweze kuwalipa fidia na nashukuru wamelipwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipeleka maombi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili wapatiwe leseni, wachimbaji hao walijiunga kwa makundi matatu ambao 1,000 wa Wilaya nzima ya Ikungi, ambao ni Dhahabu ni Mali, lakini Mang’oni Mining pamoja na Aminika na Serikali ilishapokea maombi hayo. Hivyo naomba kupatiwa majibu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mheshimiwa Mtaturu ambaye ni DC wa Ikungi. Ni lini leseni zitapelekwa na wachimbaji hawa wakapewa maeneo yao, ahsate sana. (Makofi)

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vilivyoomba hivyo vitatu alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tayari wamekwishapewa maeneo ya kuchimba, mojawapo wakiwa ni Imarika, ni kikundi chenye watu 193 walipewa dola za kimarekani milioni 25 na waliweza kununua vifaa na walianza kazi za uchimbaji. Tatizo lililotokea ni kwamba sasa hivi waliingia kwenye madeni kwa sababu walikosa yaani utaratibu mzuri wa kuweza manage pesa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunataka sasa hivi wachimbaji wote wadogo tumejipanga tutawapa maeneo mengi kwa mfano pale Muhintili tutawapa leseni zaidi ya mia moja na sabini na kitu. Hizo leseni tutawapa, lakini vilevile kama Wizara tunataka kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo waweze kuchimba kwa faida waweze kuchimba vizuri na waweze ku-manage fedha zao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivi kwa sababu tumegundua kuna tatizo kubwa la wachimbaji wanapopata fedha nyingi wanakosa ule ujuzi wa kuweza kumiliki zile fedha. Hiyo inawafanya waende kutumia vibaya na waweze kuingia kwenye umaskini tena. Hivyo tumejipanga tutatoa elimu vizuri na tutahakikisha kwamba wachimbaji wetu wanachimba kwa tija.