Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sebastian Simon Kapufi (42 total)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Katavi kijiografia upo pembezoni lakini inapotokea shida ya barabara, shida ya huduma za afya inaufanya mkoa kuendelea kuwa pembezoni. Ninavyofahamu mimi, huduma ya afya kwa maana ya hospitali ni hitaji muhimu. Je, Serikali imejipangaje kulifanya jambo hili kwa haraka ili kunusuru nguvu kazi iliyoko kule kwa kuiepusha na maradhi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, fungu linalotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa Hospitali ya Wilaya ni dogo, wananchi wote wa Wilaya ile ya Mpanda ambayo kwa sasa hivi ni mkoa, wanategemea Hospitali hiyo ya Wilaya. Je, Serikali inaisadiaje hospitali ile kwa maana ya kuiongezea bajeti?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza Serikali imejipanga vipi kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama nilivyosema awali, Serikali imetenga shilingi bilioni moja katika bajeti ya mwaka huu, tunachosubiri sasa hivi ni kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili mradi kazi hiyo ianze maana huo ndiyo mwanzo. Kazi yoyote haiwezi kufanyika lazima mshauri afanye kazi yake na kibali hicho kitakapotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali nadhani kazi hii itaanza rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato wa bajeti unaondelea sasa katika Ofisi ya Mkoa, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 matarajio ni kwamba hospitali hii itatengewa shilingi bilioni 1.8 ili kuhakikisha watu wa Mkoa huu wa Katavi wanapata huduma ya afya. Umesema miundombinu ya barabara ina changamoto kubwa sana, endapo Hospitali ya Mkoa itakamilika tutawasaidia akina mama. Jambo hili ni la kipaumbele sana katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la hospitali yetu ya Mpanda ambayo kutokana na jiografia ilivyo inahudumia wananchi wengi wanaotoka maeneo mbalimbali. Pia inaonekana wazi hata dawa zikipelekwa pale hazitoshelezi na vifaa tiba vina changamoto kubwa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri ameweza kupita katika maeneo mbalimbali, ni imani yangu tunakwenda kushughulikia jambo hili. Isipokuwa nawaagiza wataalamu wetu, mara nyingi wamekuwa na kigugumizi kikubwa sana cha kuandaa data za wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali zao. Niwaagize zile data sheet za kusema hospitali inatibu wagonjwa wangapi zikusanywe vizuri. Mwisho wa siku ndiyo hizo data sheet ndiyo itakuwa taarifa elekezi ya jinsi gani Hospitali hii ya Mpanda iweze kusaidiwa ili mradi wananchi wapate huduma bora katika maeneo yao.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa niaba ya Waziri wa Nchi (TAMISEMI), napenda kujibu sehemu ya pili ya swali, je, Serikali inaisaidiaje Hospitali ya Wilaya ya Katavi katika kuongeza bajeti?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Naibu Waziri, afya ndiyo kipaumbele cha juu katika Serikali ya Awamu ya Tano, kwa hiyo, tutaongeza bajeti katika fedha zinazotoka moja kwa moja Serikalini. Hata hivyo, nimesimama kusisitiza jambo moja, ni lazima tuhakikishe mapato yanayopatikana kutokana na uchangiaji wa wananchi katika kupata huduma za afya yanatumika pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya. Tuwahimize Wanakatavi na wananchi wote wajiunge bima ya afya kwa sababu kadri wananchi wengi wanavyojiunga katika Mfuko wa Bima ya Afya au CHF, ndivyo mnavyopata fedha za kuweza kutatua changamoto za bajeti. Tumetoa mwongozo asilimia 60 ya fedha zinazopatikana kutokana na uchangiaji zirudishwe kwa ajili ya kuboresha huduma kama vile kununua dawa, vifaa na vifaa tiba. Kwa hiyo, bajeti haitatosha kwa sababu kasungura siku zote kitakuwa kadogo. Tutumie fedha za makusanyo za Bima ya Afya na CHF ili kuweza kutatua tatizo la bajeti ndogo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanywa na Manispaa ya Mpanda ni dhamira chanya ya kuthubutu, lakini ujenzi wa chuo nafahamu ni kazi kubwa. Je, ni kwa nini Serikali Kuu isiungane na Manispaa hii, kwa maana ya kulichukua zoezi zima la ujenzi huo wa Chuo Kikuu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi nikizingatia kwamba tunapozungumzia habari ya kuifungua mikoa ya pembezoni katika maeneo ya barabara na kilimo, huwezi ukaacha kuifungua mikoa hiyo kwa maana ya eneo hili la elimu. Elimu ndiyo chanzo cha mambo mengine yote. Je, Serikali haioni kwamba wakati umefika wa zoezi hili ikalichukua? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunaposema Manispaa ikaliweke wazi suala hili…
MWENYEKITI: Kwa kifupi, tafadhali!
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Zoezi hili lilichukuliwa na Bodi. Baadhi ya watendaji waliokuwa kwenye Bodi, Serikali hii hii imewahamishia maeneo mengine kwenda kufanya utumishi. Je, ni kwa nini Serikali isije na hatua za makusudi kuhakikisha nyaraka muhimu zimerudishwa katika Manispaa ya Mpanda ili Manispaa ya Mpanda iweze kuendelea na mchakato mwingine ikiwa ni pamoja na fidia kwa watu waliotenga eneo lao?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Ufundi, ningependa kumjibu Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Kwanza kuhusu sababu ni kwa nini Serikali isichukue ujenzi huu, ningependa kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba swali lake la msingi, lilikuwa ni lini ujenzi utaanza. Ujenzi huu ulikuwa ni mchakato ambao Manispaa, ilikuwa imeomba ijenge na Wizara yangu ilikuwa kazi yake ni kutoa support ambapo TCU ilipitia kulingana na mchakato. Kwa hiyo, naona kama anachokisema ni swali jipya ambalo haliendani na swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwamba kuna baadhi ya wajumbe walihamishwa na wameondoka na nyaraka, huo sio utaratibu. Taratibu ni kwamba mtumishi anapohama nyaraka za Serikali zinatakiwa zibaki mahali husika. Kwa hiyo, bado naiomba Halmashauri kama kuna watumishi wanapopata uhamisho wanahama na nyaraka za Serikali ni kinyume cha utaratibu na Halmashauri inatakiwa kuchukua hatua husika.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mazingira magumu ya ukosefu wa vitendea kazi kama magari, mafuta na makazi ya askari yanayowakabili askari wa Masasi yanaakisi hali halisi ilivyo Wilayani Mpanda. Je, ni lini Serikali itafikiria kujenga makazi ya Askari Polisi Wilayani Mpanda? Katika hili nafarijika Waziri alikuwa huko na alijionea hali ilivyo ya askari wetu Wilayani Mpanda.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi anachozungumza Mheshimiwa Kapufi hasa ukitilia maanani Mkoa wa Katavi kama ilivyo mikoa mingine mipya, ina changamoto siyo tu za makazi hata ofisi za vyombo vya usalama. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba katika mgao ambao tumezungumza maeneo ambayo ni mapya kimkoa na kiwilaya yatapewa kipaumbele ikiwemo Jimbo la Mpanda Mjini.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Upungufu mkubwa wa Ikama na zoezi la uhakiki wa vyeti limepelekea shida kubwa ya watumishi katika maeneo ya afya, elimu, Watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata katika Manispaa yetu ya Katavi, kiasi cha kwamba mtumishi mmoja anafanya kazi zaidi ya moja.
Ni lini Serikali itaajiri katika maeneo hayo niliyoyazungumza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tunakiri ni kweli kuna upungufumkubwa wa watumishi katika baadhi ya maeneo. Niendelee tu kusisitiza kwamba lengo letu kubwa kama Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunaenda kwa kuzingatia maeneo yenye vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tutahakikisha kwamba tunaimarisha maeneo yenye upungufu mkubwa. Nimweleze tu kwamba katika kada alizozitaja zitakuwa ni miongoni mwa kada ambazo pia tutazipa ajira katika mwaka ujao wa fedha. Vilevile labda nimtoe tu hofu kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi; katika mwaka ujao wa fedha tutatoa ajira 52,436 na labda tu niseme kwa mchanganuo ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Elimu tutatoa ajira 16,516 kwa upande wa Sekta ya Afya 14,102, Kilimo 1,487, Mifugo 1,171, Uvuvi 320, Polisi 2,566, Magereza nafasi 750, Jeshi la Zimamoto 1,177, Uhamiaji nafasi 1,500, hospitali za mashirika ya kidini na hiari kwa kuwa nazo tunatoa ruzuku, nafasi 174 pamoja na nafasi nyinginezo 12,673 ambazo zitahusu Sekta zote na jumla kuu ni 52,436.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe Mheshimiwa Kapufi hofu, ikama zote na mapendekezo kutoka kwa waajiri tumezipokea na tutaangalia katika kuimarisha maeneo hayo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niishukuru Serikali kule Katavi tuliweza kupatiwa kituo hiki cha MSD kwa msaada wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini mita chache kutoka kilipojengwa kituo hicho kipo Chuo cha Matabibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ni lini Serikali itatusaidia kuhakikisha chuo hicho kimeanza kazi kwa sababu ukarabati ushafanyika kwa asilimia 99?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini, sina hakika sana lini tunaweza tukawa tumekamilisha lakini chuo hiki ni katika vyuo vinne ambavyo tumevipa kipaumbele cha kufanyiwa ukarabati na kufanyiwa maboresho ili kuweza kutusaidia katika mpango wetu wa kuendeleza na kuzalisha rasilimali watu kwenye sekta ya afya. Kwa msingi huo, ndiyo maana yeye mwenyewe anasema kimekamilika kwa asilimia 99; kwa hivyo kwa sasa hivi sina taarifa sahihi kwamba lini tutakifungua rasmi lakini naomba nifuatilie na baada ya hapo naweza nikamshirikisha kwenye uvumbuzi wa majibu nitakayokuwa nimeyapata kutoka kwa watendaji wa Wizara yetu.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kibali cha Halmashauri kinatozwa shilingi 16,000, kiwango ambacho ni nafuu, je, zimamoto kutoza 150,000 haioni kwamba kiwango hicho ni kikubwa na hivyo inapelekea wananchi wengi kujenga bila kuwa na kibali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mchanganuo wa tozo kwa mjenzi wa nyumba ya kawaida anatozwa hiyo hiyo shilingi 150,000 sawa na mjenzi wa ghorofa, hii imekaaje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza ametaka kujua tozo ya shilingi 150,000 kwamba ni kubwa na hivyo inawafanya wananchi washindwe kupata kibali hiki na hivyo kujenga majengo holela. Tozo hizi ni kwa mujibu wa Kanuni na Sheria ambazo tumejiwekea, ukiacha ile Halmashauri ambayo ni shilingi 16,000 anayosema yeye, lakini kwa mujibu wa taratibu ambazo tumejiwekea kwa maana ya Sheria yetu hasa katika Kanuni ile ya [The Fire and Rescue Force, (Fire Precautions in Buildings) Regulations], 2015 Na. 248 imezungumza kiwango ambacho kinapaswa kutozwa ukianzia katika Majiji, Halmashauri, Wilaya lakini vile vile na katika vijiji. Kwa hiyo kiasi kilichowekwa hapa cha shilingi 150,000 ni kwa mujibu wa Sheria yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ametaka kujua kuhusu utofauti wa utozwaji wa tozo hizi. Tozo hizi zinatofautiana kutokana na kiwango cha ukubwa wa jengo au vile vile mita za ujazo wa jengo. Kwa hiyo, haiwezi ikawa kuna mfanano kwa namna ambavyo tozo hizi zimewekwa. Kikubwa kinachoangaliwa hapa ni mita za ujazo. Kwa hiyo, mita za ujazo zinavyozidi kuwa kubwa zaidi ndiyo tozo zenyewe zinazidi kuongezeka.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kati ya mambo yanayosababisha Uwanja wa Ndege wa Mpanda usifanye kazi ni kutokuwepo kwa huduma ya zimamoto. Ni lini Serikali itatusaidia kuhakikisha huduma ya zimamoto inakuwepo kwenye Uwanja huo wa Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza nampongeza sana wewe na Wabunge wenzako wote wa Mpanda kwa jinsi mnavyoshughulikia masuala ya huduma za usafiri wa anga kwa ajili ya mkoa wenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, sasa hivi gari linalotoa huduma ya zimamoto kwenye uwanja ule limepata hitilafu na Serikali kupitia TAA tunaendelea kushughulikia kuhakikisha kwamba, uwanja ule unapata hiyo huduma ya zimamoto na hivi karibuni tumeendelea kuwasiliana na watu wa kule Mpanda ili walete makadirio yatakayowezesha hiyo huduma irudi katika hali yake ya kawaida.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali iliahidi kutenga maeneo ya Ibindi, Dirifu, Society na Kapanda kwa wachimbaji wadogo wa huko Mpanda, je, ni lini wachimbaji hawa watapatiwa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Kapufi kwa ufuatiliaji wake kwenye jambo hili. Kwa muda mfupi ambao nimeingia ofisini amekuwa mara nyingi akiniambia jambo hili juu ya wachimbaji wake wadogo wadogo. Naomba nitumie fursa hii kuwaambia Watanzania wote wakiwepo na wananchi wa Kibindi kwamba wale wote ambao wamejiunga kwenye vikundi wakaomba maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchimbaji madini Wizara ya Madini iko tayari kuwasaidia mara tu, Tume ya Madini itakapoanza kazi baada ya kuwa imekwishakuundwa.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kwa sasa hivi inafanya kazi kama Hospitali ya Mkoa, imeelemewa kwa kiasi kikubwa na wangonjwa wanaotoka katika Halmashauri mbalimbali. Wakati tukisubiri mipango ya Serikali ya kutujengea Hospitali ya Mkoa, ni lini Serikali itatusaidia kuongeza waganga pamoja na wauguzi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna upungufu wa wauguzi pamoja na madakatari. Nizitake Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda pamoja na Halmashauri zingine waige mfano mzuri ambao umefanywa na Halmashauri ya Handeni kwa kutumia own source ili kuweza kuwaajiri wale watumishi ambao ni muhimu sana kwa kipindi hiki wakati wanasubiri wale ambao wataajiriwa na Serikali.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo kimsingi yana afya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa mpango huo mzuri wa Serikali ili wachimbaji wadogo waweze kufikia hatua ya kupata mpango huo mzuri, ni lazima wawe na maeneo. Naibu Waziri anasema nini kwa maana ya kutenga maeneo kwa eneo hilo la Mpanda? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili, nafahamu Wizara kwa ujumla wake imekuwa ikisaidia wachimbaji wadogo nchini. Je, ni utaratibu upi unaotumika kwa maana ya suala zima la utoaji ruzuku kwa wachimbaji hawa wadogo? Naliuliza hilo ili iwe faida kwa wachimbaji wote wadogo nchini? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nipate ridhaa yako nimshukuru sana Mheshimiwa Kapufi. Kwanza nampongeza kuwa mchimbaji mdogo kati ya wachimbaji wadogo maarufu hapa nchini. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Kapufi kama mdau mzuri na ni mchimbaji mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Kapufi kwa kuwawakilisha vyema wananchi wa Mpanda. Mheshimiwa Kapufi nikuhakikishie kwamba wananchi wako ambao ni wachimbaji wadogo, kama ambavyo wewe unachimba nao watafikia kiwango chako cha uchimbaji kama unavyoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nijielekeze kwenye maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapufi. Ni lini Serikali itawatengea maeneo wachimbaji wadogo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) anafanya tathmini kwa mambo matatu; tathmini ya Kijiokemia, tathmini ya Kijiolojia na tathmini ya Kijiofizikia na mwezi wa saba tunaanza kuwatengea maeneo hayo. Zoezi la kuwatengea wananchi maeneo litakuwa ni endelevu; kuanzia mwezi wa saba na kuendelea tutafanya kazi ya kuwatengea maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali imetenga hekta 12,000 kwa ajili ya kuwatenga maeneo, kadhalika, imetenga shilingi milioni 640 kwa ajili ya Wakala wa Jiolojia kutathmini maeneo ambayo yatatengwa. Maeneo ambayo tutayatenga ni mengi sana ikiwa ni pamoja na Lindi, Geita, Sambaru – Singida, pamoja na Londoni. Maeneo mengine tutakayotenga kule Mpanda ni pamoja na eneo la Dirifu, Katuma, Society pamoja na eneo la Katasunga. Maeneo yote ya Mpanda Mheshimiwa Kapufi tutaendelea kuyatenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili kuhusu utaratibu wa ruzuku, ni kweli kabisa mwaka 2015/2016, Serikali ilitenga shilingi bilioni 7.24 na mwaka huu kwa ridhaa ya Waheshimiwa Wabunge tumetenga shilingi bilioni 6.68, hii ni kwa ajili ya kuwagawia wananchi kama ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kuhusu hili. Utaratibu tunaotumia kwa sasa, kwanza kabisa leseni lazima ziwe za Watanzania peke yake kwa asilimia mia moja. Hilo la kwanza. Pili, leseni hizo lazima ziwe hai na zinafanyiwa kazi; na tatu, tunawahamasisha sana wananchi wajiunge kwenye vikundi ili ruzuku hii iwanufaishe Watanzania wengi. La nne, tumeongeza sasa badala ya kutenga dola 50,000 kwa msimu huu, tutatenga dola 100,000 kwa kila atakayekidhi vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningesema mengi sana kwenye eneo hili, lakini niwahamasishe Watanzania; Mheshimiwa Kapufi na Waheshimiwa Wabunge wengine ili waweze kunufaika na ruzuku hii.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Uchakavu katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu ni sawa na hali ilivyo katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda. Jengo ni la kizamani, dogo na halikidhi mahitaji ya sasa ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla. Ni lini Serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mpanda?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu la mjumbe, niwe na hakika, Mbunge ni Kapufi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Mpanda imepangiwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Huko nyuma Serikali ilikuwa ikitoa mafunzo kwa Madiwani ambapo mafunzo hayo yaliwajengea uwezo mkubwa ikiwa ni pamoja na kufahamu mipaka yao. Je, ni lini Serikali itarejesha mafunzo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kwa kipindi cha nyuma kulikuwa na mafunzo ya Madiwani ambayo yalikuwa yakitolewa ili kuwajengea uwezo waweze kufanya kazi yao vizuri kwa sababu wao ndio wanafanya maamuzi katika Mabaraza yetu ya Madiwani katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hapa katikati mafunzo kidogo yalisimama. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huu wa mafunzo umeanza katika maeneo mbalimbali na mafunzo haya yataweza kuwafikia Madiwani, lengo kubwa ni kujenga uwezo wao kwa kadri itakavyoonekana kwamba itafaa.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Kigoma kunaakisi hali halisi ilivyo katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambayo inafanya kazi kama hospitali ya mkoa. Je, ni lini Serikali itatusaidia Madaktari na wataalam wengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze amekuwa anafuatilia sana masuala kuhusiana na afya katika eneo lake la Mpanda. Pia nimhakikishie tu kwamba kadri Serikali itakapokuwa tunapata watumishi na tunatarajia mwezi Julai mwaka huu tutapata watumishi wengine wa ziada, Hospitali ya Mpanda ambayo na mimi nimeshaitembelea na natambua changamoto zake itakuwa ni moja ya hospitali zitakazopata watumishi. Sambasamba na hilo, Serikali imejielekeza sasa katika ujenzi wa hospitali mpya kubwa ya rufaa katika Mkoa wake wa Katavi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuathiri wajibu wa Serikali wa kuratibu, ni kwa nini kusiwe na soko huria la mbolea kwa sababu haipatikani kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati watu wanaongezeka, ardhi hususan inayofaa kwa kilimo haiongezeki. Nini mkakati wa Serikali wa kuja na mkakati mpya wa kuratibu kilimo chenye tija katika eneo dogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameuliza swali ambalo pia linaendana na Wabunge wote hususan wale wanaotoka katika majimbo ya mijini, naye ni Mbunge wa mjini, hususan kuhusu kwamba watu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilieleze Bunge lako tukufu kwamba sisi kama Serikali tumejipanga kuongeza uzalishaji na teknolojia ya hali ya juu. Vilevile lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wakulima hawa siyo tu kwamba wanalima kilimo cha kujikimu lakini vilevile kiwe ni kilimo cha kibiashara. Naasa kila Halmashauri zote nchini ziweze kuwa na zile green houses. Kilimo kile kinalimwa katika sehemu ndogo lakini uzalishaji wake unakuwa ni mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kwamba soko huria Serikali kazi yetu ni kuratibu, ku-control na ku-regualte, kwa maana hiyo, kwenye mbolea soko huria lipo, isipokuwa katika zile mbolea za DAP pamoja na Urea kwa maana ya kupandia na kukuzia, hiyo sisi kama Serikali kama tulivyosema ni kwamba Jumapili tutatoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kuwa na uelewa mpana na wa pamoja kuhusu nini maana ya bei elekezi. Vilevile mbolea kuanzia sasa ziweze kufika kwa wakati na ziweze kuenea kwenye maeneo yote ya vijiji ili iwe kama soda na sukari. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Umwagiliaji wa Mwamkulu ni takribani miaka nane sasa haujakamilika na wananchi wa eneo hilo walivunjiwa vizibo. Napenda kuiuliza Serikali, ni lini itapeleka fedha ili kuhakikisha mradi huo umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri. Nimhakikishie kwamba hili jambo ni la haraka. Kwa hiyo, sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga katika kuhakikisha tunalikamilisha hili jambo ili wananchi wake waweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge pia baada ya saa saba mchana tunaweza tukakutana tujadiliane kwa pamoja ili tuone ni namna gani tunaweza tukalifanya hili jambo ili liweze kukamilka kwa wakati.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mpanda Town Clinic ni kituo ambacho kinaisaidia sana Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, lakini kwa bahati mbaya kituo hiki ilikuwa kikarabatiwe kwa kupitia fedha za ruzuku kwa maana ya miradi viporo. Naomba kuiuliza Serikali, ni lini watatusaidia fedha hiyo ili tuweze kukisaidia kituo hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nilipata bahati ya kutembelea Mkoa wa Katavi na Manispaa ya Mpanda nimeitembelea. Pale jirani na stand, kuna ujenzi wa Kituo kipya cha Afya, lengo ni kuhakikisha kwamba msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda unapungua.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kapufi, naye ni shuhuda, tulikuwa wote pamoja; ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma ya afya inasogezwa kwa wananchi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mpango wa maendeleo ya vitu, kwa mgano, ujenzi wa shule, visima na kadhalika ni watoto pacha na mpango wa uzazi. Serikali inasema nini katika kuhakikisha haiishii kutenga fedha bali fedha zionekane zikipelekwa eneo hilo la uzazi wa mpango?
Swali la pili, mimba za utotoni ni janga la Taifa, Mkoa wangu wa Katavi tunaongoza kwa maana ya asilimia 45. Serikali inasema nini katika kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Katavi ili kuwanusuru wananchi wale na janga hili?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Kapufi kwamba upo uhusiano wa moja kwa moja wa maendeleo na ongezeko la idadi ya watu na Serikali imeliona suala hili na ndiyo maana pia katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, suala la uzazi wa mpango na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amekuwa kisisitiza huduma za uzazi wa mpango na ndiyo maana ukiangalia tumetoka asilimia 27 mwaka 2012 sasa hivi ni asilimia 32. Kwa hiyo fedha zinatoka za Serikali na tumeamua kabisa kutumia fedha zetu za ndani badala ya kutumia fedha za wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni mimba za utotoni, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba ni changamoto. Asilimia 27 ya watoto wa kike wamepata ujauzito kabla hawajatimiza umri wa miaka 18, kwa hiyo, katika mpango wetu wa kuzuia mimba za utotoni especially katika Mikoa ya Katavi tumeamua kutumia njia za kuwaelimisha wasichana wajizuie kuingia katika vitendo vya ngono mpaka pale watakapofikisha umri wa miaka 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa kweli hali siyo nzuri, watoto wetu wa kike wanaanza ngono, asilimia 14 ya watoto wakike wanaanza ngono kabla hawajafikisha umri wa miaka 15 na watoto wa kiume ni asilimia tisa. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge mtusaidie katika kuhamasisha na kuelimisha wasichana hasa kujizuia kufanya mapenzi kabla hawajatimiza umri wa utu uzima. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Napenda kuishukuru Wizara kwa kutuchimbia visima 14, kilichobaki ni ujenzi na uwekaji wa pump.

Je, ni lini fedha za kumalizia ufungaji wa pump zitaletwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Kapufi kwa jitihada zake kubwa za kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. Alishakuja Wizarani siyo mara moja wala mara mbili katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na uwepo wa chanzo. Tumeshachimba visima vya kutosha. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kapufi, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika utoaji wa fedha ili wananchi wale waweze kutengenezewa miundombinu na waweze kupata majisafi na salama. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nikirejea hapo katika Shule ya Wasichana ya Mpanda kimechimbwa kisima kirefu, tatizo lililobaki ni ufungaji wa pump na ukizingatia ni shule ambayo ina watoto wa kike peke yake.

Ni lini Serikali itakamilisha suala la ufungaji wa pump kwenye shule hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tunapokarabati hizi shule kwanza tunaangalia mfumo wa majengo, mabweni, bwalo, madarsa, Ofisi, majengo ya utawala, mfumo pia wa maji na mfumo wa umeme. Kwa hiyo, kama alivyozungumza kwamba kuna kisima ambacho kimechimbwa katika eneo hilo, wakati wa ukarabati litaangaliwa. Tutatenga fedha kwa ajili ya kupata maji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuwa na wanafunzi wengi katika shule hii kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba ni zaidi ya wanafunzi 800, watoto wa kike, halafu kusiwe na huduma ya maji. Ahsante.
MHE. SEBASTIANA S. KAFUPI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru pamoja na majibu mazuri ya Serikali Mkoa wa Katavi ni kati ya mkoa ambayo haijafunguka kwa maana ya kuunganishwa na mikoa mingine. Kitendo cha kupewa kilomita hizo chache kinafanya mkoa huu uendelee kujifunga. Serikali inasema nini katika hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo kama haitoshi kigezo cha idadi ya magari yanayopita katika barabara ni tunda la uzuri wa barabara. Serikali inasema nini kwenda kuboresha barabara ili baadaye idadi ya magari iongezeke?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nami ni shahidi kwa sababu nimefika Mkoa wa Katavi mara kadha na Mheshimiwa Kapufi anafahamu, na ndio maana Serikali hata katika Manispaa yake pale tunawekeza fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wa barabara za lami. Lakini hata hivyo ni kweli vigezo hivi vimewekwa kwa mujibu wa utaratibu kama pale itakapobidi tutaangalia nini kifanyike kuhakikisha kwamba Mkoa wa Katavi unapatiwa fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo naomba nikuhakikishie kwamba jukumu la wizara yetu yale maeneo yenye changamoto kubwa tutahakikisha kwamba kama maoni yako ulivyotoa hayo tutahakikisha jinsi gani tunaipa nguvu. Na ndio maana hata katika addition finance ya sasa hivi ambayo bado hatua disclose tumeweka kipaumbe kwa ajili ya kuongeza katavi kupata fedha nyingi za ziada nini kifanyike katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo katika suala nzima la traffic ya magari kama ulivyosema ni jukumu la Serikali sisi tunahakikisha kwamba tunaimarisha miundombinu ya barabara hizo lengo kubwa ni kwamba barabara zikifunguka magari mengi yatapita. Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kwa hiyo Mheshimiwa Kapufi usihofu Serikali ipo kwa ajili yakuwahudumia wananchi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Matatizo yaliyojitokeza huko Kigoma, ndiyo hali ilivyo katika eneo la Kampuni Mpanda Mjini.

Je, ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro wa wananchi na Jeshi katika eneo la Kampuni?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mgogoro uliopo na nikipongeze Chama Cha Mapinduzi kwa sababu mlezi wa Chama katika Mkoa ameliwasilisha suala hili mezani kwangu na mimi nimeshachukua hatua. Nimetoa maelekezo ili uchambuzi wa kina juu ya mgogoro huu niupate.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Kapufu asiwe na wasiwasi na tutakwenda kwa kasi kubwa kuhakikisha kwamba wananchi katika Jimbo hili la Mpanda wanakaa vizuri, waendelee na shughuli zao na Jeshi nalo liendelee na shughuli zake. Kwa hiyo, taratibu zinaenda vizuri Mheshimiwa Kapufu naomba avute Subira tu kidogo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itatusaidia kupeleka umeme katika Kata ya Kasokola na Mwamkulu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian, Mbunge wa Mpanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote vilivyokuwa havijapelekewa umeme katika awamu zilizotangulia zitapelekewa umeme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili na vijiji kwa kuwa viko kwenye kata, kata hizo pia zitakuwa ni sehemu ya kupata umeme huo ambao Serikali imejipanga vyema kabisa kuhakikisha kwamba umeme unawafikia wananchi katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Aprili.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. Awali ya yote naishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Maswali yangu madogo ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kata ya Ikola wamefanya kazi nzuri ya ujenzi wa Hospitali Teule: Nini kauli ya Serikali katika kuwaunga mkono wananchi hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Awamu ya tatu na ya nne kwa maana ya upelekaji vifaatiba katika vituo vya afya, tunacho Kituo cha Afya cha Ilembo, kwa bahati mbaya hakikubahatika kupata fedha hizo: Nini kauli ya Serikali katika kupeleka vifaatiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana kwa kupongeza juhudi za Serikali za kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivi vya afya, lakini hizi kazi zote zinazofanywa ni dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Sita na Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kule walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata hii ya Ikona ambayo wananchi wamechangia nguvu zao kujenga kituo cha afya, kwanza niwapongeze sana kwa kuchangia nguvu zao, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge pia kwa kuhamasisha wananchi hawa, lakini nimhakikishie kwamba Serikali inaendelea na mipango yake ya kuchangia nguvu za wananchi kwa kupeleka fedha ili kukamilisha vituo vya afya ambavyo tayari wananchi wameanza na ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hii itawekwa kwenye mipango na kadri ambavyo tutapata fedha tutakwenda kuhakikisha kwamba kituo hiki pia kinasaidiwa ili kikamilike na kuanza kutoa huduma bora za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Ilembo nayo kuhusiana na vifaatiba, tumeweka mkakati na katika mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 100 zinazotokana na tozo kwa ajili ya vifaatiba katika vituo vyetu. Kwa hiyo, tutaenda kuhakikisha vituo kama hivi pia vinapata fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutampa kipaumbele katika kituo hicho. Ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mbele ya Rais kwa maana ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Ummy alituhakikishia kwamba itakapofika mwezi Julai, 2020 hospitali hiyo itakuwa imekamilika. Serikali inasema nini kwa Wanakatavi kutokana na ahadi hizi zisizotekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mkoa wa Katavi umbali kutoka Katavi ikitokezea amepatikana mgonjwa, anahitaji tiba na madaktari bingwa ama umpeleke Mbeya, Mwanza au Dar es Salaam. Umbali huu ukiwa salama na katika mazingira ya amani unaweza ukaenda bila matatizo, lakini ukiwa katika hali ya mahtuti, umbali unakuwa ni mrefu zaidi. Serikali inasemaje katika namna ya kuwanusuru Wanakatavi kuja na suala zima la dharura nikizingatia yapo maeneo mengine hospitali zimejengwa kwa fedha ambayo ni zaidi ya hiyo bilioni tisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mkubwa sana wa hali ya afya ya Mkoa wake na Wabunge wa Mkoa huo kwa sababu wamekuwa wakija Wizarani na nakumbuka alikuja pamoja na Wabunge wenzake. Waziri wa Afya alinituma nikaja Mkoani kwao, ni kweli kama Mbunge anavyosema kwa rufaa tu pale kwao wanatumia shilingi milioni 250 kwa mwaka kwa ajili ya ambulance tu kupeleka watu rufaa. Kwa hiyo, anachosema ni kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anasema hospitali hiyo iliahidiwa kumalizika mwaka jana na bahati mbaya haijafanyika kama ahadi ilivyokuwepo. Kama unakumbuka tulikwenda Wizarani na tayari Waziri wa Afya ameunda timu na imechunguza sababu ambazo zimesababisha hizi hospitali zichelewe na sababu hiyo utaletewa Mheshimiwa Mbunge. Vilevile tumeshatengeneza strategy ambayo kwa uhakika kabisa Januari, 2022 hospitali hiyo inakwenda kumalizika ili kuondoa wananchi katika adha hiyo ambayo tayari ulishakwenda kunionesha Mkoani kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili umezungumzia umbali, tulipokwenda mkoani kwako ulielezea suala la ramani ambayo mlitaka hasa kwenda kwenye hospitali za kanda. Ile ramani ambayo ulikuwa unaizungumzia Mheshimiwa Mbunge, tayari Waziri ameshakaa na timu yake na hata yale mapendekezo yenu ya kupunguza rufaa hasa kuelekea kwa hospitali za kanda inatafutiwa suluhisho na itafanyiwa kazi vizuri kama ambavyo mlitegemea ifanyike Wabunge wa Mkoa wenu. Ahsante. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninalo swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzoefu unaonyesha maeneo mengine duniani ikiwemo China kwa kutumia vyanzo vya kudumu imeweza kuiunganisha nchi yake kutoka kaskazini kwenda kusini kwa vyanzo vya maji. Tanzania tuna Ziwa Nyasa, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika; ni lini Serikali itatumia vyanzo hivi muhimu kuiunganisha nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maziwa makuu ni moja ya mikakati ya Serikali kuweza kutumika na kuwa suluhisho la tatizo la maji katika nchi yetu. Hivyo, napenda kukuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Ziwa Tanganyika katika eneo lako litatumika kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali yanayotia moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sura ilivyo katika eneo la mradi kuna hali ya kusuasua, nilichokuwa naomba nafahamu uhakiki wa uwezo wa mtengenezaji kwa maana ya due- diligence jambo hili bado halijafanyika sambamba na utiaji saini mikabata, nilikuwa naiomba Serikali inihakikishie ni lini suala hili litafanyika ili kuharakisha mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kapufi wa Mpanda kama ifuatavyo, kama tulivyosema katika swali la msingi ni kwamba tayari ujenzi umeanza kwenye maeneo hayo na vituo vya kupoozea umeme tayari vimetengenezwa na majengo yake yamekamilika kwa asilimia 90, ni kweli kwamba uhakiki wa uwezo wa Mkandarasi wa kututengenezea vile vifaa vya ndani ya kile chumba cha kupoozea umeme vikiwemo generator, transforma na vitu kama hivyo broker na breakers nyingine haujafanyika vizuri kwasababu ya tatizo kubwa ambalo liliwapata wenzetu ambao wanaweze kututengenezea vifaa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni vigumu kwetu sisi kutuma wataalam wetu kwenda kwenye hizo nchi ambazo zinao watengenezaji wa vifaa hivi vikubwa kwenda kuhakiki uwezo wa watengenezaji hao. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ufuatiliaji wake sisi kwetu ni faraja na tunaelekea kukamilisha kwa sababu tayari sasa nchi ambazo zinatengeneza vifaa hivi zimeanza kuruhusu watu mbalimbali kwenda kufanya shughuli mbalimbali kwenye nchi zao baada ya janga la Korona kupungua kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiandaa kutuma wataalam wetu kwenda kuhakiki kama wale tuliowapa kazi wana uwezo wa kutengeneza hizo mashine tunazoziomba na baada ya hapo mikataba itasainiwa kama tulivyosema kwenye jibu la Msingi kwamba 2023 mradi huu utakuwa umekamilika na grid ya Taifa itafika Mpanda.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru pia, majibu mazuri yenye kutia matumaini kutoka Serikalini. Hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; nafahamu tulikuwa na behewa la daraja la pili, lakini kwa bahati mbaya behewa hili lilipata ajali ya moto. Ni lini Serikali itaturejeshea huduma hiyo ya behewa la daraja za pili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kituo cha Mpanda kwa bahati mbaya sana wakati wananchi wakisubiri huduma ya usafiri, jengo lao la kusubiria huduma hiyo halipo. Ni lini Serikali pia, itatusaidia huduma hii muhimu ya jengo la kusubiria abiria? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapufi, kwa faida ya wananchi wa Mpanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama tutarejesha daraja la pili katika eneo hili. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge maombi haya yamepokelewa. Tutazingatia maombi haya hasa katika mabehewa mapya ambayo yanaendelea kununuliwa angalau huduma hiyo iweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, tumepokea pia hoja ya pili ya jengo la kusubiri abiria. Hili ni eneo muhimu kwa sababu kama kunakuwa na jua abiria wanahitaji kivuli, lakini pia kama ni wakati wa mvua inapaswa kujikinga. Namwelekeza Mtendaji Mkuu wa TRC atembelee eneo hili ufanywe mpango wa haraka kujenga jengo la kusubiria abiria ili wananchi waweze kupata huduma muhimu. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza.

Mji wa Mpanda ni kati ya miji 28 ambayo inatakiwa kupewa mradi wa maji; ni lini mradi huu utaletwa Mji wa Mpanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi kutoka Mpanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya miji 28 tutarajie itaanza ndani ya mwezi huu wa pili au wa tatu kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ilikuwa na gari zuri la zimamoto, gari ambalo lilikuwa ni la kisasa. Kwa bahati mbaya lilipata ajali mwaka 2015, toka Serikali imelichukua kwa ajili ya matengezo, gari hilo halijaweza kurejeshwa Mpanda. Swali langu, ni lini Serikali itaturejeshea gari hilo zuri na la kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna interest na Tanga kutokana na miradi mingi mliyonayo ya kiuchumi ikiwemo bandari na bomba la mafuta linalopita pale. Tutafuatilia baada ya Bunge hili kuona kwamba, matengenezo ya gari hilo yanakamilika lirejeshwe Tanga kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa muda huu wa maswali madogo mawili ya nyongeza. Ninaishukuru sana Serikali kwa fedha hizo zilizotolewa, na hivi karibuni tulipata milioni 300, nasema ahsante kwa Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa maana ya Mwamkulu fedha zilizotolewa zina uwezo wa kujenga OPD. Ni lini Serikali itatuongeza fedha ili tuweze kumalizia majengo mengine?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kituo cha Afya cha Ilembo kilibahatika kupata fedha shilingi milioni 400, lakini fedha zile hazikulenga vifaa tiba. Ni lini Serikali itatusaidia fedha ili tuweze kununua vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukrani nyingi za Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wa Manispaa ya Mpanda ambazo amezielekeza kwa Serikali yetu inayochapa kazi, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan. Na ni kweli, hakuna jimbo ambalo halijapata vituo vya afya na zahanati. Kazi inaendelea na tunaona wananchi wetu wananufaika na miradi hii ya afya.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki cha Afya cha Mwamkulu kimepewa milioni 250, na maelekezo ni kujenga majengo matatu. Jengo la OPD, maabara pamoja na kichomea taka. Kwa hiyo milioni 250 si ya kujenga OPD peke yake, na hiyo ni standard kwa milioni 250 zilizotolewa nchini kote. Awamu ya pili tutapeleka fedha tena kwa ajili ya kikamilisha majengo yaliyobaki yakiwemo wodi, majengo ya upasuaji na majengo mengine muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la vifaa, Serikali imeweka utarartibu, kuanza baada ya kukamilisha miundombinu hiyo, kwa awamu tutapeleka fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba ili kuwezesha vituo vyetu kufanya kazi vizuri zaidi. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana pia nashukuru kwa majibu ya Serikali, ninalo swali moja tu la nyongeza.

Wakati Waziri mwenye dhamana akilisukuma jengo hili, je, Serikali haioni umuhimu wa kuigeuza barabara hii kuwa ya mzunguko au ya pete ili kuepusha Mji wa Mpanda na msongamano wa magari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba hii barabara ni ya mzunguko kwa maana ya ring road ikiunganisha Halmashauri ya Nsimbo, Mpanda Manispaa pamoja na Halmashauri ya Tanganyika. Kwa hiyo, kwa umuhimu huo tunaitambua na ndiyo maana tunai-push zaidi ili iweze kupandishwa hadhi na iweze kuhudumia watu wote kwa wakati wote. Kwa hiyo, jambo hilo Mheshimiwa Mbunge tumelipokea. Ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Reli ya Kaliua – Mpanda ni mbovu na ndiyo maana inasababisha mabehewa nayo kuwa mabovu Serikali inasema nini katika hili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli reli ya kutoka Kaliua – Mpanda ina changamoto, lakini kama Serikali kupitia shirika letu la reli nchini kila mwaka tumekuwa tukitenga fedha kwa ajili ya kukarabati reli hii. Pia habari njema ni kwamba Mheshimiwa Rais ameridhia kwamba kitangazwe kipande hiki cha Kaliua - Mpanda mpaka Karemi ili kiwe standard gauge. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa kipindi hiki ina tatizo kubwa sana la maji. Naishukuru Serikali tuko katika Miji 28 lakini tunacho chanzo kizuri cha Ikorongo kwa kipindi hiki cha shida ya maji, Serikali inasema nini kwa kutu-support ukizingatia upembuzi yakinifu umeshafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa crisis ambayo tuko nayo sasa hivi ya ukame, vyanzo vyote ambavyo tunaviona bado vina maji mengi tunakwenda kuvitumia ili kuhakikisha tunakwenda kupunguza shida ya maji katika jamii zetu. Hivyo nitalichukua hili la chanzo cha Ikolongo na nitaagiza mara moja watu wetu ambao wako Mpanda kuhakikisha wanakifikia hiki chanzo na kuona kinatumika ipasavyo. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kwa maana ya Mradi huu wa TACTIC kilometa 15 Mji wa Mpanda, Soko la Kazima na kilomita 29 kutoka Mwankulu mpaka Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Mpanda ipo katika kundi la pili ambalo kwa sasa mwezi wa Pili huu tulioanza zabuni za kutafuta wataalam washauri zinaanza na utekelezaji wa miradi hiyo kwa wenzetu watu wa Mpanda utaanza mwakani mwezi Aprili, 2024. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Barabara ya Katesi - Iteka inaunganishwa na daraja muhimu katika Mto Mpanda, kwa bahati mbaya daraja hilo limekatika. Je, ni lini Serikali itaongezea fedha TARURA ili walitengeneze daraja hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda pia ni moja ya halmashauri ambazo zimeongezewa bajeti ya barabara. Lakini nimhakikishie kwamba mpango wa Serikali ni kuainisha na tayari nimeshainisha madaraja korofi yote na makalvati ili kuhakikisha tunaongeza fedha za ujenzi wa madaraja hayo yaweze kupitika. Hivyo nawaelekeza TARURA, Mkoa wa Katavi na Manispaa ya Mpanda wahakikishe wanaleta andiko la daraja hili ili TAMISEMI tuweze kuona namna ya kutafuta fedha kwenda kufanya ujenzi wa daraja hilo. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Kwa bahati mbaye, Manispaa ya Mpanda ni kati ya Manispaa zilizopo pembezoni, mwaka jana tulipata walimu sita na watumishi wa afya saba. Serikali inasema nini katika kuinusuru Halmashauri hii na upungufu wa watumishi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wamekuwepo watu ambao wamekuwa wakijitolea kwa muda mrefu bila kuathiri taratibu za ajira, Serikali inasema nini katika kuajiri watu hawa ambao wamekuwa wakijitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Kapufi kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa kuwasemea Wananchi wa Mpanda Mjini na nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaendelea kushirikiana kwa karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie kwamba tunajua mwaka uliopita walipata watumishi hawa sita wa elimu na saba wa afya lakini ukiangalia asilimia ya watumishi kwa Mpanda ni asilimia 69.1 angalia kidogo ukilinganisha na Halmashauri nyingine. Lakini hii haimaanishi kwamba hatutaleta watumishi na ndio maana kwenye ajira hizi za mwaka huu bado Mpanda itapata kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili kwa watumishi wanaojitolea Serikali imeweka utaratibu wa kuwapa kipaumbele watumishi wale ambao wanajitolea kwenye vituo vyetu na shule zetu ili ajira zinapotokea waweze kupata ajira kuwa kipaumbele zaidi, ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni lini Serikali itaanzisha huduma hii ya usafishaji figo katika Mkoa wetu wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwenye hospitali yao mpya ya Mkoa wa Katavi tayari vifaa vimenunuliwa, sasa hivi wako kwenye finishing ya aneo ambalo linatakiwa hivyo vifaa visimikwe halafu huduma hii itaanza mara moja kwenye mkoa wenu wa Katavi. Hata CT- Scan ambayo Rais wetu ameinunua imeshafika.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, Je, ni lini skimu ya umwagiliaji ya Mwamapuli itaanza?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika skimu zaidi ya 42 ambazo tutakwenda kuzijenga katika mwaka wa fedha huu ambao unaishia na ambao unaendelea ni pamoja na Skimu ya Mwamapuli. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo liko ndani ya utekelezaji wa Serikali.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Mwamkulu – Kakese hadi Misunkumilo yenye kilometa 30 kwa kiwango cha lami kupitia TACTIC Awamu ya Pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mwakulu – Kakese ipo katika mpango wa ujenzi wa mradi ule wa TACTIC na hivi karibuni watatangaza kazi ya kuweza kuwapata wale watakaofanya usanifu wa barabara hii na itaanza ujenzi wake kwa vipande. Kwa hiyo, wakipata wale watu wa kwenda kufanya usanifu tutamjulisha Mheshimiwa Kapufi ili naye aweze kushiriki katika zoezi la utiaji saini kama ambavyo tulifanya kwenye miradi mingine ambayo ipo chini ya TAMISEMI.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Je, ni lini Serikali itatusaidia changamoto ya maji katika kata ya Kasokola katika Manispa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Kapufi kwa kweli umekuwa ukifuatilia kata hii na nikuhakikishie katika maeneo ambayo tunakwenda kupeleka jitihada ni pamoja na kata hiyo uliyoitaja kuhakikisjha wananchi nao wananufaika na hekima kubwa anayotumia Mheshimiwa Rais wetu kuhakikisha wanawake tunawatua ndoo kichwani.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Manispaa ya Mpanda nayo ni kati ya Manispaa ambazo zipo kwenye Mradi wa TACTIC. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie na sisi Mpanda ni lini tutaanza Mradi huu wa TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Manispaa ya Mpanda ipo katika Awamu ya Tatu ya Utekelezaji wa Mradi wa TACTIC ambao utaanza mwaka wa fedha 2022/2023, ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru ninalo swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu spika, naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba vijana hawa wamekuwa wakifanya kazi nzuri nafahamu wapo ambao walifanya toka enzi za TRL. Je, Serikali inasema nini katika kuzingatia mafao yao wakati wa kuajiri?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali nipokee hizo pongezi za Mheshimiwa Mbunge na nipende kujibu swali lake la nyogeza kuhusu namna ambavyo Serikali inazingatia hawa vibarua kwa ajili ya maslahi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kusema kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali kupitia Waraka Namba Moja wa mwaka 2004 wa Utumishi wa Umma kwamba anayestahiki ama anastahili kuajiriwa katika ajira za kudumu inatakiwa awe amemaliza kidato cha nne, na hawa kwa kuwa wako darasa la saba na wengine hawajamaliza tunaendelea kuwashawishi na kuwashauri na kupitia Shirika letu la Reli nchini tutaendelea pia kuwaendeleza ili wafikie hicho kiwango na hatimaye kuajiri.