Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:- Maziwa Madogo nchini kama vile Ziwa dogo la asili la Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu yanaelekea kukauka kutokana na kuongezeka kwa magugu maji, kadhalika Ziwa Babati na Ziwa Manyara pia yana dalili ya kukauka na Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina uwezo wa kuyaokoa:- (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyaokoa maziwa hayo muhimu katika ustawi wa nchi yetu na kizazi kijacho? (b) Je, kwa nini kusiwe na mpango kabambe wa Kitaifa kuyaokoa maziwa hayo?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Hivi sasa Serikali inatumia gharama kubwa sana katika kuanzisha mabwawa mapya kupitia maji ya mvua; lakini rasilimali hizi za asili nyingi zimeelekea kutoweka, kwa hiyo, nilidhani Serikali pia itakuwa na mkakati.
Mheshimiwa Spika, hivyo nina maswali madogo mawili, la kwanza, fedha zilizotajwa katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 hazikuweza kupatikana hadi sasa na hivi sasa tunaingia Bajeti ya Mwaka 2017/2018, lakini hali inayotishia ziwa hili inaonesha hivi punde litakauka; je, Serikali itatoa lini fedha milioni mia moja kupitia Mradi wa DADP’s ambayo imekusudiwa kwa nia njema katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amewajibu Watanzania pamoja na mimi na wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutuma timu ya wataalam kupitia maziwa yote ya asili katika nchi yetu ili iweze kutoa ushauri wa kitaalam na kuchukua hatua za kunusuru maziwa hayo kwa haraka na wataalam hao watakwenda lini?

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba baada tu ya kupata swali lake hili nilifanya ziara katika Mkoa wa Manyara na kati ya maziwa ambayo nilikwenda kuyaona ni Ziwa Babati, tukiwa na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Mheshimiwa Pauline Gekul pamoja na Mheshimiwa Jitu Soni, na bahati mbaya siku ile Mheshimiwa alipata ajali, pole sana, lakini Mwenyezi Mungu alitusaidia.
Mheshimiwa Spika, basi niseme kifupi kwamba, bajeti haijakwisha, Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la kwanza kwamba fedha hazijapatikana, milioni 100 lakini leo tuko Aprili na bajeti yetu inakwisha Juni. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba sisi tunafanya kila linalowezekana kama Serikali kuhakikisha fedha hizo zimefika ili zifanye kazi iliyokusudiwa; na zile nyingine zilizopangwa kwa ajili ya kazi nyingine inayofuata.
Mheshimiwa Spika, la pili, timu ya wataalam itakwenda lini; hili namhakikishia kwa sababu hili sasa nimeahidi kwa niaba ya Serikali, kwamba tutafanya tathmini katika maziwa yetu. Tunaelewa changamoto ambayo sasa vyanzo vya maji vimekabiliwa, mito mingi inakauka, maziwa yetu mengi yanakauka, mabwawa yetu mengi yanakauka.
Kwa hiyo, sisi kama wenye dhamana hii ya kusimamia mazingira, kwa dhati kabisa tumeamua na katika bajeti ya mwaka huu wa fedha inayokuja mtaona jinsi ambavyo tutaanza kushughulikia vyanzo vya maji, kurudisha uhai wa
vyanzo vya maji ili viweze kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuahidi kwamba niliyowaahidi kwenye maziwa ambayo nimeyataja kwanza wataalam watakwenda tena waliobobea kutoka kwenye sekta zote ambao wako competent na wataweza kutushauri kama Serikali ili tuweze kuja na mpango sasa madhubuti wa kuhakikisha kwamba maziwa yetu yanaendelea kubaki.