Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:- Vijiji vya Kabage, Kungwi, Sibwesa, Kasekese na Kaseganyama viko kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi na WMA. Je, ni lini Serikali itaingilia kati na kutatua mgogoro huo unaoleta usumbufu mara kwa mara?

Supplementary Question 1

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wakati Jumuiya inaanzishwa maeneo haya yalikuwa na kijiji kimoja tu cha Sibwesa, lakini leo hii kuna vijiji zaidi ya sita na kata mbili zimeanzishwa kwenye maeneo hayo na Serikali inatambua maeneo hayo ya kiutawala. Je, ni lini Serikali kupitia Wizara wataenda ku-review mipaka hiyo ambayo ipo inayoleta migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo hayo ili kuondoa shida inayosababisha wananchi kupigwa mara kwa mara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati Jumuiya inaanzishwa ilikuwa na malengo mazuri ya kiuchumi ambayo kwa sasa hayapo na wananchi hawajanufaika na mradi wowote ule ulioanzisha Jumuiya hiyo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaachia hayo maeneo ili yaendelezwe na vijiji vyenyewe husika?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza kimsingi anakubaliana na hoja ya jibu la msingi kwamba tangu wazo la kuanzishwa kwa WMA lilipotolewa hadi leo mabadiliko mengi yametokea ikiwemo kuongezeka na kubadilika kwa maeneo ya utawala. Ameuliza swali ni lini Serikali itaenda kushughulikia mabadiliko hayo na kuweza kupima umuhimu wa kuendelea na wazo la WMA?
Mheshimiwa Spika, jibu langu ni kwamba mara tu baada ya kukamilika kwa kikao hiki kinachoendelea cha wiki mbili mimi na Mheshimiwa Mbunge tutapanga ratiba vizuri kwa sababu nadhani tukienda pamoja mimi na yeye tutafanya jambo ambalo ni la tija zaidi.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anasema hapo zamani eneo hili ni kweli lilikuwa linaonekana lina faida za kiuchumi na kijamii lakini kwa maoni yake anasema kwamba hali hiyo imebadilika kwa hivyo hivi sasa anadhani kwamba kuna haja ya Serikali kupitia upya mawazo au maamuzi hayo.
Mheshimiwa Spika, jibu ni kama lilivyo kwenye majibu ya msingi aya ya mwisho kabisa kwamba sasa Serikali tutakwenda kwanza kutoa ushauri lakini pia kushirikisha wataalam wa eneo hili ili tuweze kwa pamoja sasa kupima hicho ambacho tunasema kwamba zamani kilikuwepo lakini sasa hakipo. Mimi naamini tukienda wote tukakaa pamoja na kukagua maeneo yanayohusika tunaweza tukafikia muafaka. Ahsante sana.