Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Primary Question

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:- Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:- Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?

Supplementary Question 1

MHE. ALI HASSAN OMARY KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo hata na mimi sasa nimeelewa nini tatizo na chanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zimewekwa hatua za kuchukuliwa kama ambazo tumeziona pale, namuomba Waziri ambaye anahusika na masuala haya ya mazingira na utafiti, japo siku moja twende tukaone ile hali tuweze kuangalia nini kifanyike ili tuweze kupata ufumbuzi zaidi ya hapa ambapo tumeona. Ahsante.

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Ali Hassan King kwa jinsi alivyo na mapenzi mema hasa katika suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Ninachopenda kumhakikishia tu hapa kwamba niko tayari na tutafuatana na Mheshimiwa Mbunge tutatembelea maeneo haya yote ambayo yamedidimia na tutaungana na wataalam wengine kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Nataka nimwambie tu kwamba bila kupoteza muda siku ya Jumanne na Jumatano nitakuwa Zanzibar kwa ajili ya kazi hii na tutafuatana naye.

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:- Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:- Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?

Supplementary Question 2

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la tabia nchi linakabili maeneo mengine. Mji wa Mikindani ni mji ambao uko chini ya usawa wa bahari na kwa miaka mingi maji yakijaa baharini huwa yanaingia mpaka katikati ya mji lakini yalikuwa hayaleti madhara kwa sababu kulikuwa na kingo ambazo zimejengwa ili kuzuia maji yasilete athari kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kingo hizo zimeharibika kwa kiasi kikubwa na kufanya maji yanapojaa baharini kwenda kule kwenye mji mpaka katika makazi ya watu. Je, Serikali ina mpango gani wa kurejesha tena zile kingo ambazo ziliwekwa hasa kipindi hiki ambacho maji katika usawa wa bahari yamekuwa yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi?

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua tatizo kubwa la kuongezeka kwa kina cha bahari. Siku zilizopita nilieleza kwamba sasa kina cha bahari kimeongezeka kwa sentimeta 19. Serikali yetu inachukua hatua za kuhakikisha kwamba tunakabiliana na tatizo hili. Moja, ni pamoja na kuzikarabati zile kuta na tayari tuna miradi inayoendelea. Mwezi wa nne mwaka huu, tutaanza rasmi kuzikarabati zile kuta za bahari ili kuhakikisha kwamba tunadhibiti ule mmomonyoko ambao umefanyika kwenye kuta hizo na kuziwezesha kuwa bora zaidi ili kutokuendelea kumomonyoa kingo za bahari yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme kwamba hata kwenye mkutano huu wa juzi wa Paris, Serikali yetu ilipata dola za Marekani 1,052,000. Fedha zote hizi kazi yake kubwa ni kwanza kutupatia uwezo mkubwa wa kupata fedha zaidi kutoka kwenye vyanzo vya fedha vya mabadiliko ya tabia nchi kama Adaptation Fund, Least Developed Countries Fund, Green Climate Fund na maeneo mengine kama UNEP na tumejipanga vizuri tutakapopata fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine pia fedha hizi tutazitumia kufanya tathmini ya kina katika maeneo ambayo yameathirika sana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi ili tuweze kuchukua hatua mahsusi ya kutatua tatizo hili. Tutatumia fedha za wahisani lakini vilevile tutatenga fedha zetu za ndani ili kukabiliana na tatizo hili la mabadiliko ya tabia nchi ambalo sasa linatishia dunia, linatishia nchi yetu.

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:- Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:- Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?

Supplementary Question 3

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hivi karibuni tumeshuhudia kwa ukatili kabisa na pasipo kuzingatia haki za binadamu kwa kisingizio cha kutunza mazingira, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imebomolea wananchi ambao wanaishi kwenye mabonde na pembezoni mwa mito. Hata hivyo, tuna taarifa vilevile kwamba miaka minne iliyopita, wananchi hao walitakiwa wahamishwe kutoka mabondeni kupelekwa Mabwepande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa vile vile kwamba mgawanyo wa viwanja vya Mabwepande ulifanyika kinyume na utaratibu. Je, Serikali iko tayari kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali afanye uhakiki wa viwanja vya Mabwepande ili tujue nani alipata nini na kama kuna tatizo lolote hatua muafaka zichukuliwe ili wananchi waliotarajiwa kupata viwanja hivyo waweze kupata haki yao? (Makofi)

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zoezi la bomoabomoa lililofanyika Dar es Salaam - Msimbazi, sheria na taratibu zote zilifuatwa. Nataka kusisitiza tu hapa kwamba hakuna tatizo lolote katika zoezi hilo. Kumtumia Mkaguzi wetu wa Hesabu za Serikali kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaomba kama kuna mambo ya kutaka kujiridhisha sisi tuko tayari afanye hiyo kazi lakini sheria zote zilizingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sasa hivi dunia imefikia kwenye wakati mgumu sana katika suala hili la mabadiliko ya tabia nchi. Ni lazima sisi viongozi wote tujipange na tuwe mstari wa mbele kuwaambia wananchi wetu waondoke mabondeni. Kwa sababu mafuriko sasa ni suala ambalo litaendelea kuwa permanent kulingana na madhara ambayo yapo sasa hivi yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, ni lazima sisi viongozi wote tuwe firm kuwaambia wananchi wetu bila kumumunya maneno, waondoke wote mabondeni kwa sababu ni kwa ajili ya afya na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tupo tayari Mkaguzi afanye kazi hiyo kwa sababu jambo hili lilifanyika kwa mujibu wa Sheria yetu ya Mazingira kwa maana ya kifungu cha 57(1) ambapo wananchi hawapaswi kuishi ndani ya mita 60 kutoka kwenye mabonde, mito au bahari. (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Primary Question

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:- Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:- Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?

Supplementary Question 4

MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Athari za mabadilko ya tabia nchi ni donda ndugu kwa Mji wa Pangani. Kwa kuwa Mji wa Pangani ni mji mkongwe ambao umejengwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi na Mto Pangani, je, ni lini Serikali itajenga ukuta wa Mto Pangani kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu na fedha zake tayari zipo? (Makofi)

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepania na penye nia pana njia. Tutaujenga ukuta huo na fedha tumekwishapata. Tunatarajia Aprili, 2016, tutaanza ujenzi wa ukuta Pangani ili kuwahakikishia wananchi wa Pangani kwamba maisha yanaendelea. Pamoja na matatizo makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi lakini vilevile maisha lazima yaendelee. Tutatumia fedha za wahisani kutekeleza jukumu hili lakini pia tutaendelea kutenga fedha zetu za ndani katika bajeti kuhakikisha wananchi wetu wanaishi salama pamoja na athari hizo kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zinajitokeza hapa nchini.