Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- Je, Serikali ina kauli gani kuhusu mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa kuwa mfumo unawaacha nje vijana wengi kwa kukosa sifa?

Supplementary Question 1

MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya ulezi kwa vikundi hivi si tu vya vijana lakini vikundi vya wanawake na watu wenye ulemavu, ili viweze kuwa na ufanisi katika kufanya shughuli zake za ujasiriamali?

Swali langu la pili, tathmini inaonesha kwamba malipo ya fedha hizi za mikopo zinazotoka kwenye Halmashauri bado zinasuasua. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba mikopo hii inalipwa kwa wakati ili waweze kunufaika vijana wanawake na watu wenye ulemavu wengi zaidi? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zainab Katimba Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati ambao Serikali imekuwa inaufanyiakazi katika kuhakikisha vikundi hivi ambavyo vinakopeshwa wajasiliamali wadogo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuwa endelevu lakini pia kuweza kuwa na tija ni Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri husika kwanza kuwatembelea mara kwa mara, kuwafanyia mafunzo ya mara kwa mara, pia kuwashauri kuona kwamba wanakwenda vizuri na huo ndiyo ulezi wenyewe kwa maana ya kwamba viongozi wa Halmashauri lakini katika ngazi za Kata, Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine wanahusika kuvifuatilia pia kuvishauri. Tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba vikundi hivi vinakopa lakini vinarejesha kwa tija.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na malipo ya fedha kusuasua ni kweli, kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Watendaji kuchelewesha malipo haya na Serikali ilishatoa maelekezo kwamba kama kikundi kina kinakidhi vigezo kipate fedha mapema iwezekanavyo ili shughuli ziweze kuendelea, lakini mara nyingine zinacheleweshwa kutokana na baadhi ya vikundi kutokidhi vile vigezo vinavyotakiwa. Ahsante.