Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Wilaya sita zenye Majimbo tisa ya uchaguzi, unakabiliwa na tatizo kubwa la maji:- Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama katika Mkoa wa Ruvuma?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Waziri wa Maji, kumekuwa na miradi ya World Bank ambayo ilianza mwaka 2013 na miradi hii baadhi yake huwa inatolewa ripoti kwamba tayari imekamilika ilhali maji hayatoki katika maeneo hayo. Napenda kuainisha maeneo ambayo maji hayatoki ikiwa ni pamoja na kumwomba Waziri mwenye dhamana akubaliane nami baada ya Bunge hili twende pamoja kwenye maeneo hayo ili akajionee yeye mwenyewe adha ambayo wanaipata wanawake kuhusiana na miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ni yafuatayo: Litola na Kumbara ni baadhi tu ya maeneo katika Wilaya ya Namtumbo; Wilaya ya Mbinga kuna mradi wa Mkako na Litoha; Wilaya ya Tunduru kuna Nanembo na Lukumbule; lakini pia katika Manispaa ya Songea kupitia SOWASA Kata ya Ruvuma, Subira, Luwiko, Bombambili, Msamala na Matalawe ni maeneo ambayo maji hayapatikani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningependa baada ya Bunge hili tuweze kuongozana akaone mwenyewe kwa macho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la piliā€¦
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nahitaji Waziri niongozane na yeye akaone mwenyewe.
Swali la pili, katika Kituo cha Afya cha Lipalamba hakuna maji kabisa na wananchi sasa wameshaanza kujichangisha kwa ajili ya kuchimba mitaro kwa ajili ya kutandika mipira ya mabomba. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutoa fedha kwa ajili ya kununua roll mita 30 kwa ajili ya kutandika pamoja na vifaa vyake vya kuungia?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ameomba kama niko tayari kuongoza naye kwenda kuona maendeleo ya utoaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Ruvuma. Nakubali ombi lake, nitafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili na katika jibu la msingi, tumesema kweli katika vijiji 80 vipo vijiji ambavyo bado miradi haijakamilika na kwamba iko katika hatua mbalimbali. Sasa kuwa na jibu ambalo ni mahususi kujua kijiji gani tumesema imekamilika na maji hayatoki, hii inabidi tuifanyie verification. Haya majibu yanayoletwa inawezekana yakawa sio sahihi, lakini naomba sana Waheshimiwa Wabunge katika vikao vya Halmashauri za Wilaya taarifa hizi za maendeleo ya huduma za maji katika maeneo yale huwa zinatolewa kila robo mwaka, naomba sana tuwe tunahudhuria vikao vile ili tuweze kujua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama kuna tatizo la msingi la kisera ambalo Waziri inabidi nijue, naomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana ili tuweze kuona namna gani tutamaliza matatizo ya maji kwa wananchi wetu.

Name

Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Wilaya sita zenye Majimbo tisa ya uchaguzi, unakabiliwa na tatizo kubwa la maji:- Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama katika Mkoa wa Ruvuma?

Supplementary Question 2

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Rais alipotembelea Mji wa Makambako aliwaahidi Wanamakambako kwamba atatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupatiwa maji; naishukuru Serikali kwamba na kwenye bajeti zilitengwa fedha za kutoka India: Mheshimiwa Waziri anawaambia nini Wanamakambako kuhusu fedha ambazo zimetengwa kutoka Serikali ya India kutatua tatizo la Mji wa Makambako kupata maji?

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni aliahidi kwamba tutaboresha upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako. Tayari Serikali ya Tanzania pamoja na Serikali ya India imeweza kupata fedha za kuchangia uboreshaji wa huduma za maji katika Mji wa Makambako. Taratibu za kupata Mhandisi Mshauri atakayefanya usanifu wa kina ili kuweza kujua ni maeneo yapi na usambazaji wake ukafanyika zinaendelea kufanyika na hatua hizo zitakapokuwa tayari, tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge.