Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. MARY P. CHATANDA (K.n.y. MHE. HAMOUD A. JUMAA) aliuliza:- Serikali iliahidi kuwapa fidia wananchi waliopisha njia ya mradi wa umeme wa gesi toka Kinyerezi kwenda Arusha, Awamu ya Kwanza hadi Chalinze lakini hadi sasa wananchi hao hawajalipwa fedha zao. Je, ni lini wananchi wa Kibaha watalipwa fidia kutoka katika fedha zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano shilingi bilioni mbili?

Supplementary Question 1

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nimpongeze vilevile yeye mwenyewe kama Naibu Waziri na Waziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba wanawapatia wananchi umeme. Nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi huu unaonekana utakwenda hadi Arusha, na kwa kuwa tayari wananchi wa Kibaha wao wameshafanyiwa tathmini ya kuhakikisha kwamba wanapata hizi fedha ambazo zimetengwa. Je, hawa wananchi wengine ambao watapitiwa na umeme hadi Arusha ni lini sasa watafanyiwa tathmini hiyo ili nao waweze kulipwa fidia zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Korogwe Mjini tunapata umeme ambao unawaka na kuzimika au unachezacheza, nini tatizo la umeme huo Korogwe Mjini? Naomba nipatiwe majibu. (Makofi)

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya msingi katika swali la Mheshimiwa Mbunge, nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini napenda sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mary Pius Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa tathmini imefanyika katika awamu mbili, awamu ya kwanza imefanyika kutoka Kibaha na Chalinze na Chalinze hadi Segera na kadhalika imefanyika kutoka Segera hadi kwenda mpaka Arusha ambapo tathmini imepatikana. Kwa awamu ya kwanza shilingi bilioni 5.2 na lile eneo la pili mpaka Tanga shilingi bilioni 10.6. Kwa hiyo tathmini zote mbili zimeshafanyika na malipo yatafanyika kwa pamoja mara baada ya uhakiki kukamilika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na umeme kutokuwa imara katika maeneo ya Tanga na maeneo mengine, nipende tu kumpa taarifa Mheshimiwa Chatanda na kumshukuru sana kwa kuunga mkono juhudi za Serikali, kinachofanyika la kwanza ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanayopitiwa na miundombinu yanafanyiwa ukarabati. Tumeshaanza kusafisha njia kutoka Tanga katika maeneo yote ya Korogwe, Lushoto mpaka Muheza na mwisho wa mwezi huu itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na maeneo ya pili ni kurekebisha nguzo pamoja na nyaya ambayo itakamilika mwezi huu wa Mei. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Chatanda baada ya mwezi Mei, hali ya umeme kwa Korogwe itaimarika sana. Ahsante sana.