Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA Aliuliza:- Wilaya ya Same ni miongoni mwa Wilaya zinazokumbwa na baa la njaa mara kwa mara na Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kupeleka chakula cha msaada; na kwa kuwa Wilaya ya Same ina mito mikubwa na maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji:- (a) Je, Serikali inasema nini juu ya maombi ya muda mrefu yaliyowasilishwa Wizarani ya kujenga Bwawa la Yongoma ili maji yatumike kwa ajili ya umwagiliaji kwenye mashamba yaliyoko katika Kata za Maore, Ndungu, Kihurio na Bendera; (b) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga bwawa hilo ili kuokoa maisha ya wananchi na fedha nyingi za Serikali zinazotumika kununua chakula cha msaada mara kwa mara?

Supplementary Question 1

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kweli nimesikitishwa sana na majibu wa Waziri ambaye naamini ni msomi na najua ni mtaalam wa mambo ya maji. Nimesikitika sana, kwanza mradi huu ambao uligharamiwa na Serikali ya Japan ulipelekwa Wizarani tangu 2012. Mwaka jana mwezi Novemba nikamwona Waziri nikamweleza, akaniomba nilete ile proposal na maombi nikampelekea.
Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba hata hakunipa majibu, nashangaa leo akisema bwawa hili ni dogo ambalo
gharama zake 2012 ilikuwa milioni 800 na linahudumia wananchi ambao ni zaidi ya 40,000. Hata hivyo, kibaya zaidi amejichanganya tena na huo mradi wa Kalema dam ambao mwenyewe mwaka jana tukiongea juu ya bwawa hili. Nilimweleza wazi kwamba hawa UN-CDF wamekuwa tayari kulihudumia bwawa hili, nilichokuwa nimekosa kwenye Halmashauri ilikuwa utaalam.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Umoja wa Mataifa, wamekuwa tayari na Serikali ya Norway imeonesha kwamba
iko tayari kusaidia mradi huu, leo anajichanganya hapa na kusema anarudisha Halmashauri. Mradi huu wa Kalimawe ni square kilomita 24; Je, hilo ni bwawa la kati? Hapo nilikuwa nazungumzia masikitiko yangu. Swali langu ni kwamba kama Waziri aliona hili lingerudishwa kwenye Halmashauri, kwa nini hakunijibu hivyo, tangu mwaka jana Novemba?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wizara hii kutokana na ripoti ya Mkaguzi wa Ufanisi katika Ujenzi wa Miradi ya
Maji Mijini, imeonesha uzembe mkubwa sana na upotevu mwingi wa hela za miradi, kiasi kwamba naamini ndio
maana wanashindwa hata kujenga miundombinu ya kumwagilia maji ili wananchi wetu, wakulima waweze
kuvuna….
Mheshimiwa Spika, nauliza je, kama Wizara inaona haiwezi kufanya mambo ya umwagiliaji badala yake walijua kuchakachua tu miradi ya maji, kwa nini wasiachie kazi hiyo au watumishi wake wakafukuzwa?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge
kwamba jinsi tunavyojibu maswali haya inategemea na namna ulivyouliza. Wewe umeuliza kwamba hili bwawa
umeleta maombi kwa muda mrefu, sasa na sisi tunatengeneza majibu kulingana na swali ulilouliza. Kwa hiyo,
hatujafanya uzembe wa aina yoyote katika kujibu.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpe taarifa pia kwamba miradi hii ya mabwawa ya umwagiliaji ilikuwa ina
wafadhili mbalimbali ikiwepo JICA ndiyo walioweza kufadhili. Hatukuwa tumeiweka katika mipango ya bajeti ya Serikali ambayo sisi tunasimamia moja kwa moja. Sasa maombi yake tumesema kwamba sasa tunafanya mapitio, siyo kwa bwawa lake tu yako mengi nchi nzima, ili tuweze kuona ni namna gani tutayashughulikia.
Mheshimiwa Spika, pia swali la nyongeza la pili, kwamba kuna mradi ambao una uzembe, ambao haridhiki na utekelezaji wake. Naomba atuletee ili tuweze kuona nini kifanyike na kama kuna watu waliofanya uzembe basi
tuwachukulie hatua.