Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 1

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuna majibu mengine yanasikitisha sana. Kituo cha Mugeta kimeisha mwaka 2019, wakati kituo hiki tunajenga tulipewa shilingi milioni 700, siyo kwamba hela zinatafutwa hapana, shilingi milioni 700, shilingi milioni 400 wakasema tujenge majengo kwa kushirikiana na wananchi na shilingi milioni 300 zinaenda MSD vifaatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoenda kufuatilia mwaka 2020 tukaambiwa vifaatiba vitakuja vya shilingi milioni 161 na vimeshakuja. Wakasema vifaa vingine vya shilingi milioni 139 viko njiani, leo unaambiwa kuna bajeti inatengwa, hizi shilingi milioni 300 zilizoenda MSD ziko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua tutatengaje bajeti ambayo tayari ilishaenda? Kwa hiyo, naomba hili jokofu la Mugeta lipelekwe, fedha zipo MSD. (Makofi)
Swali la pili, tumejenga Kituo cha Afya Hunyari lakini hakina theater, sasa naomba kujua ni lini hii theater ya Kituo cha Afya Hunyari itakamilika?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namwelewesha Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha za vifaatiba haimaanishi ni fedha za kununua jokofu la mochwari peke yeke. Tukikamilisha ujenzi wa kituo cha afya vifaatiba vya kipaumbele ni vifaa ambavyo vitakwenda kutibu wananchi. Vifaa vya upasuaji, vifaa vya wodini, vitanda, magodoro na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili tunakwenda kupeleka vifaa kwa ajili ya kuhifadhia maiti kwa maana ya majengo ya mochwari pamoja na majokofu. Kwa hiyo, hiyo shilingi milioni 300 ambayo ilikwenda MSD ilinunua vifaatiba ambavyo viliwezesha kituo cha afya hicho kuanza kutoa huduma kwa wananchi. Mwaka huu wa fedha tayari Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshawaletea shilingi milioni 700 kwa ajili ya kununua vifaatiba vingine likiwemo jokofu la mochwari. Naomba Mheshimiwa Mbunge tuishukuru Serikali kwamba imefanya kazi kubwa, imeleta fedha nyingi za vifaatiba, jokofu litanunuliwa kati ya Februari na Machi ili wananchi wa Bunda waweze kupata huduma nzuri za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu Kituo cha Afya cha Hunyari ni kweli kwamba kuna majengo ambayo yamejengwa lakini bado hatuna jengo la upasuaji. Safari ni hatua, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa awamu ili twende kukamilisha majengo mengine kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Hunyari. Ahsante. (Makofi)

Name

Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 2

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutupatia gari la ambulance katika Kituo cha Afya cha Kinesi. Kituo cha Afya cha Kinesi kinahudumia tarafa mbili kwa maana ya vijiji zaidi ya 25. Kwa sasa tunapopata maafa Wananchi hutulazimu kusafirisha miili ya ndugu zetu hawa kwenda Musoma Mjini kwa kutumia mtumbwi ama boti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari tuna jengo la mochwari katika kituo hiki, ni nini mpango wa dharura kuhakikisha kwamba mnatupatia jokofu ili kunusuru na kuondoa adha wanayopata Wananchi wakati wanapopata maafa haya?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinesi, kimekamilika na kinatoa huduma. Tunafahamu kwamba kituo hiki bado hakijakamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti na upo katika hatua ya asilimia 85. Tunafahamu pia kwamba jengo hili halijapata mashine kwa maana ya jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambaye alishatoa maelekezo hayo, kwamba wahakikishe kupitia mapato ya ndani wanakamilisha asilimia 15 iliyobaki kukamilisha jengo la mochwari. Mheshimiwa Rais ameshapeleka shilingi milioni 400 kwa ajili ya kununua vifaatiba na kati ya fedha hiyo watenge hiyo shilingi milioni 32.5 kwa ajili ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kinesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa ujumla, tumekuwa na hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge kutoka katika Majimbo yote, Mheshimiwa Rais amepeleka fedha shilingi milioni 500, vituo vya afya vimekamilika vimeanza kutoa huduma. Wakurugenzi wa Halmashauri, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wasimamie mapato ya ndani kukamilisha majengo ya kuhifadhia maiti katika vituo vyote ambavyo vimekamilika ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaleta fedha ni kazi ndogo ya shilingi milioni 30 tu kukamilisha yale majengo lakini pia waweke kipaumbele kununua majokofu kwa ajili ya majengo hayo katika vituo hivyo. Ahsante.(Makofi)

Name

Charles Muguta Kajege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 3

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa Getere na mimi liko kwangu Mwibara; je, ni lini Serikali itajenga majokofu katika Vituo vya Afya vya Kasaunga, Kisolya, Kasuguti na Isanju?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaelekeza Halmashauri zetu zote kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha majengo ya mochwari, pia kutenga fedha ambazo zinapelekwa kwa ajili ya vifaatiba kwa ajili ya kununua majokofu ya mochwari. Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafuatilia kuona Halmashauri ya Rorya Jimbo la Mwibara pia wanatenga na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma zinazostahili. Ahsante.

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 4

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wananchi wa Kijiji cha Lungemba na Kitelewasi kwa kushirikiana na Halmashauri na Mfuko wa Jimbo wamejenga majengo ya mama na mtoto; je, Serikali iko tayari kuwasapoti kwa kuwaletea vifaatiba katika majengo hayo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Cosato Chumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza Wananchi wa Lungemba na Kitelewasi kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya huduma ya mama, baba na mtoto. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo vyote ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi vikishasajiliwa Serikali inachangia nguvu zake, kwa maana ya kupeleka fedha kuhakikisha kwamba vinaanza kutoa huduma. Kwa hiyo, tuko tayari kuwaunga mkono wananchi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika majengo haya, ahsante.

Name

Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 5

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia gari la wagonjwa ambalo tumelipeleka katika Kituo cha Afya cha Umbwe. Kituo hiki cha afya kinahudumia Kata sita katika Tarafa ya Kibosho na hakina mortuary. Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia kutujengea mortuary katika kituo hiki?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na kuwapongeza kwa kupokea magari ya wagonjwa ambayo Mheshimiwa Rais amenunua kwa ajili ya Majimbo yetu na Halmashauri zetu zote kote nchini. Pamoja na hilo tunaendelea kuboresha sana huduma za mortuary, natumia nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Vijijini kutenga fedha ya mapato ya ndani kwa ajili ya jengo la mortuary na kutumia fedha ya vifaatiba kwa ajili ya kununua majokofu ili kuboresha huduma kwa wananchi, ahsante. (Makofi)

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:- Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kupeleka majokofu manne ya mochwari kwenye Kituo cha Afya Mugeta?

Supplementary Question 6

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kiponzero ni moja ya vituo kongwe katika Jimbo la Kalenga, bahati mbaya mpaka leo hakina cha chumba cha mortuary; je, ni lini Serikali itatupa jokofu pamoja na chumba cha mortuary?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza na narejea kusema kwamba maelekezo yameshatolewa kuhakikisha kwamba Wakurugenzi wanajenga majengo ya kuhifadhia maiti. Pia wananunua majokofu katika vituo vyote vilivyopo ambavyo vinatoa huduma kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, namuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa Vijijini kuhakikisha wanaanza kujenga jengo la mortuary, lakini pia wananunua jokofu kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kiponzero, ahsante.