Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Primary Question

MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:- Jimbo la Mlimba lina mito mingi inayotiririka mwaka mzima ambayo inaweza kutumika kujenga malambo kwa ajili ya mifugo:- Je, ni lini Serikali itajenga Malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Mlimba?

Supplementary Question 1

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimepokea majibu ya Naibu Waziri. Kwa kuwa ametoa ahadi na bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakuja tarehe 17 Mei,2018 na tarehe 18 Mei, 2018, nitajiridhisha kwenye vitabu vyao kama kweli wametenga na wameingiza kuhusu ujenzi wa malambo ndani ya Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nampongeza Mkurugenzi na Halmashauri ya Kilombelo angalau tumetenga sisi kwa mapato ya ndani shilingi milioni 103 kwa ajili ya kuboresha na kujenga malambo ndani ya Halmashauri na Jimbo la Mlimba. Hizo ni jitihada tunafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu linakuja, kwa kuwa, Jimbo la Mlimba lina takribani vijjiji 18 na kuna kilometa 606 eneo ambalo wafugaji wamekaa huko kwa wingi na vinaenda kufutwa, je, Wizara hii au Naibu Waziri yupo tayari sasa kwenda Jimbo la Mlimba kuangalia taharuki hii inayotokea kwa wafugaji hao na kuona umuhimu wa kuweka malambo ili wananchi hao na wafugaji wasiende kuingia kwenye haya maeneo ambayo yanachukuliwa na Serikali kwa ajili ya kupeleka maji kwenye Stiegler’s Gorge? Kuna taharuki kubwa sana ndani ya Jimbo la Mlimba. Je, yupo tayari sasa kwenda kuangalia na kupanga mipango sahihi? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Susan Kiwanga. Kwa ruhusa yako, naomba nimpongeze sana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mlimba kwa kutenga pesa hizo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mifugo yetu inapata maji.
Mheshimiwa Spika, swali lake ni kutaka kujua kama niko tayari kwenda naye Mlimba kuangalia juu ya adha wanayopata wafugaji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi tunafahamu ufugaji ni maisha yetu na maisha yetu ni ufugaji. Hivyo, nipo tayari kwenda Mlimba kuungana naye kwa ajili ya kwenda kuwaona wafugaji hawa.