Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima (11 total)

MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
Gereza la Ilagala limehodhi eneo kubwa la shamba na kufanya wananchi wa Kata ya Ilagala kukosa maeneo ya kulima.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa sehemu ya eneo kwa ajili ya wananchi wa Ilagala ili na wao waweze kupata maeneo ya kulima?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Ilagala ni gereza la kilimo na mifugo ambapo linamiliki jumla ya ekari 10,760 na kati ya ekari hizo, ekari 4,500 ziko katika milima na mabonde ambapo zimehifadhiwa kwani ni vyanzo vya mito katika eneo hilo. Ekari 3,000 zimetengwa na zinatumika kwa ajili ya ufugaji wa ng‟ombe, mbuzi na kondoo; na ekari 5,000 kwa ajili ya makazi na ekari 2,760 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya mahindi; mahindi ya mbegu, michikichi, mihogo, mbaazi, mboga pamoja na matunda. Hata hivyo, pamoja na shughuli tajwa hapo juu, eneo hilo bado halitoshelezi kwa ajili ya mahitaji yaliyokusudiwa.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-

Tarafa ya Nguruka na Uvinza zinalima zao la tumbaku na kuiingizia Halmashauri ya Uvinza fedha nyingi kwenye makusanyo ya ndani lakini wamekuwa wakinyonywa kwenye bei ya uuzaji na upangaji wa viwango vya pamoja vya soko:-
Je, ni lini Serikali itawatumbua wakulima wa tumbaku wa Uvinza ili nao wapate chama kikuu ndani ya Mkoa wa Kigoma na kuwapunguzia gharama za usafirishaji kwenda hadi Tabora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa wakulima wa tumbaku kuendelea kunufaika na huduma zitolewazo kupitia vyama vya ushirika. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013 na Kanuni za mwaka 2015 ili chama cha ushirika kiweze kusajiliwa kinapaswa, pamoja na kutimiza masharti mengine, kikidhi kigezo cha kuwa na uhai wa kiuchumi katika maana ya economic viability.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa chama kikuu kuanzishwa, uhai wa kiuchumi unazingatia viwango vya uzalishaji kwa mwaka wa vyama vya msingi vinavyohudumiwa na chama kikuu hicho na ufanisi wa mfumo wake wa masoko. Kwa mujibu wa matakwa hayo ya kisheria ili chama kikuu cha ushirika wa tumbaku kiweze kusajiliwa kinapaswa kiwe kinazalisha na kuuza angalau kilogramu milioni kumi za tumbaku kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika Mkoa wa Kigoma kipo chama kikuu kiitwacho Kigoma Tobacco Growers Cooperative Union (KITCU). Chama kikuu hicho kinahudumia Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Uvinza. Takwimu zinaonesha kuwa kutokana na wanunuzi wa tumbaku kupunguza mahitaji ya tumbaku kwa mwaka, uzalishaji wa chama kikuu hicho umepungua hadi kufikia wastani wa kilogramu milioni nane kwa mwaka. Wilaya ya Uvinza ambayo inajumuisha Tarafa za Nguruka na Uvinza inazalisha takriban 55% ya tumbaku yote ya KITCU, ambazo ni takriban kilogramu milioni 4.5. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wilaya hiyo imezalisha kilogramu 3,586,175 za tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na taarifa hiyo na umuhimu wa kuzingatia Sheria ya Ushirika katika kuanzisha vyama vya ushirika, kwa sasa chama kikuu kingine cha ushirika kinachojishughulisha na zao la tumbaku katika Mkoa wa Kigoma hakiwezi kuanzishwa. Badala yake Serikali inajielekeza katika kuimarisha nguvu za uzalishaji za KITCU, chama ambacho makao yake makuu yako Nguruka katika Wilaya ya Uvinza ili kiweze kukidhi vigezo vya kiuchumi na kisheria na hivyo kuendelea kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi zaidi, wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Uvinza.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
(a) Je, Serikali inawaeleza nini wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwabana wamiliki wa kiwanda hicho ili waboreshe mazingira ya kiwanda pamoja na mazingira ya wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo lilishashughulikiwa, ambapo wafanyakazi husika walilipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria ikiwemo kiinua mgongo. Aidha, kwa kuzingatia Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016 yaliyopitishwa na Bunge lako Tukufu wakati wa Kikao cha Bajeti, kama kuna mfanyakazi au wafanyakazi wanaoona kuwa hawakulipwa stahiki zao za kupunguzwa kazi ipasavyo, wanayo fursa ya kuwasilisha moja kwa moja madai yao kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pasipo kupitishia kwa Kamishna wa Kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuimarisha mikakati na huduma za usimamizi na ukaguzi kazi kwa kuchukua hatua stahiki kwa waajiri wanokiuka sheria ili kuboresha mazingira ya kiwanda na mazingira ya wafanyakazi. Aidha, kupitia Marekebisho ya Sheria za Kazi ya mwaka 2016, Maafisa Kazi wamepewa mamlaka ya kuwatoza faini za papo kwa papo waajiri wanaokiuka sheria. Kanuni kwa sasa zinaandaliwa ili kuweka mwongozo na utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nivisihi vyama vya wafanyakazi nchini, navyo vitimize wajibu wao wa kutetea na kusimamia haki za wafanyakazi pamoja na kukuza tija na uzalishaji sehemu za kazi.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika ni uvuvi lakini nyavu zimekuwa zikikamatwa na kuchomwa moto.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wavuvi hao nyenzo au vifaa vya kisasa vya uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili kuwawezesha wavuvi wakiwemo wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kufanya uvuvi endelevu na wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeondoa kodi kwenye zana na malighafi za uvuvi zikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio kupitia Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2007. Aidha, kupitia Umoja wa Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Community Common External Tariff) engine za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake kwa maana ya fishing gear accessories 10% na outboard engine 0%) zimepewa punguzo la kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wananchi wakiwemo wavuvi ili waweze kununua zana bora za uvuvi. Hivyo wavuvi wahamasishwe kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili kuwawezesha kupata mikopo hiyo.
Vilevile Serikali inatekeleza mpango wa kutoa ruzuku ya zana za uvuvi, ambapo wavuvi wenyewe huchangia 60% na 40% iliyobaki ya gharama huchangiawa na Serikali. Hadi sasa engine 73 zimenunuliwa kupitia mpango huu, nakati ya hizo engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa na vikundi vya wavuvi vilivyokidhi vigezo vikiwemo vitatu kutoka katika Wilaya ya Kalambo na kimoja kutoka katika Wilaya ya Sumbawanga.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE (K.n.y. MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia Wakazi wa Kata Nne za Tarafa ya Nguruka pamoja na wananchi wa Usinge katika Wilaya ya Kaliua.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi kituo hicho kwa kuongeza miundombinu na kumalizia ukarabati wa jengo la Mama na Mtoto ambalo limeachwa bila kukarabatiwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Nguruka kinahudumia watu wapatao 108,330 wa Kata nne za Tarafa ya Nguruka na majirani Wakazi wa Tarafa Usinge Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora kama kituo cha rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona haja ya kukiboresha Kituo cha Afya cha Nguruka ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi ikizingatiwa kwamba Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya kukiboresha kituo hicho alipokuwa katika kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetenga shilingi milioni
• katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuongeza miundombinu ikiwemo wodi ya akinamama wajawazito na watoto, ujenzi wa uzio, ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, mfumo wa maji taka na ukarabati wa nyumba ya watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya hapa nchini.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
(a) Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu miradi ya maji ya Kali, Rukoma, Ilagala, Kandego, Uvinza na Nguruka ambayo wakandarasi wamesimama kwa ukosefu wa fedha?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza chini ya Mpango wa Vijiji 10 kwa kila halmashauri, Miradi ya Maji ya Rukoma na Kandaga ilitekelezwa katika Halmashauri ya Kigoma na miradi ya maji katika vijiji vya Kalya, Ilagala, Uvinza na Nguruka ilitekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wakandarasi wa miradi hiyo walikuwa wamesimama kutokana na changamoto ya kifedha. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018, Serikali tulitumia kiasi cha shilingi bilioni 1.01 katika Halmashauri ya Uvinza kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya maji ambayo haijakamilika ikiwemo miradi ya Kayla, Ilagala, Uvinza na Nguruka. Aidha, Halmashauri ya Kigoma ilitumia jumla ya shilingi bilioni 581.2 kuendelea kukamilisha miradi ya maji vijijini ikiwemo Rukoma na Kandaga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.8 na shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya Halmashauri za Wilaya ya Uvinza na Kigoma mtawalia ili kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji. Aidha, halmashauri zote nchini zimeshauriwa kuwasilisha kwa wakati hati za madai ya wakandarasi wanaojenga miradi ili ziweze kulipwa mapema iwezekanavyo.
MHE. HASNA S. MWILIMA aliuliza:-
Wananchi wa Humule, Ubanda, Tandala na maeneo mengine ya Itebula wamekuwa wakisosa maeneo ya kulima kwa madai kuwa wanaingilia maeneo ya hifadhi:-
• Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kusogeza mipaka kwa kushirikiana na TAMISEMI ili wananchi wapate maeneo ya kulima?
• Je, ni lini Serikali itamaliza usumbufu wanaoupata Wananchi wa Kijiji cha Kalilani kwa kudaiwa kuwa wamo ndani ya Hifadhi wakati Kijiji hiki kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Humule, Ubande, Tandala na Itebula ni vitongoji ndani ya Kijiji kipya cha Lufubu kilichozaliwa ndani ya kijiji cha Kashagulu, Kata ya Kalya, Wilaya ya Uvinza ambacho kinatambulika kisheria. Eneo tajwa lilifanyiwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi mwaka 2006. Mchakato wa kuidhinisha mipaka ya ramani ya kijiji ulikamilika mwaka 2007 na ramani hiyo kusajiliwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji kama Kashagulu pia kilifanya mpango wa kurasimisha msitu wao wa kijiji wenye ukubwa wa hekta 38,313 kupitia mchakato shirikishi kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Misitu Na.14 ya 2002. Eneo hili ni vyanzo vya maji na linatambuliwa kama mapito ya wanyamapori yaani (Ushoroba) hususani tembo, nyati, sokwe na wengine wahamao kutoka Hifadhi ya Taifa Mahale kwenda Hifadhi ya Taifa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongeza maeneo ya kilimo lazima lifanyike kisheria kwa kuwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi uliidhinishwa na mkutano mkuu wakati huo. Mpango huo uliangalia matumizi ya wakati huo na ya baadaye kwa miaka 10 mpaka 15 ijayo.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale ilitangazwa rasmi katika GN Na. 262 ya tarehe 14 Juni, 1985. Maeneo ya Kalilani ni muhimu sana kwa uhifadhi wa sokwe, tembo, wanyama wengine pamoja na mazalia ya samaki. Aidha, wakati hifadhi hii inatangazwa, eneo hilo lilikuwa na wananchi jamii ya Watongwe waliopisha kutangazwa Hifadhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kalilani kilisajiliwa tarehe 5 Juni, 1995 ikiwa ni miaka takriban 10 baada ya Hifadhi ya Taifa kutangazwa. Wakati huo wavuvi wachache waliobakia eneo la Kaskazini Magharibi mwa hifadhi hii walianzisha kitongoji na baadaye kijiji kinachofahamika sasa kama Kalilani. Hii inadhihirisha kuwa eneo ambalo wanakijiji wanadai kuwa ni sehemu ya kijiji bado kisheria ni sehemu ya Hifadhi ya Mahale.
HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
Jimbo la Kigoma Kusini lenye ukubwa wa kilometa za mraba 10,178 lina jiografia mbaya na idadi ya wakazi wake ni kubwa sana:-
a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuligawa jimbo hilo na kuanzisha halmashauri nyingine ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za kijamii kiurahisi?
b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo katika Tarafa ya Nguruka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali refu la Mheshimiwa Hasna Sudi Katundu Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuyagawa majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia vigezo vya idadi ya watu, jiografia, hali ya mawasiliano, ukubwa wa jimbo na uwezo wa ukumbi wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Jimbo lolote ligawanywe, Tume hutoa tangazo kuhusu nia hiyo. Baada ya tangazo, mapendekezo hujadiliwa katika vikao vya Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na hatimaye kuwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo hutangaza jimbo jipya baada ya kupata kibali cha Rais.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vinavyozingatiwa katika kuanzisha Mamlaka za Miji Midogo ni pamoja na idadi ya watu wasiopungua elfu hamsini, kata zisizopungua tatu, eneo lisilopungua kilomita za mraba mia moja na hamsini, viwanja vilivyopimwa visipungue asilimia
30 ya eneo lote, uwepo wa mpango kabambe wa uendelezaji wa mji (master plan) na huduma za jamii za kukidhi ukuaji wa mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mapendekezo ya kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo yanapaswa kuanzia kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa kwa kuzingatia vigezo hivyo kwa mujibu wa sheria. Mapendekezo ya vikao hivyo huwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kumshauri ipasavyo Waziri mwenye dhamana.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-

Tarafa ya Nguruka ina wakazi zaidi ya 100,000 na ndio kitovu cha biashara:-

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme wa Grid ya Taifa kutoka Usinge, Wilaya ya Kaliua?

(b) Wakazi wa Kata za Mwambao, Sunuka, Kaliya, Buhigu, Igalula, Haramba na Sigunga hawana umeme na Jiografia ya kuwaunganishia umeme kutoka Uvinza ni ngumu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka umeme kutoka Mpanda, Mwese kwenda Kata ya Kaliye, ili iwe rahisi kuzipitia kata zingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 katika Mikoa ya Kusini Magharibi, ikiwemo Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma kwa lengo la kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo na Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua za awali Serikali kupitia TANESCO kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika imeanza kutekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 North West Grid Kv 400, Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga
– Mpanda – Kigoma – Nyakanazi wenye urefu wa kilometa 1,372. Kwa sasa Benki ya Dunia imeshatoa dola za Kimarekani milioni 455 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utekelezaji wa mradi huu Serikali kupitia TANESCO mwezi Disemba, 2018 imeanza kutekeleza mradi wa kuunganisha Mkoa wa Kigoma na Grid ya Taifa kutoka Mkoa wa Tabora. Mradi unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora, Urambo, Usinge – Kaliua, Nguruka hadi Kidahwe Kigoma Mjini wenye urefu wa kilometa 370. Kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya 132/33 Kv katika Miji ya Urambo na Nguruka. Gharama ya kazi hiyo inakadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 81 na ujenzi wa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huu na miradi mingine inayoendelea kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma ikiwa ni pamoja na kuwasambazia wananchi umeme katika Kata za Mwambao, Sunuka, Kaliya, Buhigu, Igalula, Haramba na Sigunga. Nakushukuru.
MHE. HASNA S. MWILIMA aliuliza:-

Jiografia ya Halmashauri ya Uvinza ni mbaya na kusababisha wanafunzi wanaomaliza Kidato cha Nne kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika kusafiri zaidi ya kilometa 200 kufuata Shule za Kidato cha Tano na Sita zilizopo katika ukanda wa Reli:-

(a) Je, kwa nini Serikali isianzishe Shule za Kidato cha Tano na Sita kwenye Kata nane za Ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuwapunguzia usumbufu wanafunzi hao?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kuongeza miundombinu katika Shule za Kidato cha Tano na Sita Rugufu Wasichana na Wavulana ambazo miundombinu yake ni chakavu na haitoshelezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katumba Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza inaundwa na Tarafa tatu za Nguruka, Ilagala na Buhingu. Shule za Sekondari za Kidato cha I – IV ziko 20 (18 za Serikali na 2 za binafsi) zote zikiwa na jumla ya wanafunzi 11,622. Shule za Kidato cha Tano na Sita zipo tatu ambazo ni Lugufu Wavulana, Lugufu Wasichana, zote za Tarafa ya Nguruka na Kalenge iliyopo Tarafa ya Ilagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uanzishaji wa Shule za Kidato cha Tano na Sita ni la kisera, lakini Serikali inaendelea kuboresha na kupanua miundombinu katika Shule za Sekondari Buhingu katika Tarafa ya Buhingu na Sunuka katika Tarafa ya Ilagala ambazo zinatarajiwa kupandishwa hadhi na kuanza kutoa elimu ya Kidato cha Tano na Sita ifikapo Julai, 2020.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Shule za Sekondari za Lugufu Wavulana na Wasichana ni miongoni mwa Shule za Sekondari zilizoanzishwa kwenye maeneo yaliyokuwa Makambi ya Wakimbizi Mkoani Kigoma. Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri imekuwa ikitumia mapato ya ndani ya Halmashauri na kukamilisha vyumba vitatu vya maabara za Sayansi.

Vile vile Serikali Kuu kupitia progrmu ya EP4R imepeleka fedha za ukarabati wa matundu manane ya vyoo na shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili mapya kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. HASNA S. K. MWILIMA) aliuliza:-

Wilaya ya Uvinza imeanzishwa tangu mwaka 2002 lakini hadi sasa Jeshi la Polisi katika Wilaya hii halina nyumba za kuishi, Ofisi pamoja na vitendea kazi:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha vitendea kazi Jeshi la Polisi katika Wilaya hiyo kama vile magari, Ofisi pamoja na makazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Mwilima, Mbunge Wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi lina jumla ya Wilaya 168 za kipolisi ikiwa ni pamoja na Wilaya za Kiserikali. Kati ya hizo Wilaya 127 zina majengo kwa ajili ya Ofisi na Vituo vya Polisi vya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuliboresha Jeshi la Polisi kwa awamu. Mathalani, Serikali imejenga na inaendelea kujenga nyumba za makazi kwa askari nchi nzima katika ngazi ya Mkoa na ni mpango wa Serikali kujenga Ofisi na nyumba za kuishi askari katika ngazi za wilaya zote nchini. Aidha, Wilaya ya Uvinza ina magari mawili ambayo ni T/Land cruiser PT 1415 linalotumiwa na OCD na Leyland Ashock kwa matumizi mbalimbali ya Kipolisi.