Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Primary Question

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:- Jeshi la Polisi lina kazi kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini cha kusikitisha ni kwamba askari wanaishi kwenye nyumba duni sana jambo ambalo linashusha hata hadhi zao hasa kwa upande wa Tanzania Zanzibar. (i) Je, ni lini askari wetu watatengenezewa nyumba bora nao wajisikie kuwa Serikali yao inawajali? (ii) Katika Makao Makuu ya Polisi pale Ziwani kuna majengo yaliyoachwa na wakoloni, je, kwa nini yasifanyiwe ukarabati mkubwa ili yaweze kutumiwa na askari wetu?

Supplementary Question 1

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake zuri. Vilevile lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Masauni kwa ziara aliyoifanya ndani ya Jimbo langu na kupunguza uhalifu, nimpe hongera sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini nyumba hizi zitaanza kujengwa kwa upande wa Unguja?
Swali la pili, kuna vituo vya polisi ambavyo hali yake ni mbaya sana kwa sasa hasa ukiangalia kama kituo cha Ng’ambu pamoja na Mfenesini na vipo vingi ambavyo hali yake ni mbaya sana, je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifanyia marekebisho vituo hivyo angalau vilingane na hadhi ya Jeshi la Polisi kwa sasa? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi zake. Ni kweli Jimboni kwake kuna eneo ambalo lilikuwa ni hatarishi sana kwa usalama wa wananchi na tulifanya ziara pamoja na yeye na tukaweza kuchukua hatua. Napongeza sana Jeshi la Polisi kwa kuweza kudhibiti ile hali. Sasa hivi nimeambiwa kwamba hali ni shwari na wananchi wanafanya shughuli zao vizuri. Kuhusiana na hizi nyumba kwamba ni lini zitajengwa, ni pale ambapo taratibu za kifedha zitakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine anazungumzia kuhusu vituo vya polisi kwamba vina hali mbaya. Ni kweli tuna matatizo ya vituo vya polisi, siyo tu vina hali mbaya, lakini ni pungufu. Tuna upungufu wa takribani vituo 65 hasa katika Wilaya za Kipolisi nchini. Kwa hiyo, hili vilevile linakwenda sambamba na hali ya kibajeti. Pale ambapo hali ya kibajeti itaruhusu tutajenga vituo vipya katika maeneo ambayo hakuna, lakini vilevile kukarabati vile ambavyo viko katika hali mbaya.