Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:- Mji wa Sirari unakua kwa kasi kubwa sana kutokana na kuwa na mapato mengi yatokanayo na ushuru wa forodha na bandari kavu. Hata hivyo Mji huo una tatizo la ujenzi holela kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kukosa fedha za kupanga mji na kulipa fidia stahiki kwa wananchi wanaotakiwa kuhamishwa:- Je, Serikali itatoa lini fedha za fidia ili kazi ya ujenzi wa Mpango wa Mji huo ifanyike?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Mji wa Sirari, Mji wa Nyamwaga na Mji wa Nyamongo, kwanza Mji wa Sirari una wakazi zaidi ya 40,000, Mji wa Nyamongo una wakazi zaidi ya 32,000, Mji wa Nyamwaga una wakazi zaidi ya 25,000 na hii ni miji ambayo imekua, ni mikubwa sasa kuna nyumba mpaka za milioni 600 pale, lakini kwa sababu tu haijakuwa surveyed wananchi hawawezi kutumia zile nyumba kukopa kama collateral ili waweze kuendesha biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Mji wa Sirari ulitamkwa kwamba ni Mamlaka ya Mji, hakuna Mkurugenzi, bado ni vijiji kwa kifupi tu na miji yote hii, sasa ni lini Serikali itaifanya ile miji iwe Mamlaka za Miji ili iweze kupanga hii miji na kuipima ili wananchi watumie nyumba zao kukopa benki waweze kukwamua maisha yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sisi tunaishi mpakani mwa Kenya na Tanzania, upande wa pili tu pale mtu ana kiwanja square meters 2,000 anakwenda benki anakopa pesa anaendesha maisha, upande wa Tanzania mtu ana eka 20, 30, hawezi kukopa kwa sababu vijiji vyote havijapimwa. Ni lini Serikali itapima vijiji vyote vya Jimbo la Tarime wapatiwe hati za kimila ili waweze kutumia kwenye mabenki kuendesha maisha yao?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza kwamba ni lini sasa tutafanya mamlaka ya mji. Nakumbuka katika wiki hii nilijibu swali kwamba mchakato ule wa maeneo mbalimbali ambao vikao vya Madiwani na vikao vingine vya kisheria vimekaa na kufika katika RCC na kuja katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tulituma timu ya uhakiki katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu, kwa sababu Mji wa Sirari kama mapendekezo yake yalishafika maana yake ni sehemu mojawapo tunayokwenda kufanyia uhakiki. Kwa hiyo, nithibitishe kwamba ni mchakato unakwenda kwa sababu sija-specify katika eneo lako, lakini tumefanya zoezi hili kwa Tanzania nzima, lengo letu ni nini? Yale maeneo ambayo yanatakiwa kupandishwa hadhi sasa yatapandishwa hadhi kwa kufikia vile vigezo vyao vilivyofikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la upimaji. Ni kweli unaposema kwamba huku Sirari ni changamoto lakini upande wa pili imepimwa vizuri, ndiyo maana katika hili tumetoa maelekezo mbalimbali katika halmashauri zetu, waweke mipango mikakati mipana ya kuhakikisha kwamba wanapima maeneo yao. Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, hatukuishia hapo, tulichokifanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunatafuta funds kutoka maeneo mbalimbali, kupitia DFID sasa hivi katika maeneo yote ya mipakani, lengo letu ni kuweza kuyaboresha yawe mazingira rafiki yakiwemo maeneo ya Sirari. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili litakapokamilika kupitia mradi huu mpana tutayaboresha na kuyapandisha hadhi maeneo yetu, maana yake ni nini, hata thamani ya ardhi katika maeneo yetu itakua na wananchi wetu wataweza kuhakikisha mazingira yao yanakuwa mazingira rafiki hata zile hati zitapatikana, maana yake hata investment ya huku Tanzania itafanana kuwa na investment shindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ndugu yangu Mheshimiwa Heche, naomba niseme kwamba tunaomba ushirikiano wa kutosha, pindi zoezi hili litakapokuja basi niombe halmashauri zote tutoe ushirikiano wa kutosha lengo kubwa ni kwamba tuki-invest pesa hizi pesa ziweze kuleta matunda mazuri. Kwa hiyo tufanye subira tu katika mchakato huu unaokuja kupitia DFID.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:- Mji wa Sirari unakua kwa kasi kubwa sana kutokana na kuwa na mapato mengi yatokanayo na ushuru wa forodha na bandari kavu. Hata hivyo Mji huo una tatizo la ujenzi holela kutokana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kukosa fedha za kupanga mji na kulipa fidia stahiki kwa wananchi wanaotakiwa kuhamishwa:- Je, Serikali itatoa lini fedha za fidia ili kazi ya ujenzi wa Mpango wa Mji huo ifanyike?

Supplementary Question 2

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na nimpongeze Naibu Waziri kwa maelezo ya swali la msingi. Tatizo la ujenzi holela wa miji katika Tanzania yetu inakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha, watumishi kwa maana ya Maafisa Mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu takribani miaka sita tulikuwa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe wa Master Plan ya Mji wa Mbulu na hatimaye kushindikana, hivyo ni kwa nini Serikali isifanye mapitio upya kuona rasilimali watumishi kwa maana ya wataalam wa Mipango Miji, fedha za kuhakikisha kwamba miji midogo na miji mikubwa inayopanuka inafanyiwa utaratibu wa mipango miji ili nchi yetu isikumbwe mara nyingi na bomoabomoa zinazojirudia mara nyingi? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na ndiyo maana hapa mwanzo nimezungumzia hii programu kubwa ambayo kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaanza nayo hivi sasa na hii maana yake haitogusa maeneo yale ya pembezoni, isipokuwa yale maeneo ya mipakani kwanza ndiyo yatakuwa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivi kwa nini, ni kwamba ukipita nchi mbalimbali, maeneo yaliyopangwa yatafurahisha hata unaposhuka katika ndege unapoona jinsi gani mji umepangwa vizuri na bahati mbaya sana katika maeneo yetu mbalimbali miji yetu imekuwa ikijengwa katika squatter na ndiyo maana tumetoa maelekezo hasa kwa Maafisa Mipango Miji wa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa haipendezi, kwa mfano, eneo kama la Kibaigwa ndiyo kwanza linakua na Afisa Mipango Miji yupo pale, anaacha tu ujenzi unaendelea, ndiyo sababu tumetoa maelekezo kwamba kila Afisa Mipango Miji ahakikishe kwamba kupimwa kazi yake na Wakurugenzi tumewaagiza hili, katika zile performance appraisal za Maafisa Mipango Miji wahakikishe jinsi gani wametumia taaluma zao kuhakikisha miji yetu inayokua inapangwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imejipanga tutatafuta funds, lakini vilevile tutatumia human resources tulizonazo kuhakikisha kwamba watu wetu wanawajibika. Hata hivyo, tunakiri kwamba Maafisa Mipango Miji bado wapo wachache tutajitahidi kutafuta uwezekano wa kadri iwezekanavyo kuongeza nguvu kazi hii ilimradi maeneo yetu yaweze kuwa maeneo rafiki kama nchi ya Tanzania ambayo inakwenda katika Awamu ya Tano ambayo inakwenda kwa kasi zaidi.