Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:- Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya kutaka kuongeza mapato kwa ufuatiliaji na kuondokana na ukwepaji kodi bandarini, lakini kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikikosa mapato kwa kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za uwekezaji katika sekta ya madini:- Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuondokana na misamaha ya kodi inayotolewa kwa kampuni ya uwekezaji?

Supplementary Question 1

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ripoti ya PAC ya Januari 2015 iliyojadili ripoti maalum ya CAG ikionesha upotevu kutokana na watu kukiuka utaratibu. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kuhakikisha watu waliokwepa kodi na kukiuka taratibu waweze kulipa pesa hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ripoti hazioneshi kiuhalisia faida ambazo Serikali inazipata kutokana na misamaha hii ya kodi na makampuni haya hayafanyi social responsibility kwa kiwango kinachoridhisha. Je, Serikali inafanya mkakati gani ili kuhakikisha kwamba makampuni haya yanaondolewa misamaha ya kodi, walipe kodi stahiki na wajibu wa huduma kwa jamii ubaki ni wajibu wa Serikali? Ahsante

Name

Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza misamaha ya kodi ambayo tumekuwa tunaitoa kwa makampuni ya madini imekuwa inapungua kutoka takriban asilimia 17.6 ya exemptions zote zinazotolewa za kodi, mpaka sasa imefika takribani asilimia tisa. Hatua ambazo tumekuwa tunachukua, moja ni kurekebisha Sheria za Kodi na Waheshimiwa Wabunge mlipitisha hapa marekebisho ya Sheria ya VAT ambayo iliondoa misamaha mingi ya kodi na VAT peke yake misamaha ya kodi ni takriban asilimia 56 ya mapato ya exemptions zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kurekebisha sheria hiyo, msamaha wa kodi umepungua kwa kiasi kikubwa. La pili, tunafanya jitihada kubwa kushughulikia mazingira ya biashara na uwekezaji, kwa kuwa uwekezaji hautegemei kodi peke yake, ndiyo maana Serikali imeelekeza nguvu kuongeza upatikanaji wa umeme ambayo ni malalamiko makubwa ya wawekezaji, lakini pia ulinzi kwa ajili ya wawekezaji na kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya kutoa leseni za biashara na vibali vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeongeza kujenga uwezo wa kuchambua vipengele vya misamaha ya kodi, vile vitengo ambavyo ndani ya Wizara ya Fedha lakini pia ndani ya Mamlaka ya Mapato ili kuhakikisha kwamba misamaha inakuwa tu ile ambayo inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Waziri wa Fedha atakataa misamaha yote ambayo haina maslahi kwa Taifa. (Makofi)