Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo Kikuu katika Mkoa wa Tabora hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa huo hauna Chuo Kikuu hata kimoja cha Serikali?

Supplementary Question 1

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa Mkoa wa Tabora ni Mkoa ambao uko katikati ya Mikoa ya Singida, Shinyanga, Kigoma na Katavi; na kwa kuwa Mikoa hii haina Vyuo Vikuu vya Serikali ambavyo mwanafunzi anaweza akapata mkopo wa Serikali tofauti na Open aliyoisema Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itaweka mkakati wa kukipandisha hadhi Chuo cha Uhazili Tabora ambacho ni kikubwa na ni kizuri kama ilivyofanya katika Chuo cha Chang’ombe cha Dar es Salaam na katika Chuo cha Ushirika Moshi, walivipandisha hadhi, sasa wana mpango gani wa kupandisha hadhi Chuo cha Utumishi wa Umma cha Uhazili cha Tabora? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwe Chuo Kikuu cha Serikali ambacho kitaweza kutoa degree ambayo sasa hivi haitoki.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa maswali yake ya nyongeza; nikianzia na umuhimu wa Mikoa ya Tabora pamoja na jirani zake kuwa na Chuo eneo hili, kimsingi Vyuo Vikuu ni Vyuo vya Kitaifa na kwa sasa hivi tuna Vyuo ambavyo bado havijaweza kudahili kwa idadi ambayo ni ya kutosha kwa mfano Chuo Kikuu cha UDOM bado kina nafasi nyingi na hata vyuo vingine, kwa hiyo tutakuwa tunaanzisha Vyuo kulingana na uhitaji.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Chuo cha Uhazili Tabora ambacho kimsingi kipo chini ya Wizara ya Utumishi, naomba tu niseme kwamba hiyo sasa itategemeana na hali halisi ya Mazingira na uainishwaji wa kozi husika kulingana na mitaala iliyoboreshwa, ikitokea hivyo nadhani Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba wataona namna gani kinavyoweza kufanyika.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu kwa majibu mazuri nipende tu kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, Chuo hiki ni mahususi kabisa kwa kuwaendeleza watumishi wa umma na kitaendelea kubaki hivyo na kama alivyoeleza kwa masuala ya Vyuo Vikuu kwa kuwa yako chini ya Wizara ya Elimu endapo wataona kuna haja ya kufungua Vyuo Vikuu vingine hayo yako chini yao, lakini kwa Chuo hicho cha Uhazili ni Chuo cha Watumishi wa Umma na tuna mipango ya kuviendeleza zaidi ili kuhakikisha kwamba wanatoa kozi nyingi kuwahudumia Watumishi wa Umma. Ni mafunzo maalum kwa watumishi wa umma.