Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama za ukaguzi wa filamu ambapo kwa hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja kwa dakika? (b) Je, Bodi ya Filamu imejipanga kwa kiasi gani kuhakikisha huduma zake zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo ni wasanii wachache wa filamu ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu wa Bodi hiyo ambayo hata ofisi zake hazijulikani ipasavyo sehemu zilipo Jijini Dar es Salaam?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja
na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nieleze masikitiko yangu
kwamba yaani kumbe mpaka leo Bodi haina tovuti, 2017, this is very bad, ni
jambo la kusikitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niende kwenye swali langu la kwanza la
nyongeza, nimeona muainisho wa hizo gharama, wasanii wanapokwenda
kusajili, pamoja na hizo gharama lakini wanalazimika kwenda kupata huduma hii
Dar es Salaam tu haitolewi katika maeneo mengine. Wakishapata hii huduma ya
kutoka BASATA kusajili COSOTA na Bodi ya Filamu, kuna huduma nyingine
kwenda TRA ili wapate stika ambayo ni mapato na stika zinatolewa tu Makao
Makuu ya TRA Dar es Salaam. Je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba angalau
Ofisi hizi za BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zinakuwepo hata katika ngazi ya
mikoa ili kuwarahisishia wasanii na kuwapunguzia gharama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna hizi filamu za kutoka nje
maarufu sana kwa jina la mazagazaga kwa sababu unakuta wametandika chini
zimezagaazagaa, gharama yake maximum kwa CD moja ni Sh.1,200 lakini
hazitozwi gharama zozote za usajili wala hakuna mapato yoyote ambayo Serikali
inapata. Kwa kulinda kazi za ndani za wasanii wetu wa filamu wa ndani ambao
CD zao sasa zimeshuka thamani hadi Sh. 2,000 halafu wanashindana na za nje za
Sh.1,200 na Serikali inakosa mapato, je, inasemaji katika kudhibiti filamu hizi za
kutoka nje, imeshindwa kabisa?

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa
Naibu Spika, swali la kwanza anataka kujua kama kuna utaratibu wowote
ambao Serikali imefanya ili wasanii waweze kupata vibali kutoka mikoani.
Ninachoweza kusemea ni kuhusiana na Bodi ya Filamu, kama nilivyosema awali,
Bodi ya Filamu tayari inazo ofisi katika Wilaya na Mikoa na kule kuna Bodi za
Filamu za Mikoa na Wilaya ambapo RAS kwa upande wa Mkoa ndiye Mwenyekiti
na Afisa Utamaduni ndiye Katibu na kwa upande wa Wilaya DAS ni Mwenyekiti
na Afisa Utamaduni wa Wilaya ni Katibu na kuna wajumbe wengine katika Bodi
hizi. Kwa hiyo, vibali vinatoka pia katika wilaya na mikoa na siyo lazima wafuate
huduma hizi Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa TRA zipo ofisi za mikoa lakini
upande wa COSOTA sina uhakika sana. Hata hivyo, tunafanya mazungumzo na
vyombo vyote hivi ambavyo vinadhibiti wizi wa kazi za wasanii na wajumbe wake
wote ni wajumbe wa Kamati ya Urasimishaji na hivyo basi, tunafanya kila jitihada
ili tuweze kuona tunamkomboa msanii kuanzia ngazi za wilaya, mkoa na hata
makao makuu Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa BASATA, mpaka sasa tunataka
kufanya utaratibu wa usajili kwa njia ya mtandao pamoja na Bodi ya Filamu.
Hivyo, niwahakikishie wasanii kwamba huduma hizi zitafikishwa kwao na
watakuwa hawapati usumbufu sana kufika Dar es Salaam kwa sababu
tunawatakia mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa filamu za nje, nadhani wengi
tumekuwa mashahidi kwamba Serikali inafanya kila jitihada. Zoezi la urasimishaji
lilianza tangu mwaka 2009 ambapo kazi za wasanii zilianza kuwekewa ushuru wa
stempu tangu mwaka 2013 kwa Sheria ya Ushuru wa Stempu. Kwa zile kazi
ambazo zinatoka nje na hazifuati utaratibu zimekuwa zikikamatwa na wahusika
kuchukuliwa hatua. Napenda kuwatangazia kwamba zoezi hili ni endelevu,
tumekuwa tukifanya msako au opereshenitangu 2014 hadi 2016 na tunaendelea.
Hivyo, nawaomba wote ambao wanauza kazi za wasanii nje ya utaratibu
wafuate utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu
Spika, nakushukuru. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini pamoja na
majibu yake mazuri, naomba kuongezea kwenye sehemu ya pili ya swali la
Mheshimiwa Cosota Chumi. Ni kweli tatizo la kazi za sanaa kutoka nje katika nchi
yetu ni kubwa na baya na linaua kwa kiasi kikubwa kazi za sanaa za ndani. Ili
kushughulika na tatizo hili kuna sheria za vyombo zaidi ya vitano zinahusika. Kuna
Sheria za TRA, BASATA, Bodi ya Filamu, COSOTA, ukizijumlisha zote kwa pamoja
ndiyo at least unaweza kushughulika na tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapitia upya sheria hizi na kuangalia
upungufu uliopo, turekebishe na tuzi-harmonise kwa pamoja ili tuweze kulimaliza
tatizo hili. Kwa sheria zilizopo, namna ya kushughulika na tatizo hili bado ni ngumu
sana. Kwa hiyo, tunachoweza kuahidi hapa ni kwamba tunazipitia na tuko
mahali pazuri na tukilikamilisha zoezi hilo kazi hii itakuwa imekwenda vizuri na kwa
hiyo tutapambana na tatizo hili la piracy kwenye nchi yetu.

Name

Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama za ukaguzi wa filamu ambapo kwa hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja kwa dakika? (b) Je, Bodi ya Filamu imejipanga kwa kiasi gani kuhakikisha huduma zake zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo ni wasanii wachache wa filamu ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu wa Bodi hiyo ambayo hata ofisi zake hazijulikani ipasavyo sehemu zilipo Jijini Dar es Salaam?

Supplementary Question 2

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Wizara hii inashughulika na habari, utamaduni, sanaa na michezo. Kwa idhini
yako, naomba uniruhusu niulize swali la michezo. Timu yetu ya vijana under 17
imebahatika kwenda kwenye fainali itakayofanyika Gabon Aprili, ni mwezi
mmoja tu sasa umebaki. Je, Serikali pamoja na TFF tunajiandaa namna gani ili
timu yetu hii isiende kushiriki bali iende kushindana na kuleta ushindi katika nchi
yetu?

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli kwamba Serengeti Boys wamefanya vizuri sana katika mchezo wa
mpira wa miguu katika nchi yetu na kuiletea heshima nchi yetu. Nichukue nafasi
hii kuwapongeza kwa moyo wao wa dhati ambapo wamejitahidi kupambana
na kwa kweli wanafanya vizuri. Kama Serikali, kwanza nilihakikishie Bunge lako
kwamba tumeshiriki kikamilifu kwa wao Serengeti Boys kufanikiwa kufika pale
walipofika ikiwemo kutafuta rasilimali kwa wadau. Niwashukuru sana wadau wa
sekta binafsi ambao wamekuwa wakijitolea kuhakikisha timu yetu hii inafanya
vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwa kushirikiana na TFF tumejipanga
kwamba Serengeti Boys watakwenda kupiga kambi ya mwezi mzima kabla ya
kwenda kwenye fainali za mashindano haya. Serikali ikishirikiana na wadau wa
sekta binafsi, tutahakikisha zinapatikana rasilimali za kutosha kuhakikisha vijana
hawa wanapiga kambi yao, lakini pia wanakwenda kuchukua kombe na siyo
kushiriki. Kila tukiangalia uwezekano wa kushinda, ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na
Watanzania kwa pamoja tuungane pamoja kwa dua zetu na rasilimali zetu
kuhakikisha kwamba Serengeti Boys wanakwenda na wanarudi na ushindi hapa
nchini.