Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanzisha Mkoa wa TANESCO katika Wilaya ya Kahama na kujenga Ofisi ya TANESCO Halmashauri?

Supplementary Question 1

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu hata maeneo ambayo ameyataja hapa kwamba yamejengewa ofisi kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu hakuna kata inayoitwa Bulungwa wala Chambo.

Sasa Mheshimiwa Waziri niseme kwamba ni lini sasa mtaanzisha ofisi hizo ambazo wewe umezitaja hapa ikiwemo Kata ya Isaka, Kata ya Segese, Kata ya Bulige na Kata ya Jana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza wakati mnaendelea kufanya upembuzi yakinifu au tathmini, Mheshimiwa Waziri alifanya ziara kwenye Halmashauri ya Msalala na tukampatia kiwanja na tofali 1000 na akaahidi kujenga ofisi kwenye Halmashauri ya Msalala.

Sasa ni lini Serikali mtaanza ujenzi wa ofisi ya Wilaya kwenye Halmashauri ya Msalala? Ahsante. (Makofi)

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la pili la ni lini Serikali itaanza kujenga ofisi; kama tulivyoeleza kwenye jibu la msingi TANESCO inaendelea na tathmini mahitaji ya vigezo kwa ajili ya kufungua ofisi hiyo, kwa hiyo tathmini itakapokamilika mara moja mahitaji yakabainika ni kwa kiasi gani basi itaamuliwa ijengwe hiyo ofisi kwa mazingira yatakayo kuwepo.

Mheshimiwa Spika, lakini kweli swali la kwanza kwamba ofisi hazijafunguliwa; kwa sababu ya uhaba wa watumishi tuliokuwa nao na kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya kujenga majengo yetu katika maeneo yote wenzetu wa TANESCO walianzisha utaratibu wa kufanya visiting offices ambazo ni katika haya maeneo ya hizo ofisi ndogo tukiazima maeneo ya ofisi za kata. Kwa hiyo, maeneo haya hautaenda na kukuta jengo limejengwa lakini tunapata vyumba kwenye ofisi za watendaji wa Kata na tunaanza kuhudumia watu kutokea kwenye maeneo hayo, wakati Serikali ikiwa inajihimu kuongeza bajeti kwa ajili ya kuweza kujenga majengo hayo kwenye maeneo yote yanayohitajika. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanzisha Mkoa wa TANESCO katika Wilaya ya Kahama na kujenga Ofisi ya TANESCO Halmashauri?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Moja ya sababu za kujenga ofisi na kupeleka vifaa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya TANESCO inakuwepo kwa wananchi; sasa pale Halmashauri ya mji wa Bunda tuna ofisi lakini bado hamjaweza kutoa huduma stahiki ya umeme, watu wameomba maombi ya umeme, wana control number, lakini mpaka leo hawajaunganishiwa umeme.

Ni lini mtahakikisha huduma bora inaenda kwa wananchi na sio tu ofisi peke yake?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika bajeti tutakayoisoma hapa siku chache zijazo itaoneshwa ni kwa kiasi gani Serikali ya Awamu Sita imejipanga kuwahudumia wananchi kwa kuongeza fedha kiasi zaidi ya bilioni 500 kwa ajili ya kupeleka huduma kwa wananchi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya siku mbili ataona neema iliyoshushwa na Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Nishati. (Makofi)