Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Tamima Haji Abass (4 total)

MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali imefanya utafiti na tathmini na kujua kama elimu inayotolewa inatija na inaleta mabadiliko katika jamii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali haioni haja sasa kutumia taasisi za dini kuiandalia programu maalum kwa ajili ya kutoa elimu kusaidia kukinga vitendo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tamima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kupitia MTAKUWA uliomaliza muda wake 2020/2021 uliotolewa kwenye Kikao cha Mawaziri wa Wizara mtambuka kilichofanyika tarehe 26 Januari, 2023 inaonesha kuwa jamii iliyopewa elimu inapata tija kwa jamii na inaendelea kuripoti taarifa za vitendo vya ukatili katika vyombo vya usalama.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali kwa kushirikiana na madhehebu ya dini nchini itaendelea kutekeleza programu ya malezi kwa ajili ya kutoa elimu ya kujikinga na vitendo vya ukatili katika taasisi zote za dini, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; baada ya kutambua sababu za uwepo wa watoto hao, Je, Serikali ina mpango gani? Swali la pili kwa kuwa mikoa iliyofanyiwa utafiti huo ni michache; Je, Serikali ina mpango wa kuendelea na utafiti kama huo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika,napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tamima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na mikakati endelevu kutoa malezi bora kwa wazazi na mafunzo ili kuwatunza watoto katika ngazio ya familia lakini itafanya iwakutanishe watoto hao na wazazi wao. Watoto wasio na wazazi watapata huduma na haki zote stahiki katika vituo vyetu vya watoto tunavyolelea watoto yaani, Kikombo – Dodoma na Kurasini – Dar es Salaam lakini pia tutaimarisha ulinzi na usalama kwa watoto hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali itaendelea kufanya tafiti mbalimbali katika mikoa ambayo inachangamoto za mitaani ili kuhakikisha usalama wao. Lakini pia nitoe rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakaa na familia yao familia za watoto wao ili kuhakikisha wanapata malezi bora. Pia mtoto wa mwenzio ni wako, na watoto wote wanastahili kupewa haki muhimu kwa vile mtoto wa leo ni Taifa la kesho, ahsante. (Makofi)
MHE. TAMINA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya matumaini ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile fedha hizo zitatengwa kwenye bajeti ya mwaka ujao; je, itawasaidiaje askari wanawake ambao wanaishi mbali na vituo vyao vya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imeelezwa, nyumba hizi 14 zitakapokarabatiwa, mgao wa nyumba hizo kwa Askari wetu uzingatie uwiano wa jinsia ili Askari wa kike ambao Mheshimiwa ana mashaka kwamba wanakosa nyumba za kuishi waweze kupata nyumba, nashukuru.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali imejipangaje kutoa uelewa kwa watumishi wanaotarajia kustaafu hasa kuhusu kikokotoo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tamima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeendelea kutoa elimu ya kuhusiana na kikokotoo na kwa msingi huo mifuko yetu imeshirikiana na Chama cha Waajiri (ATE) katika kutoa elimu, lakini pia Shirikisho la Wafanyakazi (TUCTA), lakini pia tumekuwa tukiwafikia hata kwenye makundi kulingana na kada zilizopo za ajira. Kwa hiyo, hata hao ambao ameeleza Mheshimiwa Mbunge tutawafikia na swali la utoaji wa elimu kuhusiana na kikokotoo ni endelevu ili waweze kuona faida ambayo wanaweza kuipata kutokana na kikokotoo hiki kipya, ahsante.