Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Primary Question

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:- Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa utoaji wa elimu ya msingi mpaka kidato cha nne bure, jambo litakaloanzisha wahitaji wa elimu ya kidato cha tano, sita na kisha chuo kikuu. Mkoa wa Katavi kwa dhamira safi ulianzisha zoezi la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo, lakini kwa bahati mbaya zoezi zima la ujenzi wa chuo hicho limegubikwa na sintofahamu na suala zima kuwa na usiri na utata:- a) Je, ni lini ujenzi huo muhimu utaanza? (b) Je, ni kwa nini jambo hili lisiwekwe wazi kwa wananchi ili kuondoa sintofahamu kutokana na usiri uliopo?

Supplementary Question 1

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanywa na Manispaa ya Mpanda ni dhamira chanya ya kuthubutu, lakini ujenzi wa chuo nafahamu ni kazi kubwa. Je, ni kwa nini Serikali Kuu isiungane na Manispaa hii, kwa maana ya kulichukua zoezi zima la ujenzi huo wa Chuo Kikuu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi nikizingatia kwamba tunapozungumzia habari ya kuifungua mikoa ya pembezoni katika maeneo ya barabara na kilimo, huwezi ukaacha kuifungua mikoa hiyo kwa maana ya eneo hili la elimu. Elimu ndiyo chanzo cha mambo mengine yote. Je, Serikali haioni kwamba wakati umefika wa zoezi hili ikalichukua? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunaposema Manispaa ikaliweke wazi suala hiliā€¦
MWENYEKITI: Kwa kifupi, tafadhali!
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Zoezi hili lilichukuliwa na Bodi. Baadhi ya watendaji waliokuwa kwenye Bodi, Serikali hii hii imewahamishia maeneo mengine kwenda kufanya utumishi. Je, ni kwa nini Serikali isije na hatua za makusudi kuhakikisha nyaraka muhimu zimerudishwa katika Manispaa ya Mpanda ili Manispaa ya Mpanda iweze kuendelea na mchakato mwingine ikiwa ni pamoja na fidia kwa watu waliotenga eneo lao?

Name

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Answer

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Ufundi, ningependa kumjibu Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Kwanza kuhusu sababu ni kwa nini Serikali isichukue ujenzi huu, ningependa kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba swali lake la msingi, lilikuwa ni lini ujenzi utaanza. Ujenzi huu ulikuwa ni mchakato ambao Manispaa, ilikuwa imeomba ijenge na Wizara yangu ilikuwa kazi yake ni kutoa support ambapo TCU ilipitia kulingana na mchakato. Kwa hiyo, naona kama anachokisema ni swali jipya ambalo haliendani na swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwamba kuna baadhi ya wajumbe walihamishwa na wameondoka na nyaraka, huo sio utaratibu. Taratibu ni kwamba mtumishi anapohama nyaraka za Serikali zinatakiwa zibaki mahali husika. Kwa hiyo, bado naiomba Halmashauri kama kuna watumishi wanapopata uhamisho wanahama na nyaraka za Serikali ni kinyume cha utaratibu na Halmashauri inatakiwa kuchukua hatua husika.