Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:- Wilaya ya Liwale ina miradi mikubwa miwili ya umwagiliaji, Mradi wa Ngongowele na Mtawango lakini Mradi wa Ngongowele umesimama kwa muda mrefu sasa. (a) Je, ni nini hatma ya mradi huu wa Ngongowele kwa sasa? (b) Je, Serikali iko tayari kumpeleka Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kukagua mradi huu ambao unaonekana kuhujumiwa kwa muda mrefu?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utangulizi tu nipende kusema kwamba jibu ni jibu hata kama halikutosha kwa muuliza swali huwa ni jibu. Hii bla bla yote iliyotolewa kwenye aya ya pili mimi sioni kama ni jibu linalijitosheleza kwa sababu mradi huu umehujumiwa kwa kiwango kikubwa sana. Kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye Jimbo langu, mimi na Mkuu wetu wa Wilaya na Mkurugenzi wetu wa Halmashauri tulipanga ziara Mheshimiwa Waziri Mkuu akakague aone nini kimefanyika kwenye mradi ule. Hata hivyo, hao watu wa Kanda wa Umwagiliaji wakishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi waliifuta hiyo ziara katika mazingira yasiyofahamika na ni kwa sababu tu huu mradi umehujumiwa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, Serikali iko tayari sasa kama hii awamu wanayotaka kuisema awamu ya tatu, kutukabidhi Halmashauri mradi huu tuutekeleze badala ya kuwaachia hawa watu wa Kanda ambao wamekuwa wakiuhujumu mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea mradi huu ili aangalie pesa hizi shilingi milioni 746 za Serikali ambavyo zimepotea bila sababu zozote zile za msingi? (Makofi)

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na la mwisho, tuko tayari kuongozana na wewe kwenda kuangalia ule mradi. Kwanza nishukuru kwamba umekubali kwamba ule mradi tumetekeleza lakini mafuriko yalitokea, sasa kama tulivyojibu katika swali la msingi tutaunda timu ya wataalam tuipeleke kule iende ikachunguze na huo ndiyo utaratibu wa kisheria wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tu kwamba Halmashauri ni taasisi ya Serikali, umwagiliaji ni taasisi ya Serikali, hawa wote wanafanya kwa niaba ya Serikali. Kwa sababu wote ni wa Serikali hakuna kitu chochote kwamba pengine Mkuu wa Mkoa alifuta ratiba ya Waziri Mkuu ili asije kuangalia mradi ule, tusilete mgongano kati ya Halmashauri na Idara ya Umwagiliaji iliyo chini ya Wizara ya Maji, zote ni Serikali.
Suala la msingi ni kwamba changamoto ipo, tushirikiane na Mheshimiwa Mbunge tutume timu ikaangalie na kama tulivyojibu kama kuna hujuma yoyote imetokea basi waliofanya hivyo watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)