Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:- Liwale ni Wilaya ya zamani hapa nchini lakini hadi leo haina jengo la Mahakama zaidi ya jengo lililorithiwa toka iliyokuwa Mahakama ya Mwanzo Liwale. Je, ni lini Serikali itajenga jengo la Mahakama Liwale sambamba na nyumba za watumishi?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Awali naomba uelewe kwamba haya maswali tunayoyauliza hapa na sisi wawakilishi yanaulizwa kwa niaba ya wananchi wetu, kwa hiyo, hii ni kero ya wananchi. Sasa tunapopata majibu yasiyoridisha na majibu ambayo yana mkanganyiko, tunapata mashaka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa Septemba, 2017 niuliza swali hili na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana alitumia sekunde zisizozidi tano akaniambia Mahakama ya Wilaya ya Liwale itajengwa mwaka 2018. Sasa leo hii naambiwa itajengwa kwenye bajeti ya 2018/2019. Kwa nini wanakuwa na majibu ya kudanganya wananchi wakati sisi ni wawakilishi wao na hizi ni kero wanatupa ili wapate majibu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sambamba na Mahakama ya Wilaya ambayo nadanganywa kwamba itajengwa kwenye mwaka ujao wa bajeti, je, Serikali ina mpango gani kujenga Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Kibutuka na Makata? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma za Mahakama zinawafikia wananchi wote nchi nzima kwa ukaribu na pasipo upendeleo wowote na ndiyo maana katika bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria ameisoma hapa tumeelezea mahitaji yaliyopo na mpango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba Mahakama hizi zinajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondelee hofu Mheshimiwa Kuchauka kwamba Serikali hii si Serikali ya kudanganya kama alivyokuwa ameainisha awali Mheshimiwa Waziri na mimi pia nimesema hapa leo ni kwamba Mahakama hii itajengwa na ipo katika mpango huo kwa sababu hivi sasa tumepata nafasi ya kuwa na ushirikiano mzuri na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Nyumba la Taifa ambapo tunatumia teknolojia rahisi sana ya ujenzi wa Mahakama kupitia teknolojia ya moladi. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali ilivyoahidi, Mahakama ya Wilaya ya Liwale itajengwa. Hivi sasa navyozungumza katika mpango wa bajeti ya mwaka huu tuna mpango wa kujenga takribani Mahakama za Wilaya 29. Kwa hiyo, Mheshimiwa atupe imani, Mahakama hiyo itajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu Mahakama za Mwanzo, ni kweli ni dhamira ya Serikali kuendelea kuzijenga Mahakama za Mwanzo nyingi kadri ya upatikanaji wa fedha kwa sababu kwa hivi sasa tuna upungufu wa Mahakama za Mwanzo takribani 3,304 nchi nzima. Kwa hiyo, nimuondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi pale bajeti itakaporuhusu na fedha zitakapopatikana Mahakama hizo pia zitajengwa ili kuwafanya wananchi wa Jimbo la Liwale waweze kupata huduma ya Mahakama kwa urahisi zaidi.

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:- Liwale ni Wilaya ya zamani hapa nchini lakini hadi leo haina jengo la Mahakama zaidi ya jengo lililorithiwa toka iliyokuwa Mahakama ya Mwanzo Liwale. Je, ni lini Serikali itajenga jengo la Mahakama Liwale sambamba na nyumba za watumishi?

Supplementary Question 2

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jimbo la Liwale linafanana kabisa na Jimbo Mbulu Vijijini; katika Mji wa Haydom hakuna Mahakama ila kuna kituo kikubwa cha polisi, kwa hiyo, mahubusu inabidi wapelekwe kilometa 86 kutoka Haydom mpaka Mbulu. Je, ni lini sasa pamoja na maombi niliyoleta watajenga Mahakama katika Mji wa Haydom?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiweke commitment ya ni lini lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni mpango wa Serikali kuhakikisha tunaendelea kujenga Mahakama nyingi za Mwanzo katika nchi yetu. Kwa hiyo, pindi pale fedha zitakapopatikana pia Mahakama ya Mwanzo Haydom itaingizwa kwenye mpango ili wananchi waweze kupata huduma ya mahakama.

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:- Liwale ni Wilaya ya zamani hapa nchini lakini hadi leo haina jengo la Mahakama zaidi ya jengo lililorithiwa toka iliyokuwa Mahakama ya Mwanzo Liwale. Je, ni lini Serikali itajenga jengo la Mahakama Liwale sambamba na nyumba za watumishi?

Supplementary Question 3

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama ya Lupembe ambayo ni Mahakama ya muda mrefu sana, jengo lile lilijengwa na wakoloni na mpaka sasa hivi karibu linaanguka. Tayari tulishaleta mihtasari ya kuomba ujenzi wa Mahakama eneo lingine ambalo tayari wananchi wameshatoa na nimeshaandika barua ya kuomba. Nataka kujua ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hii ambayo sio muda mrefu itaanguka?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu yote ya awali ya kwamba Serikali inayo dhamira ya dhati ya kwanza kabisa kuhakikisha kwamba wilaya nyingi zinapata Mahakama za Wilaya pamoja na Mahakama za Mwanzo vilevile na kufanya ukarabati wa majengo chakavu ya zamani.
Kwa hiyo, nimuahidi tu kwamba maombi yao yameshawasilishwa Wizarani, tunaendelea kuyafanyia kazi, pindi pale fedha zitakapopatikana basi tutawasiliana na mamlaka husika ili tuone namna bora ya kuweza kufanikisha ujenzi wa Mahakama hiyo katika Wilaya ya Njombe pia.