Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ndani ya Halmashauri mbili na Majimbo matatu, hospitali hii inategemewa na watu zaidi ya 500,000. Je, ni lini Serikali itaifanyia upanuzi hospitali hiyo hasa wodi ya akina mama wajawazito?

Supplementary Question 1

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Kwa kuwa Jimbo la Lushoto lina kituo kimoja tu cha afya, ambacho kinahudumia takribani Kata saba; je, Serikali haioni sasa kuwa umefikia wakati wa kujenga vituo vya afya hasa katika Kata ya Makanya, Ngwelo, Kilole, Gare, Ubiri, Magamba, Malibwi pamoja na Kwai?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Lushoto wamejitolea kujenga zahanati katika vijiji vya Mzalagembei, Bombo, Mavului, Mbwei, Mazumbai, Ilente, Mbelei, Makanka na Kwemachai, lakini zahanati hizi zimebakia kukamilika tu.
Je, Serikali inatoa tamko gani sasa la kumalizia zahanati hizi pamoja na kupeleka watumishi ili wananchi wa Jimbo la Lushoto waondokane na usumbufu wa kutembea umbali mrefu hasa kwa mama zetu na dada zetu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza katika kumbukumbu yangu Mheshimiwa Shekilindi amekuwa akiuliza maswali mengi sana ya sekta ya afya, ofisi yetu inakiri mchango mkubwa wa Mheshimiwa Shekilindi katika Jimbo lake na wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, katika kulifanikisha suala hili, Serikali tumeelekeza mpango wetu wa sasa tunaondoka nao, jinsi gani tutafanya katika mwaka huu wa fedha, kuhakikisha kwamba tunajenga vituo vya afya. Mheshimiwa Shekilindi kwa sababu jana nilikujibu hapa kwamba nina mpango wa kuanzia katika Mkoa wako wa Tanga, tena ratiba nimeibadilisha nitaanza siku ya tarehe 21, na Mheshimiwa Shangazi, nitakuwa naye hiyo tarehe 21, tutaangalia jinsi gani tutafanya baada ya kuwa kule site, kutembelea hivyo vituo. Katika mpango wa bajeti inaokuja lengo kubwa ni kuimarisha vituo vya afya, katika ujenzi kwenye maeneo yetu, tumelenga kwamba angalau kila Halmashauri katika mwaka wa fedha tunaoondoka nao tujenge kituo kimoja cha afya.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika katika suala zima la maboma nimesema, tulifanya assessment katika Halmashauri zote, na hili ni agizo la Kamati ya Bajeti, maboma yote ambayo hayajakamilika, tumepata idadi ya maboma. Ndiyo maana nimesema katika bajeti ya mwaka huu unaokuja sasa, ninaomba Waheshimiwa Wabunge, tuungane pamoja kwamba jinsi gani tutafanya mpango mkakati wa kibajeti tuweze kumaliza maboma yale ambayo Mheshimiwa Shekilindi umeyazungumza katika maeneo yako, tukimaliza yale tutakuwa tumesogeza kwa ukaribu zaidi huduma za afya kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, nakuunga mkono katika hilo na Serikali imesikiliza kilio chako.

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ndani ya Halmashauri mbili na Majimbo matatu, hospitali hii inategemewa na watu zaidi ya 500,000. Je, ni lini Serikali itaifanyia upanuzi hospitali hiyo hasa wodi ya akina mama wajawazito?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Wilaya ya Longido imeanzishwa mwaka 2007, takribani miaka tisa mpaka leo Wilaya ile haina hospitali ya Wilaya, matokeo yake wagonjwa wakipewa rufaa, wanapelekwa, Mount Meru - Arusha, kiasi cha kilometa 94 na Serikali imekuwa ikiahidi itajenga Hospitali ya Wilaya. Tunataka majibu ya uhakika, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Longido?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Longido haina Hospitali ya Wilaya kama zilivyo Wilaya nyingine nyingi tu hapa nchini. Niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba miradi ya Halmashauri, inaanzia kwenye mipango ya Halmashauri na baadaye bajeti ya Halmashauri. Kwa hiyo, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge kwamba kule kwenye mipango ya Halmashauri ndiko vitu hivyo vionekane ili baadaye vikija huku Bungeni tuweze kuvitengea bajeti kwa mujibu wa taratibu za kibajeti.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kawaida mimi kupata wageni wanaoomba vitu nje ya bajeti. Uwezo huo sina na hata Waziri wa Fedha, nadhani hana. Bajeti ikishapitishwa ndicho kitakachofanyika. Hivyo, Wilaya ipange mipango yake, mipango hiyo iwemo kwenye bajeti za Halmashuari zao. Jambo kubwa litakalobakia sasa ni kwa Wabunge ku-demand utekelezaji wa bajeti ili tufikie yale malengo hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, kwamba kwa sera ya Serikali ni kuweka kituo cha afya kila kata, lakini Serikali tumeamua na tumepanga na Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba kila Halmashauri basi angalau ijenge kituo kimoja. Katika Halmashauri 185 tulizonazo, tukifanya tutapata vituo karibu zaidi ya 400, wakati toka uhuru tuna vituo kama 600 tu.
Mheshimiwa Spika, nadhani hii itatusaidia sana, wa-dedicate maeneo, indication kulingana na maeneo ambako kuna problem kubwa. Jambo lingine ni kwamba kwenye zahanati wananiomba ramani, ramani ile iliyotolewa na Wizara ya Afya tumekubaliana na Waziri wa Afya kwamba ni kubwa mno kwa zahanati kila kijiji na haitekelezeki kwa sababu ya gharama kubwa karibu ya 1.8 billion ili iweze kutekeleza ule mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumekubaliana ku-review ile bajeti, kwa sababu tuna zahanati ambazo zilijengwa wakati tulipopata uhuru tu, zilitosha kutuhudumia mpaka leo tupo. Kwa hiyo, tunadhani zisiwe kubwa kiasi cha kushindwa ku-manage uchumi wa kijiji kwa sababu sehemu kubwa ni michango ya wananchi itatumika pamoja na kwamba Serikali itaweka mkono wake, lakini lazima ramani iwe ya kawaida inayoweza kuwa manageable.

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:- Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ndani ya Halmashauri mbili na Majimbo matatu, hospitali hii inategemewa na watu zaidi ya 500,000. Je, ni lini Serikali itaifanyia upanuzi hospitali hiyo hasa wodi ya akina mama wajawazito?

Supplementary Question 3

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi napenda niulize swali la nyongeza.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini tayari imeshapanua kituo chake cha afya cha Nanguruwe, ambapo pia kinacho chumba cha upasuaji cha kisasa, chenye vifaa na kimeanza kutoa huduma kwa lengo la kuifanya iwe hospitali ya Wilaya, ambapo majengo yote yanayotakiwa yamekamilika.
Je, ni lini Serikali itaibadilishia hadhi kutoka kituo cha afya na kuwa hospitali ya Wilaya baada ya kuwa kila kitu kimekamilika?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mpango wa bajeti tulipokuwa tunajadili na watu wa Mtwara kule Nanguruwe, mwaka huu kwamba wameonesha demand ya kituo hiki, na ni kweli walihakikisha kituo hiki kimekamilisha vitu vyote vya msingi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Hawa Ghasia, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Afya kuangalia zile taratibu za kikawaida kuhakikisha kituo hiki sasa kinapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, tukijua wazi kwamba ikiwa hospitali ya Wilaya hata kasma ya bajeti itabadilika eneo hilo na wananchi wataendelea kupata huduma nzuri baada ya kituo hicho kupanda kuwa Hospitali ya Wilaya.