Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 2 Finance and Planning Wizara ya Fedha na Mipango 20 2021-02-03

Name

Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Primary Question

MHE. ALI HASSAN OMAR KING Aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kufuatilia fedha za wananchi zilizopo katika Benki ambazo zimezuiliwa kuendesha shughuli zao hapa nchini?

Name

Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kuchukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuijaalia nchi yetu amani na utulivu na kutujaalia sisi sote uzima na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu, Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. Aidha, nitoe shukrani kwa familia yangu kwa kuendelea kunitia moyo hivyo kunipa nguvu na kuendelea kutekeleza majukumu yangu kiufanisi. Vilevile niwashukuru viongozi wangu wa CCM pamoja na UWT kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Taifa kwa kuniamini na kunipa nafasi hii kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017 na 2018, Benki Kuu ya Tanzania ilizifutia leseni ya kufanya biashara ya kibenki benki saba kwa mujibu wa vifungu vya 11(3)(i), 41(a), 58(2)(a), na 61(1) vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Benki zilizofutiwa leseni ya kufanya biashara nchini ni pamoja na: FBME Bank Limited; Mbinga Community Bank Plc, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited, Meru Community Bank Limited; Efatha Bank Limited; na Covenant Bank for Women (T) Limited.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzifutia leseni benki hizo Benki Kuu ya Tanzania iliteuwa Bodi ya Dhima ya Amana (Deposit Insurance Board) kuwa Mfilisi. Katika kutimiza wajibu wake wa msingi Bodi ya Bima ya Amana ilianza zoezi la kulipa fidia ya bima ya amana ya Sh.1,500,000 kwa waliostahili kulipwa bima ya amana na zoezi hili bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia. Sanjari ya zoezi hili DIB inaendelea na zoezi la ufilisi wa benki hizo tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2020, Sh.9,440,305,975.88 zimeshalipwa kwa wateja ambao wenye amana katika Benki sita za Wananchi (Community Banks) kama zilivyotajwa hapo juu ukiiondoa Benki ya FBME. Malipo hayo ni sawa na asilimia 77.27 ya kiasi cha Sh.6,393,690,743.89 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia. Aidha, jumla ya wateja waliolipwa ni 21,675 kati ya wateja 57,076 ikiwa ni asilimia 37.98 ya wateja waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Benki ya FBME, hadi mwishoni mwa mwezi Desemba 2020, jumla ya Sh.2,428,779,092.11 zimelipwa kwa wateja wenye amana ambazo ni sawa na asilimia 52.13 ya kiasi cha Sh.4,659,011,005.76 zilichotengwa. Aidha, jumla ya wateja waliolipwa ni 3,443 kati ya wateja 6,628 ambao ni sawa na asilimia 51.95 ya wateja waliokuwa na amana zinazostahili fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, wateja waliokuwa na amana inayozidi Sh.1,500,000/= watalipwa kiasi kilichobakia chini ya zoezi la ufilisi ambalo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Zoezi hilo la kukusanya madeni na mali za benki hilo linaendelea ili kupata fedha za kuwalipa wateja wenye amana zenye thamani zaidi ya Sh.1,500,000/=. Ahsante.