Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ALMASI A. MAIGE aliuliza:- Sehemu kubwa ya Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui halina maji chini ya ardhi na hivyo wananchi hawawezi kupata maji kwa kuchimba visima, hivyo Serikali ikabuni mradi wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Kahama, Nzega mpaka Isikizya na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora. (a) Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi huo ili wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini katika vijiji vya Isikizya, Upuge, Majengo na Kanyenye wapate huduma ya maji? (b) Kwa kuwa bomba hilo la maji litatoa maji umbali wa kilometa 25 kushoto na kulia na kuwafikia wananchi wachache; je, Serikali haioni kuna sababu ya kuanzisha mradi wa kuchimba mabwawa na kukinga maji ya mvua kama chanzo kingine cha maji kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa vile Serikali imebuni mradi huo ambao utatusaidia sana sisi Wana-Uyui hasa Tabora Kaskazini, je, Serikali sasa iko tayari kuviorodhesha vijiji ambavyo vitakuwa katika mradi huo ili vijiji ambavyo havitakuwa ndani ya mradi tuvishughulikie kuvipatia maji?
Swali la pili kuhusu mradi wa Malambo ya maji, je, Serikali sasa iko tayari kutoa ahadi kwamba iko tayari kuanza utafiti wa wapi malambo hayo yatachimbwa? Ahsante sana.

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la pili kuhusu mpango wa Serikali kujenga mabwawa, kwanza naomba nitoe taarifa kwamba kulingana na survey ambayo tumeifanya, tuna mabwawa 3,000 ambayo yameshajengwa hapa nchini kwetu. Katika hayo, asilimia 50 yanafanya kazi na asilimia 50 hayafanyi kazi.
Kwa hiyo, mpango tulionao ni kuhakikisha kwamba haya asilimia 50 ambayo hayafanyi kazi tunayafanyia ukarabati. Pamoja na hiyo, Bunge la Bajeti lililopita tulielekeza kila Halmashauri wahakikishe kila mwaka wanasanifu bwawa moja na wanaleta ili tuweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri kila mwaka inajenga bwawa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu ni vijiji gani ambavyo vimeainishwa kwenye huu Mradi wa Kutoa Maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora? Maeneo yatakayopitiwa na mradi huu ni pamoja na Kata ya Upuge; ambayo ni Kijiji cha Upugwe, Muhogwe, Lungunya na Kasenga vitapata maji.
Kata ya Magiri ambayo ni kijiji cha Magiri, Imalampaka, Kalemela vitapata maji. Kata ya Isikizya; ambapo kijiji cha Ilalwasimba, Isikizya, Igoko, Ibushi vitapata maji. Kata ya Ibelamailundi; kijiji cha Ibelamailundi, Mtakuja, Itobela, Isenegeja vitapata maji na pia Kata ya Ilolangulu; ambapo Kijiji cha Kasisi „A,‟ Ngokolo na Isenga vinatarajiwa kupata maji kupitia katika mradi huu. (Makofi)