Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:- Katika Mkoa wa Mara kuna usumbufu mkubwa unaosababishwa na tembo. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo hao?

Supplementary Question 1

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana. Majanga ya tembo katika Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla ni makubwa sana, lakini majibu ya Waziri yamekuwa ni mepesi sana. Nitanukuu, naambiwa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka 2016 ni matukio 128 na mwaka 2016 mpaka 2017 wamepunguza hadi 105, kwa maana hiyo matukio waliyoweza kuyapunguza ni 23 tu. Hatuoni kwamba itachukua muda mrefu sana mpaka kuhakikisha kwamba tatizo la tembo hapa Tanzania kwa ujumla litakuwa bado ni tatizo kubwa sana kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, hawa tembo zamani wananchi walikuwa wanajichukulia wenyewe hatua mikononi na tembo hawa walikuwa hawasumbui wananchi. Lakini kwa sababu Serikali imeona kwamba tembo ni wa thamani kuliko binadamu, na ukiua tembo ni shida unafungwa miaka mingi, na tembo akiua binadamu ni halali. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu mazuri kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, je, warudi kule kule wajichukulie hatua mkononi? Kwa sababu ile nyama ya tembo inaliwa na wanasema kwamba aidha…

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kweli kwamba uvamizi wa tembo katika maeneo ya wananchi ni changamoto kubwa katika maeneo ya Bunda, Tarime na Serengeti. Hata hivyo Serikali inachukua kila aina ya hatua kuhakikisha kwamba inapambana na kuzuia hali hii, na orodha ya hatua ambazo zimechukuliwa nimezitaja. Pamoja na hayo, tunaendelea na utafiti wa kuweza kutambua njia nyingine bora zaidi za kukabiliana na jambo hili. Na Mheshimiwa Mbunge atakuwa ni shahidi kwamba wafanyakazi wetu pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri wanafanya juhudi kubwa sana ya kusaidia wananchi katika jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, si kweli kabisa kwamba tembo ni bora kuliko wananchi. Lakini ni jambo lisilopingika kwamba wanyamapori ni rasilimali kubwa yetu sisi sote kama wananchi wa Tanzania na tunawashukuru sana wananchi wa Mara kwa juhudi kubwa ambazo wanafanya kusaidia nchi nzima katika kuwahifadhi wanyama hawa.

Name

Willy Qulwi Qambalo

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Karatu

Primary Question

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:- Katika Mkoa wa Mara kuna usumbufu mkubwa unaosababishwa na tembo. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo hao?

Supplementary Question 2

MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, uko utaratibu kama si sheria au kanuni katika nchi hii, kwamba mifugo ya wananchi au wananchi wenyewe wakiingia kwenye hifadhi kuna tozo inawakuta. Je, Mheshimiwa Waziri haoni ili kuondokana na hili tatizo la wanyama kutoka nje umefika wakati sasa wanyama wakitoka nje kwenye maeneo ya wananchi, tozo hiyo hiyo ambayo wananchi wanatozwa wakiingia kwenye hifadhi nayo itozwe? Nakushukuru. (Makofi)

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, wanyamapori si binadamu na wanyamapori hawana akili za kibinadamu, ni wanyama wa porini. Kwa hiyo, tujitahidi sana kuwalinda kwa kuwaeleza askari wanyamapori pale wanapotokea na mimi nasema kwa kweli ni furaha kubwa kwamba kwa mara ya kwanza sasa tembo wameongezeka kutokana na hali mbaya ya ujangili iliyokuwepo hapa nchini na sasa wanaonekana, wanakuja mpaka kwenye maeneo ya watu. Rai yangu kwa kweli tushirikiane ili tuwataarifu askari wanyamapori pale wanyama hao wanapotokea na sisi tunachukua hatua haraka iwezekanavyo kila tukio la namna hii linapotokea.

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:- Katika Mkoa wa Mara kuna usumbufu mkubwa unaosababishwa na tembo. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tembo hao?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katoa majibu mazuri sana, lakini mimi nina concern moja kubwa kwamba hawa tembo madhara yao ni makubwa sana katika Wilaya ya Busega ambayo inapakana na Wilaya za Bunda na Serengeti. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba hawa tembo wanazidi kudhibitiwa, lakini mwishoni amesema kwamba tembo wameongezeka zaidi, sasa sijaelewa kwamba sasa kwa vile wameongezeka zaidi madhara yatakuwa makubwa kwa wananchi. Serikali sasa kupitia Wizara yake ina mkakati gani kuwaokoa wananchi ambao wanasumbuliwa na tembo kwa kusababishiwa hasara kubwa zaidi?

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma nchi yetu ilikuwa na tembo wengi sana, wanafika 110,000, hivi sasa hatua tuliyofikia hapa wanyama hawa walipunguzwa sana na ujangili wakafika chini ya 10,000. Sasa hivi ndiyo idadi hiyo inaanza kukua na tunaanza kuwaona. Katika eneo lile la Serengeti na eneo la Maswa tunafanya utafiti kuangalia kama tunaweza kujenga uzio wa kuwatenganisha watu, mashamba yao na hifadhi. Tunafanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa hapa nchini kwetu na mazungumzo yanaelekea vizuri. Sikupenda nifike mahali ninasema jambo hili, lakini Serikali inalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa sana na ndiyo maana tunafanya utafiti wa uwezekano wa kujenga uzio wa kilometa 140 tuone kwamba italeta afueni kiasi gani katika kuwadhibiti wanyama hawa.