Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:- Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) iliingia mkataba wa utafiti wa uchimbaji wa gesi na mafuta na Kampuni ya Mafuta ya Swala (SOGTP). Katika utekelezaji wa mpango huo wamegundua kuwepo kwa wingi mafuta ya petroli na gesi katika vijiji vya Kipenyo na Mtimbira Wilayani Malinyi katika Mkoa wa Morogoro. (a) Je, ni lini uchimbaji wa visima na uvunaji wa mafuta utaanza rasmi katika maeneo hayo? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatayarishia wananchi wa maeneo hayo ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza baina yao na Serikali kama vile gesi ya Mtwara?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na vilevile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na dhamira yao ya dhati kabisa kufanya mradi huo ukamilike. Nina maswali mawili madogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, uchimbaji wa kisima cha mradi huu,ulipangwa kufanyika mwaka 2016 na tafiti zilifanyika ikabainika kuna mafuta ya kutosha kupata mafuta ya kuendesha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kwa utaratibu ambao wameuwekeza ukiritimba umezidi mno umesababisha mpaka sasa hivi mkataba kati ya mwekezaji kampuni ya Swala ya Kitanzania na TPDC bado haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni lini sasa mtakamilisha mkataba huu ili mradi huo wa uchimbaji wa haya mafuta uanze kwa sababu haraka haraka tu pale itaajiri wananchi karibuni 500 kwa kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nakubali mmetoa elimu lakini mafundisho tuliyopata Mtwara mnaelekea huko huko, elimu mnayo toa mnafanya vi semina na mikutano, watu wachache sana wanahusishwa, eneo lengwa tarafa nzima ya Mtimbira lina wakazi karibu 75,000, hizo semina sijui mtaendeshaje nawashauri na baadaye nauliza swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumieni media, tumieni vyombo vya habari ambavyo vitaweza kusambaza taarifa na habari haraka sana kuliko hizo semina mnazofanya. Katika maeneo yetu kuna redio za jamii mbiliā€¦
redio FM Ulanga, je, Serikali mpo tayari kutumia redio hizo za jamii ili kuelimisha jamii katika eneo hilo?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla ya kujibu maswali napenda nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mponda anavyofuatilia utekelezwaji wa mradi huu. Mradi utakapoanza kutelezwa utaajiri watanzania takribani 200 hadi 300, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mponda hongera sana kwa kufuatilia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali lake la kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mkataba ulishasainiwa tangu mwezi Februari, 2012 kwa hiyo, kilichobaki ni uekelezaji wa kufanya drilling kwa maana ya uchimbaji na ugunduzi wa mafuta, na katika eneo hilo Mheshimiwa Mponda mafuta yanayotarajiwa kuchimbwa katika eneo hilo yanafikia milioni 180 hadi milioni 200. Kwa hiyo, ni mtaji mkubwa na utakuwa na manufaa kwa wananchi wako na watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa uchimbaji utaanza, kama ambavyo nimeleeza kama ambavyo nimeleleza kwenye hilo la msingi kwamba kinachosubiriwa ni kupata kibali cha mazingira kutoka NEMC na wenzetu NEMC wanalifanyia kazi pamoja na Mamlaka ya TAWA yaani Hifadhi ya Mamlaka ya Wanyamapori, wametuhakikishia kwamba kuja kufika mwezi Julai vibali vimepatikana na mwezi Septemba uchimbaji utaanza rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kuhusiana na elimu, kwa kweli niwapongeze sana TPDC na Swala wametoa elimu katika mkoa mzima wa Morogoro sasa takribani ya watu 350 wamepewa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumepeleka elimu pia katika vijiji vingi, ikiwemo kijiji cha Mheshimiwa Dkt. Mponda, Ipera, Kipenyo, Mtimbira lakini pamoja na maeneo ya Mnazini pamoja na vijiji vingine anavyovijua Mheshimiwa Mbunge na maeneo mengine ya Kijiji cha Kitete na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, takribani ya wananchi 350 walipata elimu, lakini tutaendelea na kutoa elimu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri. Lakini kuhusu vyombo vya habari tumeshaanza kutumia TBC na nimechukua ushauri wake kwamba chombo cha FM media cha Ulanga nacho tutazingatia tutakipa kazi hiyo.