Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Susan Anselm Jerome Lyimo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:- Mojawapo ya jukumu la Serikali katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma na waathirika kupatiwa huduma za matibabu kulingana na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo ndiyo hufadhili huduma hizo kwa takribani 100%. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizo zinaendelea kutolewa hata kama msaada kutoka Shirika la Afya Duniani utatetereka?

Supplementary Question 1

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitwa Susan Lyimo. Nashukuru kwa majibu mafupi sana ambayo hayana uelekeo; nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati ya UKIMWI ilipotembelea MSD, pamoja na mambo mengine ilipata taarifa kwamba kuna shehena kubwa sana ya dawa za UKIMWI ambayo ilikwama bandarini kwa sababu ya kutokulipa VAT, nataka kujua kama dawa zile tayari yameshaondoka bandarini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; natambua kwamba wafadhili wengi walisema watajitoa na hivyo Serikali ikaanzisha Mfuko wa UKIMWI, nataka kujua mpaka sasa hivi mfuko huo una kiasi gani cha fedha hasa ikizingatiwa kwamba wagonjwa hawa au waathirika hawa wakishaanza kutumia madawa wanapaswa kuendelea kuyanywa mpaka mwisho wa maisha yao. Nataka kujua mfuko huo toka umeanzishwa mpaka leo una kiasi gani cha fedha na tusipewe ahadi za uongo kama ambavyo tumesikia?

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumtoa hofu kwamba Serikali haishindwi kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI katika nchi hii, lakini ni utaratibu wa kawaida tu wa kujenga mahusiano mema na marafiki ambao wanajitokeza kutusaidia kubeba mzigo mzito wa kutoa huduma za afya kwa watu wetu. Na huu ni utamaduni wa nchi zote duniani na haitarajiwi hata mara moja kwamba itafika siku wataamua ghafla kusitisha misaada hii ambayo wanaitoa kwa wagonjwa wa UKIMWI, lakini kama tutafika huko tayari tumeandaa fall back position kwa kuanzisha Mfuko wa UKIMWI anaouzungumzia, na mfuko huo tumeanza kuuwekea bajeti kwenye bajeti hii iliyopita na tumeanza kwa kiwango kidogo cha shilingi bilioni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo waweze kuchangia fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye mfuko huu. Na nitoe rai kwake Mheshimiwa Mbunge na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla tujitolee kuchangia Mfuko wetu wa UKIMWI kadri tutakavyoweza na pia hata kuvutia marafiki wawekeze kwenye mfuko huo ili iwe fall back position ambayo ina uwezo wa kutosha huko mbeleni kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisahau kuhusu shehena ya dawa, hakuna shehena ya dawa mpaka hivi sasa ambayo imekwama popote pale na kwamba dawa zinapatikana nchini kwa asilimia mia moja. Kwa sababu taarifa za dawa za UKIMWI na miradi misonge yote tunazipata kila wiki, kwa update niliyonayo kufikia Ijumaa iliyopita hakukuwa na shehena ya dawa iliyokwama bandarini, lakini dawa zote zipo kwenye bohari zetu za mikoa na bohari za kanda kwa kiwango cha asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nizungumzie jambo la kitaalam, tukisema kuna availability ya dawa kwa asilimia mia moja, tunamaanisha kwenye Bohari ya Taifa kuna dawa zinazojitosheleza kutumika kwa miezi sita mbele na kwenye bohari za mikoa tuna dawa za kujitosheleza kwa matumizi ya miezi mitatu mbele na kwenye bohari za wilaya tuna dawa za kujitosheleza kwa mwezi mmoja mbele hiyo ndiyo availability tunayoizungumzia ya asilimia mia moja, sasa kwenye dawa zote za miradi misonge zikiwemo dawa za UKIMWI tuna availabaility a hundred percent.