Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Primary Question

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: - Je, uchimbaji wa madini kando ya mito na maziwa ni chanzo cha upungufu wa samaki?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanyika Aprili, 2018 huko Tennessee Marekani, unaonesha kwamba sehemu zenye machimbo ya makaa ya mawe karibu na mito kuna upungufu wa viumbe wa majini kwa asilimia 53 wakiwemo samaki. Swali la kwanza; je, sisi Serikali yetu imefanya utafiti huo na kuja na majibu haya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi tunaanza kuchimba makaa ya mawe Kiwira Coal Mine na Mto Kiwira na Mto Songwe vimeathirika kwa namna hiyo. Je, ni hatua gani zinazochukuliwa kwa Serikali ili kusiendelee kupatikana kwa athari hizo?

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mlaghalila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa taarifa anayosema kwamba kuna tafiti za kidunia zinazothibitisha kwamba uchimbaji wa makaa ya mawe una uhusiano na kupungua kwa samaki katika maziwa na mito; nikiri kwamba sisi hatuna scenario kama hiyo katika Nchi yetu ya Tanzania kwa sababu hatuna uchimbaji katika maeneo ya karibu na mito ambayo ina samaki au maziwa ambayo kuna upungufu uliobainika kwa tafiti za kisayansi.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo la machimbo ya makaa ya mawe lililoko Kiwira na Kabulo tuna Mradi unaoitwa Kiwira-Kabulo Coal Project ambao uko chini ya taasisi yetu ya STAMICO. Katika eneo Kasumulu, Wilaya ya Kyela ilianzishwa site ndogo ya heka mbili kwa ajili ya kuwa selling point ya yale madini kutokana na shida ya barabara ya kutoka Kabulo kwenda Kiwira kuliko na kituo kikubwa cha makaa ya mawe ya STAMICO. Kwa sasa hivi, barabara hiyo ya kilomita saba ilishakamilika na utaratibu wa kuhamisha kile kituo umeshafanyika na kuna tani 1,200 za makaa ya mawe mpaka kufikia mwezi Agosti, 2022 yatakuwa yameondolewa yote, ila tahadhari zote zilichukuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwanza; kulingana na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Kifungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto. Site iliyotengwa kule katika mradi huu wa makaa ya mawe kule Kasumulu upo mita 120; lakini kana kwamba hii haitoshi makingamaji ya kuchepusha maji yasielekee mtoni yamejengwa na kuna mashimo makubwa kama mvua itanyesha na maji yakatiririka yakaingia mle yakakaukia humo. Pia kana kwamba hiyo haitoshi, kulingana na Kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, sisi kama Wizara ya Madini tunazingatia sana suala la utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hiyo, Kifungu cha 107(2) cha Sheria ya Madini Na. 123, kinazingatia utunzaji wa mazingira kwamba baada ya ile site kuachiwa tutapenda kuirejesha na kuzungushia fence na kutumika kwa matumizi ya kufundisha wananchi wa eneo la Kyela na Ileje namna ya kutengeneza makaa mbadala ya makaa ya mawe yanaitwa Coal Breakage. Kwa hiyo, hakuna athari ya mazingira na sisi tupo makini. Ahsante sana.