Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa maabara ya sayansi katika shule za Mkoa wa Katavi?

Supplementary Question 1

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kutenga bilioni tano kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivi, lakini, pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba inaboresha elimu nchini hususan elimu ya sekondari kwa upande wa sayansi. Nidhahiri kabisa katika Mkoa wetu wa Katavi bado kuna upungufu mkubwa sana wa walimu hususan walimu wa kike na walimu wa sayansi. (Makofi)

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na Mkoa wa Katavi ambao una upungufu mkubwa, ikiwepo shule ya Mwangaza ina mwalimu mmoja tu wa sayansi na Shule ya Rungwa ambayo ina zaidi ya wanafunzi 1500 lakini haina kabisa walimu wa sayansi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Je, Serikali inaongeza jitihada gani kuhakikisha kwamba ina boresha elimu ya sayansi hususan kuhakikisha watoto wa kike wanakwenda kuongezeka na kupata elimu ya sayansi nchini?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Martha Mariki na hili la kwanza la upungufu wa walimu Mkoani Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inaondoa upungufu wa walimu katika maeneo yote nchini ikiwemo Mkoa wa Katavi; na katika Mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali iliajiri jumla ya walimu wa sayansi 6,949.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu ambayo inatekelezwa ya 2023/2024 Serikali imetenga ajira kwa ajili ya kupunguza upungufu wa walimu wa sayansi. Tunaendelea kuratibu na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishii li kuweza kupata vibali vya kuweza kuajiri walimu hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu swali la pili la Mheshimiwa Martha Mariki linalohusu jitihada za Serikali; Serikali hii, hasa utashi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, alihakikisha kwamba tunakwenda kujenga shule za wasichana za sayansi katika kila mkoa. Awamu ya kwanza, Mheshimiwa Rais alitoa fedha kwa ajili ya kujenga shule kumi kwenye mikoa kumi na awamu ya pili kuna fedha bilioni 48 imekwenda kwenye mikoa 16. Hii yote ni kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanapata elimu iliyobora na elimu ya sayansi katika mikoa yote. Hivyo, awamu ya kwanza jumla ilienda bilioni 40 na awamu ya pili bilioni 48.